Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ameshiriki mafunzo maalum kwa waandaaji wa maudhui (content creators) yanayofanyika leo Machi 24, 2026 mkoani Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo waandaaji hao wa maudhui ili kuboresha ubunifu na kuongeza tija ya kazi zao.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, huku Wizara ya Nishati ikiwa miongoni mwa wawezeshaji.
Uwezeshaji wa Wizara ya Nishati katika mafunzo hayo ni kielelezo cha kutambua kazi zinazofanywa na waandaaji hao wa maudhui ambao ni daraja muhimu la kutoa elimu na kuhamasisha kupitia majukwaa yao kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mafunzo yanayotolewa leo yanalenga kuwasaidia watengeneza maudhui kuboresha kazi zao kupitia kubiasharisha maudhui mtandaoni (Content Monetization & Sustainability), kujiongezea thamani binafsi na chapa (Personal Branding na Channel Optimization), pamoja na masuala ya hakimiliki.
Aidha, waandaji hao wa maudhui watapata elimu ya namna ya kufikia masoko ya kimataifa, maadili na miongozo ya utoaji huduma mtandaoni, pamoja na usalama wa taarifa binafsi katika utengenezaji wa maudhui.





