Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameituhumu Urusi kwa kutaka kuleta machafuko barani Ulaya kwa kutumia droni kwa ajili ya hujuma na kuvuruga hali ya usalama.

Katika hotuba yake ya jioni ya Jumanne kwa njia ya video, Zelensky amesema serikali ya Moscow inatumia kile alichokiita “msafara wa kivuli” si tu kufadhili vita kupitia usafirishaji wa mafuta kwa meli kubwa, bali pia kwa hujuma na juhudi mbalimbali za kuvuruga utulivu barani Ulaya.

Kurushwa kwa droni kutoka kwenye meli hizo ni mfano mmoja wa hali hiyo. Hata hivyo taarifa rasmi kuhusu asili ya droni zilizogunduliwa hivi karibuni katika mataifa kama Denmark na Ujerumani bado hazijathibitishwa.Na Urusi imekanusha kuhusika kwa namna yoyote.

Dmitry Medvedev, naibu mkuu wa baraza la usalama la taifa la Urusi, alionesha kuwa huenda majeshi ya Ukraine yenyewe ndiyo yanayotumia droni hizo kwa makusudi ili kuichochea Ulaya iingie vitani dhidi ya Urusi.