Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema hakitasusia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 badala yake kitashiriki kikamilifu zoezi hilo kwasababu ni haki yao ya kikatiba .
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara wa chama hicho cha ACT Wazalendo uliyofanyika katika jimbo la Mtwara, Kiongozi Mkuu Mstaafau wa chama na Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi wa ACT Zitto Kabwe watu wa mtwara wasisikilize hadithi za kususia uchaguzi kwasababu kuna madhara.
‘’Watu wa mtwara tunawaomba msisikie hadithi za kususia uchaguzi, tufanye maamuzi sahihi ya kuingia kwenye uchaguzi’’amesema Zitto.
Mbali na hilo ameitaja moja ya sera ya chama hicho kitapoingia madarakani ikiwemo kuhakikisha kinaboresha mazingira ya kiuchumi kupitia rasilimali ya Gesi Asilia iliyopo nchi jirani ya Msumbiji pamoja na Tanzania ili wananchi wahangaike kutafuta kipato kitachowezesha kukuza uchumi wao.
‘’Ukiboresha mazingira ya kiuchumi kati ya nchi zetu hizi mbili watu watahangaika kutafuta kipato chao kwasababu fursa za kiuchumi zipo, tunataka kufainya mtwara iwe kituo cha huduma kwa ajili ya Gesi Asilia upande wa Tanzania na upande wa Msumbiji na hiyo ndiyo sera ya ACT Wazalendo’’amesisitiza Zitto
Ameongeza kuwa, ‘’Sisi tunataka kuigeuza mtwara kuwa kituo cha huduma za kibiashara kati yetu na Msumbiji maeneo yenye Gesi Asilia ili vijana wapate ajira, uchumi mzunguko uongezeke’’
Naye Waziri Kivuli wa Uchukuzi wa ACT, Halima Nabalang’anya amesema lengo la kufanya mkutano huo ni kuwaambia wananchi lengo la chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu huo kwani ni haki yao ya msingi na ya kikatiba.


