Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imepanga kuanzisha kongani za biashara katika kila wilaya nchini kuwasadia Wakulima,Wafanyabiashara na Vijana kuchakata mazao ili kuyaongezea thamani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema mpango huo unalenga kuweka mnyororo wa thamani utakao wanufaisha wakulima na wafanyabiashara, hususan vijana, katika maeneo yao.
Juditha amesema kongani hizo zitawawezesha wakulima na wafanyabiashara, hususan vijana, kunufaika moja kwa moja na uzalishaji katika maeneo yao badala ya kuuza mazao ghafi.
Amesema Serikali inaendelea kuendeleza kongani za viwanda zilizopo sambamba na kuanzisha nyingine katika kila wilaya.
‘’Hatua hii inalenga kuongeza ajira kwa Watanzania wote , kukuza shughuli za viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizochakatwa ndani na nje ya nchi.
Pia Serikali imefanya marekebisho ya sheria takribani 13 katika sekta ya viwanda na biashara, hatua iliyoleta mafanikio makubwa katika kurahisisha taratibu za kuanzisha biashara, kupunguza muda na gharama za kupata leseni, pamoja na kuboresha udhibiti wa vipimo na mizani’’amesema.

Amesema maboresho hayo yamehusisha pia kutoa msaada kwa viwanda vidogo, kuimarisha maeneo ya kimkakati ya kiuchumi, kuongeza majukumu ya Shirika la Utafiti wa Viwanda Tanzania (TIRDO), kupunguza vikwazo vya ushuru, kurekebisha viwango vya kodi na kuboresha mfumo wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Akitoa takwimu za mafanikio ya wizara, Judith amedai katika kipindi cha miaka minne iliyopita usajili wa makampuni umeongezeka kutoka 9,630 hadi 23,365, huku majina ya biashara yakiongezeka kutoka 17,202 hadi 31,123.
Ameongeza kuwa idadi ya alama za biashara imeongezeka kutoka 2,406 hadi 3,148.
Aidha, amedai leseni za biashara daraja A zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zimeongezeka kutoka 11,726 hadi 22,718, huku leseni za viwanda zikiongezeka kutoka 236 hadi 991.
Amesema mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.0 mwaka 2023 hadi asilimia 7.3 mwaka 2024.
Judith amesema ukuaji wa sekta ya viwanda umeongezeka kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 4.8 katika kipindi hicho.
Kwa upande wa sekta ya biashara, amesema mchango sekta ya Viwanda na biashara katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 8.4 mwaka 2023 hadi asilimia 8.6 mwaka 2024, hatua inayotokana na maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara na upanuzi wa masoko.
Kwa upande wa masoko ya nje, Judith amesema Serikali imeendelea kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania katika nchi za Afrika na Ulaya.
Amesema mauzo katika soko la Afrika yalifikia dola bilioni 3.94 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 2023, huku mauzo hayo yakichangiwa zaidi na bidhaa za kilimo.
Amedai mauzo katika soko la Umoja wa Ulaya yameongezeka kutoka dola milioni 633.5 hadi dola milioni 686.3 mwaka 2024.
Judith amesema Wizara inaendelea kuboresha mifumo ya usajili wa leseni
ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na kupunguza changamoto katika ufanyaji wa biashara.

