Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Mkoa wa Njombe, Henry Msambila, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara na watu wote wanaotumia vipimo batili kwa lengo la kuwapunja wakulima, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai linaloadhibiwa kwa faini ya kati ya shilingi 100,000 hadi milioni 20, au kifungo jela.
Msambila ametoa kauli hiyo Agosti 5, 2025, alipokuwa akizungumza katika banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Kuna baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kutumia mizani na vipimo visivyokidhi viwango ili kujinufaisha kwa kuwanyonya wakulima. Tunawaonya, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa kushirikiana na vyombo vya dola,” alisema Msambila.
Aliongeza kuwa, tayari baadhi ya watu walishachukuliwa hatua, huku akisisitiza kuwa zoezi la ukaguzi wa vipimo ni endelevu na linahusisha sekta zote zinazotumia vipimo katika shughuli zao.
Akifafanua kuhusu jukumu la WMA, Msambila alisema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wakulima wanalindwa kupitia matumizi ya vipimo sahihi tangu awali, ikiwemo wakati wa maandalizi ya mashamba, ununuzi wa pembejeo kama mbegu, hadi hatua ya kuuza mazao.
“Tupo hapa kutoa elimu. Tunaeleza namna vipimo vinavyomlinda mkulima kuanzia anaponunua mbegu ambazo zimehakikiwa ujazo wake, hadi anapouza mazao yake,” aliongeza.
Alisema WMA inahakiki pia bidhaa na mazao yaliyovunwa, pamoja na kutoa ushauri kwa wakulima kuhusu matumizi ya mizani sahihi ili waweze kupata faida stahiki katika shughuli zao.
“Tunashauri wakulima wauze kwa kutumia vipimo halali na mizani badala ya kutumia vifungashio batili ambavyo vinaweza kuwapelekea kupata hasara,” alisema.
Kwa upande mwingine, Msambila alisema wakulima wanaoongeza thamani ya mazao yao kupitia vifungashio wanapaswa kuhakikisha ujazo unaozingatia vipimo sahihi ili kuepuka migogoro ya kibiashara na kisheria.
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu shughuli za wakala huo, hasa umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika sekta ya kilimo na biashara.
