Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mgombea Ubunge Jimbo la Temeke kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP) Yusuph Rai amesema kuwa endapo wananchi watampa dhamana ya kuwa Mbunge atahakikisha Jimbo hilo linapiga hatua kubwa kimaendeleo tofauti na Majimbo mengine yaliyopo Mkoani Dar es Salaam.

Rai amesema hayo leo Agosti 19,2025 wakati akichukua fomu ya uteuzi wa kugombea Jimbo la Temeke kutoka Ofisi ya Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Temeke Fortunata Shija.

“Tunafahamu Majimbo ya Dar es Salaam changamoto zake zimekua sio kubwa kama maeneo mengine ukweli ndo huo, unapozungumzia barabara,Dar es Salaam ndio sehemu ambayo ina barabara nyingi zaidi,ukizungumizia vituo vya afya imekua kama sehemu ya mfano(Sample) ya kila kitu kwenye nchi hii. ” amebainisha Rai.

Hata hivyo amesema amewiwa kuomba nafasi ya Ubunge Jimbo la Temeke, kwa sababu anatafsiri Temeke kama ndio Jimbo pekee katika Mkoa wa Dar es Salaam ambalo linatakiwa liwe tofauti na majimbo mengine,uhalisia wa sasa ukiangalia anaona kabisa Temeke ni kama dampo katika Majimbo yote ya Mko wa Dar es Salaam,huwezi kufananisha na majimbo ya Kinondoni,Ilala,Kawe,Kibamba na mengine.

Aidha amesema kuwa Temeke ina rasilimali za kutosha,wawekezaji,Makampuni mbalimbali,wafanyabiashara,pamoja na vitu vya msingi vinavyotafsirika kama vya Kitaifa ikiwemo Uwanja wa Taifa, Uwanja wa Sabasaba ambazo ni sehemu ya mapato yanayoenda Serikali kuu,hivyo lazima watu wa Temeke waweze kunufaika hata kwa asilimia moja.

“Mkimpeleka Mbunge wa karibu na Nyie ataenda kusema zile fursa mbalimbali ambazo zinatakiwa zitokeze kwa Vijana,Wanawake,Watu wenye ulemavu na jamii nyingine,niweze kuwambia Temeke kunahitaji moja mbili,tatu lakini pia kuwashawishi matajiri na wafanyabiashara wanapowekeza kwenye Jimbo la Temeke wawaangalie Vijana au watu wanaoishi kwenye Temeke yao.”

Aidha amesema kuwa pindi atakapoteuliwa ataanza mchakamchaka wa kuwafikia Wananchi katika kata zote 13,pamoja na mitaa yote,huku akiwa na imani kuwa Wananchi watampokea vizuri kwasabubu haendi kumtukana mtu,bali anaenda kueleza Ilani ya Chama Chake Cha AAFP endapo kikitapata dhamana ya uongozi kitawafanyia nini Wananchi wa Jimbo la Temeke.

“Nataka niwambie kwamba naenda kutoa nywira(password) kwa Watanzania wajue ni kwa nini chama chetu cha Wakulima AAFP makao Makuu yake yalikua Temeke,Temeke niya kwetu,tupo tayari kupambana usiku na mchana barabara na chochoro zote kuwafikia watu wote na kuhakikisha Temeke mwaka huu wanapata mbunge mwenye kiu ya kutatua kero za Wananchi.