Zaidi ya vijana 1,990 wa Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara, wamenufaika na awamu ya kwanza ya Programu ya Mining For A Brighter Tomorrow (MBT) inayotekelezwa katika eneo la Nyamongo, ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Sekta ya Madini.

Kupitia programu hiyo, jumla ya leseni 106 za uchimbaji madini zimetolewa kwa vikundi 53 vinavyowajumuisha wanufaika 1,998. Sambamba na hilo, vijana hao wamepatiwa mafunzo mbalimbali yanayohusu uchimbaji salama wa madini, Sheria ya Madini, usimamizi wa fedha, ushirikiano kazini, afya na usalama pamoja na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza na wanufaika wa programu hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Programu ya MBT ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya kwa walengwa. Amewahimiza vijana kuwa wavumilivu, kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia Sheria na taratibu za uchimbaji madini ili kujenga maisha bora na endelevu.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa mnamo Mei 3, 2025, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alikabidhi rasmi leseni 106 kwa vikundi 53 vya wachimbaji wadogo kutoka vijiji 13 vinavyozunguka Mgodi wa Barrick–North Mara. Aidha, wanufaika hao waliwezeshwa mafunzo ya utekelezaji bora wa shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia tija, usalama na uhifadhi wa mazingira.

Ameongeza kuwa, baada ya uzinduzi wa awamu ya kwanza ya MBT, Serikali imejipanga kutekeleza awamu ya pili ya programu hiyo itakayolenga kufanya utafiti kwenye leseni za program ya MBT, kuwawezesha vijana zaidi kwa kuwapatia mitaji, vifaa vya kisasa vya uchimbaji pamoja na kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na usalama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuanzisha Programu ya MBT ambayo amesema imeleta mabadiliko chanya kwa vijana wa Tarime. Amesema programu hiyo imewawezesha vijana wengi kumiliki leseni halali, kujipatia kipato na kuachana na vitendo vya uvamizi na uchimbaji katika maeneo ya leseni ya mgodi wa Barrick-North.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uendelezaji Wachimbaji Wadogo, Mhandisi Moses Kongola, amesema Wizara ya Madini imeendelea kutekeleza programu ya mafunzo kwa wachimbaji wadogo nchi nzima kwa lengo la kuwajengea uelewa katika uchimbaji, uchenjuaji wa madini, utunzaji wa mazingira pamoja na masuala ya afya na usalama kazini.

Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Hamad Kallaye, Mkoa huo umefanikiwa kukusanya maduhuli ya Serikali kiasi cha shilingi 133.34 sawa na asilimia 63.5 ya lengo la mwaka wa fedha, hali inayoonesha ukuaji na uimara wa Sekta ya Madini mkoani humo.

Awali, Dkt. Kiruswa alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Mara kwa lengo la kusikiliza taarifa za utekelezaji wa shughuli za madini pamoja na changamoto zinazowakabili ambapo amewapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri wanayoifanya, hususan katika ukusanyaji wa maduhuli na usimamizi wa shughuli za madini, na kuahidi kushughulikia changamoto ikiwemo upungufu wa watumishi.

Aidha, amewataka kuongeza bidii, ubunifu na uzalendo katika kusimamia sekta ya madini ili mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa uendelee kuimarika.

Programu ya MBT inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kiuchumi, hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum, ambapo uzinduzi rasmi wa programu hiyo unatarajiwa kufanyika Februari 2026.