ZAIDI ya watu milioni 14 wanaoishi kwenye mazingira magumu zaidi duniani huenda wakafariki baada ya utawala wa Rais Donald Trump kupunguza misaada.

Utafiti uliochapishwa leo na Jarida la tiba la Lancet unakadiria kuwa miongoni mwa watu hao, theluthi moja ni watoto wadogo.

Kulingana na watafiti wa kimataifa, ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Marekani, USAID uliepusha vifo milioni 91 katika nchi zinazoendelea kati ya mwaka 2001 na 2021.

Lakini kupunguzwa kwa misaada kunaweza kusababisha vifo zaidi ya milioni 14 vinavyoweza kuepukika ifikapo 2030.

Utafiti huo umechapishwa huku viongozi wa dunia na wafanyabiashara wakikusanyika kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa nchini Uhispania wakitumai kuimarisha sekta ya misaada inayoyumba.

Shirika la Marekani la Maendeleo (USAID) lilikuwa linatoa zaidi ya asilimia 40 ya ufadhili wa kibinadamu duniani hadi Trump aliporejea Ikulu ya Marekani mwezi Januari.