Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora inaandaa utaratibu mpya wa upatikanaji wa viongozi kupitia mfumo maalum wa Leadership Competency Framework, lengo ni kuongeza msisitizo wa kuwajengea uwezo viongozi wapya na waliopo ili nafasi za uongozi zisigeuke majaribio.

Akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Open University of Tanzania (OUT) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Leadership School, Kibaha , Machi 11, 2026, Xavier Mrope, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais–Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, alieleza kutokana na dunia kuwa ya ushindani na matumizi ya mifumo ya tathmini ya uongozi, taifa linahitaji viongozi walioandaliwa.

Hata hivyo, Serikali inaendeleza utamaduni wa kuchuja na kupima uwezo wa viongozi si kwa kuangalia vyeti pekee bali pia haiba ya uongozi, uwezo wa kufanya maamuzi, maadili, usimamizi wa migogoro na uwezo wa kuongoza mabadiliko.

Xavier aliongeza kuwa, ubunifu na mabadiliko ya kidijitali ni eneo muhimu ili taasisi mbalimbali ziwe za kisasa na zenye ufanisi.

“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kama taasisi yenye mtandao mpana na jukumu la kitaifa la kufikisha elimu kwa jamii kina nafasi ya kipekee kuonyesha kwamba ubunifu wa kidijitali unaweza kuongeza tija,” alisisitiza Xavier.

Akizungumzia matarajio ya mafunzo hayo, Kaimu Makamu Mkuu wa OUT, Harieth Hellar-Kihampa, alisema mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika kuanzia Machi 11 hadi 14, 2026 yakihusisha washiriki 75, na yanalenga kuwajengea uwezo wakiwemo viongozi wapya, wakuu wa idara ili kuongeza ufanisi kazini.

Alieleza OUT ilianzishwa mwaka 1992 kwa Sheria ya Bunge Na. 17 kwa lengo la kupanua upatikanaji wa elimu ya juu kwa Watanzania kupitia mfumo wa elimu ya masafa na hivyo kuongeza wataalamu na rasilimali watu nchini.

Nae Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa OUT anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Paul Kwaba, alieleza chuo hicho kwa sasa kina vituo 26 katika mikoa ya Tanzania Bara vinavyotoa huduma mbalimbali huku mpango ukiwa kufikia ngazi ya wilaya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Leadership School, Marcellina Chijoriga, Meneja Taaluma John Baitan alieleza shule hiyo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ikiwemo uzalendo, uongozi wa kimkakati, utawala bora, uadilifu, usimamizi wa miradi, falsafa ya ukombozi pamoja na ubunifu na mabadiliko ya kidijitali ili kuongeza tija na kupanua huduma kwa Watanzania.