Na Mwandishi Wetu
KUNDI la pili la wanafunzi 100 wanatarajia kuondoka wiki ijayo kusoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchi za nje mwaka huu wa masomo kupitia Wakala wa Vyuo Vikuu Nje ya nchi Global Education Link (GEL).
Wanafunzi hao waliagwa katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za GEL jijini Dar es Salaam ambapo walipewa nyaraka mbalimbali tayari kwa safari hiyo zikiwemo hati na tiketi za ndege.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel aliwataka wanafunzi hao kwenda kuchukua maarifa kwenye vyuo hivyo na kurudi kuyatumia kwa manufaa ya taifa lao.
“Wazazi watakuwa na furaha utakapotimiza lengo lililokupeleka kule na kwa wakati kwa hiyo mwende kusoma mpate matokeo mazuri ili muwape furaha wazazi wenu ambao wanajinyima kwaajili ya elimu yenu kwa hiyo msiwaangushe,” alisema
Mollel alisema GEL imekubaliana na Bodi ya Utalii nchini (TTB), kuendelea kushirikiana kutangaza utalii na kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye maeneo mbalimabli nchini.
Alisema ushirikiano huo utahusisha vijana wa Kitanzania wanaopata fursa za kusoma nje ya nchi kupitia taasisi ya Global Education Link ambapo vijana watafundishwa kuhusu vivutio vya utalii na nyanja za uwekezaji zilizopo nchini,.

Alisema elimu watakayopewa itawasaidia wanapokuwa masomoni nje ya nchi wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kimataifa.
Akizungumza na wanafunzi katika kikao hicho, mwakilishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nassoro Garamatatu, aliwashauri wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi na kuitangaza Tanzania kwa mazuri yake na kuzingatia maadili ya nchi.
Alisema Tanzania ina mazingira mazuri yenye vivutio vingi vya utalii kwenye mbuga mbalimbali kama Mikumi, Serengeti, Ngorongoro Manyara hali ambayo italiingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
“Mkiwa nje ya nchi lazima mtapata marafiki wanaotoka kwenye familia tajiri ambazo huwa zinasafiri mara kwa mara kwenye maendeo mbalimbali duniani nyinyi mnawajibu wa kuwashawishi waje hapa Tanzania,” alisema.

“TTB tunaahidi kuwa ipo siku tutaandaa safari ili tuwapeleke mkatembelee vivutio vya utalii, sisi tunaamini mkifahamu vizuri kuhusu utalii uliopo nchini mtaweza kufanya vizuri kwenye kuitangaza nchi yenu huko mnakoenda,” alisema
Hilo ni kundi la pili la wanafunzi wanaelekea masomoni nje ya nchi kwa mwaka wa masomo 2025/2026 katika vyuo vikuu mbalimba nje ya nchi zikiwemo China, India, Malaysia, Cyprus, Uturuki, Uingereza na Poland.


