.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa akimshinikiza vikali katika kujaribu kupata suluhu ya vita vya karibu miaka minne akisema ni jukumu la Kyiv kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanikiwa.

Zelensky, katika mahojiano na tovuti ya Marekani ya Axios yaliyochapishwa Jumanne, pia alisema mpango wowote unaoitaka Ukraine kutoa eneo ambalo Urusi haijaliteka katika eneo la mashariki mwa Donbas utakataliwa na Waukraine ikiwa utapigiwa kura ya maoni.

Axios alimnukuu Zelensky akisema “sio haki” Trump kuendelea kutoa wito hadharani kwa Ukraine, wala si Urusi, kufanya makubaliano katika kujadili masharti ya mpango wa amani.

“Natumai ni mbinu zake tu na sio uamuzi,” Axios alimnukuu Zelensky alisema katika mahojiano hayo yaliyofanywa kwa simu wakati wapatanishi wa Urusi, Ukraine na Marekani walipokuwa wakizungumza mjini Geneva.

Trump amependekeza mara mbili katika siku za hivi karibuni kwamba ilikuwa ni jukumu la Ukraine na Zelensky kuchukua hatua ili kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanikiwa.

“Ni vyema kwa Ukraine ije katika meza ya mazungumzo haraka. Hayo ndiyo ninayokuambia,” Trump aliwaambia waandishi wa habari ndani ya Air Force One siku ya Jumatatu.