Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kwamba raia wa Zambia na Malawi sasa watatakiwa kulipia dhamana ya dola 15,000 ili kuweza kuingia nchini Marekani kwa vibali vya biashara ama utalii.

Uamuzi huo unaanza kutekelezwa tarehe 20 Agosti kama sehemu ya mradi wa majaribio unaodhamiria kupunguza idadi ya wageni wanaoamua kubakia nchini ya Marekani hata baada ya vibali vyao kumalizika muda.

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Tammy Bruce, dhamana hiyo itarejeshwa kwa muombaji, pale atakapokuwa ametimiza masharti ya kibali chake cha kuingia Marekani.

Malawi na Zambia ni miongoni mwa mataifa masikini barani Afrika na ni nadra kwa raia wake kuitembelea Marekani.

Utawala wa Trump umekuwa kwenye kampeni kubwa ya kupambana na kile unachosema ni uhamiaji haramu.