Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini Mwa Afrika (World Vegetable Center) kilichopo Tengeru, Arusha, kimesema kuwa kitaendelea kuongoza juhudi za kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo cha mbogamboga hapa nchini na Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia tafiti za kisayansi, ukuzaji wa mbegu bora na uwekezaji katika rasilimali watu.

Kufuatia changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mimea na matumizi ya mbegu duni, kituo hicho kimeweka kipaumbele katika kuzalisha mbegu chotara bora zinazohimili ukame na magonjwa, zikiwemo mboga muhimu kama nyanya, vitunguu, pilipili, kabichi pamoja na mboga za asili zenye virutubisho vya hali ya juu.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya uzalishaji wa mbegu bora kwa mazao yanayohimili magonjwa na ukame yaliyofanyika hivi karibuni katika kituo hicho mkoani Arusha, Dkt. Sognigbe N’Danikou, mtaalamu wa utunzaji na matumizi ya mbogamboga asilia kutoka kituo hicho alisema lengo kuu ni kukuza kizazi kipya cha wataalamu watakaoongoza sekta hiyo kwa kutumia maarifa ya kisayansi.

“Tunajikita katika kufanya tafiti na kuzalisha mbegu bora za chotara zinazoweza kustahimili hali ngumu ya hewa na mashambulizi ya magonjwa, lakini muhimu zaidi ni kuandaa wataalamu wakiwemo wa ndani wenye uwezo wa kusaidia wakulima moja kwa moja,” alisema Dkt. N’Danikou.

Aliongeza kuwa kituo hicho hutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa watafiti, maofisa ugani na wanafunzi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu za kisasa katika uzalishaji wa mbegu, utunzaji wa vinasaba na kilimo endelevu.

“Hatuzalishi tu mbegu, tunazalisha suluhisho. Tunataka wataalamu wakiwemo wa Kitanzania wawe mstari wa mbele katika tafiti na kusaidia wakulima kupata mbegu bora, teknolojia mpya na hivyo kuimarisha maisha yao,” aliongeza Dkt. N’Danikou.

Mbali na tafiti na mafunzo, kituo hicho pia hufanya kazi ya moja kwa moja na wakulima wadogo kuwapatia mbegu bora pamoja na mafunzo ya mbinu bora za kilimo, lengo likiwa ni kuongeza mavuno, kuboresha usalama wa chakula na lishe hasa katika jamii zenye kipato cha chini.

Mbogamboga ni chanzo kikuu cha kipato na lishe kwa mamilioni ya wakulima wadogo, lakini bado sekta hii haijaendelezwa kikamilifu kutokana na ukosefu wa mbegu bora na maarifa ya kisasa.

Hivyo, kituo hicho kinalenga kuziba pengo hilo kwa kuunganisha tafiti za ndani na uzoefu wa kimataifa.

“Ushirikiano wetu na taasisi kama Chuo Kikuu cha Taiwan unatuongezea nguvu, lakini msingi wa mafanikio yetu ni kuwawezesha wataalamu na taasisi za ndani kuongoza mabadiliko haya,” alisema.

Mmoja wa wanaohudhuria mafunzo hayo, Daktari Aloyce Callist Kundy kutoka Benki ya Vinasaba vya Mimea iliyo chini ya Mamlaka ya Viuatilifu na Mimea (TPHPA) amesema Tanzania imekua na mahusiano mazuri na Taiwan katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kwa kufanya tafiti zenye kukuza sekta hiyo hapa nchini.

Naye Magdalena Kiungo, mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela anayesomea uzalishaji wa mbegu bora za kisasa amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo, hasa katika uzalishaji wa mbegu bora zenye kutoa mazao mengi na kuhimili ukame.

Kwa kuzingatia ongezeko la mahitaji ya kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya chakula yenye tija, Kituo cha World Vegetable Centre kimejipanga kuwa kitovu cha ubunifu, utafiti na mafunzo ili kusukuma mbele sekta ya mbogamboga Tanzania na Afrika kwa ujumla.