📌Kunufaisha Kaya 3,960 kutoka katika Vitongoji 120 ndani ya Wilaya Tano
📌Vitongoji 15 katika kila Jimbo la uchaguzi kunufaika
📌RC Dendego amshukuru Rais Samia na aipongeza REA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha vitongoji vyote vilivyosalia vinapatiwa umeme
Na Mohamed Saif, JamhuriMedia, Singida
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 17.39 wa kusambaza umeme katika vitongoji 120 utakaonufaisha Kaya 3,960 Mkoani Singida.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amebainisha hayo Mei 14, 2025 Mkoani Singida wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya M/s Transpower Limited na Whitecity International Contractor Ltd JV kwa Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego.
“Tunamshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 17,394,214,690.85 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 120 Mkoani hapa, leo hii tumefika hapa kumtambulisha Mkandarasi na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” alisema Mhandisi Olotu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoani humo hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa maendeleo ya jamii.
“Ninayo furaha kubwa leo hii kumpokea mkandarasi huyu kwani kama mtakumbuka Serikali iliahidi ifikapo 2025 itakuwa imekamilisha kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara na sasa tumeshuhudia kabla hata ya 2025 vijiji vyote vilikuwa vimefikiwa na umeme na sasa tunatekeleza vitongojini,” alisema Mhe. Dendego.
Mhe. Dendego aliipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza miradi yake kwa ufanisi na uwazi na pia alimpongeza mkandarasi kwa ahadi yake aliyoitoa ya kukamilisha mradi huo kwa miezi 12 badala ya 24 kama ilivyo katika mkataba wake.
“Nimefarijika, tumepata mkandarasi mzuri kwani ametuahidi hapa atakamilisha kazi ndani ya miezi 12 nasi tutampatia ushirikiano na tutamsimamia ipasavyo ili ahadi hii ikamilike kwa kupata mradi bora,” alisema.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika vitongoji Mkoani humo, Mhandisi Olotu alisema kati ya vitongoji 2,289 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 1,052 vimefikishiwa umeme na kwamba vitongoji 120 vitakavyopata umeme awamu hii vitaongeza idadi ya vitongoji vitakavyokuwa na umeme Mkoani humo.
Alisema mradi unatekelezwa katika vitongoji vya Wilaya za Singida DC, Ikungi, Manyoni, Mkalama na Iramba na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kusambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Kwa mujibu wa mkataba, mradi huu unapaswa kutekelezwa ndani ya miezi 24 lakini mkandarasi ametuahidi na kutuhakikishia kuwa ndani ya kipindi cha miezi 12 atakuwa amekamilisha mradi,” alibainisha Mhandisi Olotu.
Kwa upande wake Meneja Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena alisisitiza kuwa umeme ni hitaji la muhimu na kwa kutambua hilo Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa.
“Serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya kusambaza umeme kote nchini, wito wetu kwa wananchi ni kuwapa ushirikiano wakandarasi na kuwa walinzi wa miundombinu hii,” alisisitiza Mhandisi Lwena.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi ambaye ni Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Transpower Ltd, Mhandisi Jackline Mushi aliahidi kufanya kazi kwa weledi na kukamilisha mradi kwa muda mfupi na kwa ubora unaopaswa.
