Rais Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo ya pande tatu kuhusu kumaliza vita nchini Ukraine yatafanyika kati ya Ukraine, Urusi na Marekani katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), baada ya kukutana na Rais Donald Trump huko Davos.
Wakati juhudi za kidiplomasia zikionekana kuongezeka kasi, Trump alisema kuwa mkutano wake na Zelensky ulikuwa mzuri, huku mjumbe wa Marekani Steve Witkoff akielekea Moscow kwa mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Witkoff, aliyekuwa akisafiri kwenda Moscow akiwa na mkwe wa Trump, Jared Kushner, alisema ana matumaini makubwa kuhusu kufikiwa kwa makubaliano.
“Nadhani tumebakiza suala moja tu, na tayari tumejadili njia mbalimbali za kulitatua, jambo linalomaanisha linaweza kutatuliwa,” alisema kabla ya kuondoka katika eneo la mapumziko la Uswisi.
Mjumbe wa Trump hakutoa maelezo kuhusu suala lililobaki kuwa kikwazo, lakini baadaye Zelensky alifafanua kuwa hali ya baadaye ya mashariki mwa Ukraine bado ndiyo hoja ambayo haijapatiwa suluhu.
Alibainisha wazi kuwa mazungumzo yaliyopangwa kufanyika katika Falme za Kiarabu yataihusisha Urusi pamoja na Marekani na Ukraine, akiongeza kuwa “Warusi wanapaswa kuwa tayari kwa maridhiano, si Ukraine pekee.”
“Yote yanahusu ardhi. Hili ndilo suala ambalo bado halijatatuliwa,” Zelensky aliwaambia waandishi wa habari katika Jukwaa la Kiuchumi Duniani (World Economic Forum) huko Davos, Uswisi, akiongeza kuwa mazungumzo ya pande tatu yanaweza kutoa “mbinu mbalimbali” kwa pande zote mbili.
Pendekezo la Marekani kuhusu eneo la Donbas, kitovu cha viwanda cha Ukraine, ni kuanzishwa kwa eneo lisilo na wanajeshi na lenye uhuru wa kiuchumi, kwa kubadilishana na dhamana za usalama kwa Kyiv.
“Ikiwa pande zote mbili zinataka kutatua hili, basi tutalitatua,” Witkoff alisema, akieleza kuwa baada ya Moscow ataelekea Abu Dhabi, ambako vikundi kazi vitashughulikia masuala ya kijeshi pamoja na ustawi wa kiuchumi.

