Kauli ya Rais Volodymyr Zelensky kwamba Rais Vladimir Putin hana nia ya kushiriki katika mazungumzo ya kusitisha mapigano amekuwa akiirudia mara kwa mara tangu kuanza kwa vita vya Ukraine mwaka 2022.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema haoni dalili yoyote kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin yuko tayari kushiriki katika mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea.

Katika hotuba yake ya jioni kupitia njia ya video, Zelensky ameeleza kwamba Marekani ilisema wiki mbili zilizopita kuwa Moscow ilipaswa kuwa tayari kufikia sasa kuandaa mkutano wa ngazi ya viongozi.

Hata hivyo, kiongozi huyo amesema badala ya kuonyesha nia ya mazungumzo, “kitu pekee ambacho Urusi inachokifanya ni kuwekeza zaidi katika vita.”

Akizungumzia kuhusu ziara ya Putin nchini China, Zelensky amemshtumu kwa mara nyingine kwa kujaribu kukwepa mazungumzo ya kuvimaliza vita hivyo akisema “huo ndio mchezo wake namba moja.”

Licha ya matarajio ya Marekani ya kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja kati ya viongozi hao wawili – Putin na Zelensky, Urusi hadi sasa haijaonyesha utayari wa kushiriki mazungumzo hayo. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov hivi karibuni aliweka bayana kwamba Putin amekataa kuzungumza na Zelensky, akitilia shaka uhalali wake kama rais wa Ukraine.