GMO yafyekelewa mbali

Wananchi wadau wa kilimo wameupokea kwa shangwe na nderemo uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku majaribio ya uhandisijeni yanayofanyika kwenye vituo vya utafiti nchini.

Novemba 21, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, aliiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kusitisha mara moja utafiti huo nchini kote.

 Uhandisijeni, yaani Genetic Modified Organism (GMO), ni utafiti wa kisayansi unaolazimisha wakulima maskini kununua mbegu kwa bei ghali kutoka kwa kampuni za kibepari zinazopigiwa upatu na mataifa yaliyoendelea.

Katibu Mkuu huyo aliielekeza TARI kuhakikisha mabaki yote ya majaribio ya GMO yanateketezwa mara moja. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya taasisi hiyo kuanza kutoa matokeo ya utafiti bila kupata idhini ya serikali.

Siku za hivi karibuni TARI kupitia kituo cha Makutupora mkoani Dodoma imekuwa inaalika watu mbalimbali kwenda kuona matokeo ya utafiti wakati serikali haijaruhusu matumizi ya uhandisijeni nchini.

Kwa wiki kadhaa JAMHURI limechapisha barua na makala ndefu zikieleza athari kubwa za kukubaliwa kwa teknolojia hiyo nchini. Baadhi ya barua na makala hizo ziliandikwa na wasomi; Dk. Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (JAMHURI Toleo Na. 372) na Dk. Yahya Msangi (JAMHURI, Toleo Na. 373).

Dk. Mbunda anasema: “Sababu mojawapo ya kukataliwa GMOs inatokana na athari zake katika mazingira. Kwa mfano, katika utafiti uliofanywa na mwanazuoni John Paul na kuchapishwa mwaka huu wa 2018, ikiwa na kichwa: Genetically Modified Organisms (GMOs) as Invasive Species unaonyesha kuwa GMOs ni viumbe vamizi. Huharibu mazao asilia, mimea mingine, wanyama na kuleta athari katika mazingira ya viumbe hai.

“…Kupotea kwa mbegu zetu [kutokana na kuingiliana na mbegu za GMOs] kutatufanya tuwe watumwa wa makampuni ya mbegu. Mheshimiwa Rais, naamini umefuatilia habari kuhusu Kampuni ya Monsanto, ambayo sasa imenunuliwa na Kampuni ya Bayer ya Ujerumani kwa zaidi ya Sh trilioni 120 (USD 62 bn). Monsanto imekuwa ikipigwa vita hasa Amerika ya Kusini kwa namna ilivyotaka kuwafanya watu wake watumwa wa chakula. Pale ambapo tutapoteza mbegu zetu za asili au tulizoziendeleza muda mrefu kupitia taasisi zetu za utafiti, tutakuwa tumekubali kuwa mateka.”

Wasomaji wengi kwenye mitandao ya kijamii wamepongeza uamuzi wa serikali wakisema unalenga kuliokoa taifa, hasa wakulima wadogo ambao ni wengi.

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) umetoa tamko la kuunga mkono hatua ya serikali ya kuzuia majaribio ya mbegu za mahindi zilizobadilishwa vinasaba kwa njia ya uhandisijeni kupitia mradi wa WEMA.

MVIWATA wamesema: “Hatua hii imekuja kwa wakati muafaka ambapo tumeshuhudia kuongezeka kwa kasi kwa harakati na propaganda za kuupotosha na kuuaminisha umma kwamba mahindi yaliyobadilishwa vinasaba kwa njia ya uhandisijeni ni suluhisho la usalama wa chakula kwa taifa letu kutokana na uwezo wake wa kukabiliana na ukame na wadudu.

“Marufuku hii ya serikali imetolewa wakati kuna taarifa kwamba Serikali ya Afrika Kusini imekataa maombi ya leseni ya kuzalisha na kusambaza kibiashara mbegu za mahindi za WEMA (MON 87460X MON 89034 X NK 603) baada ya kuthibitisha kwamba takwimu za utafiti wa miaka mitano zimeshindwa kuthibitisha madai kwamba mbegu hizo zinakabiliana na ukame kama inavyodaiwa wakati hapa kwetu ni mbegu hizo hizo zimekuwa zikipigiwa chapuo la nguvu na watafiti wetu kwamba ni suluhisho la ukame na wadudu waharibifu.

“Hakuna shaka yoyote kwamba mradi wa mahindi yaliyobadilishwa vinasaba wa WEMA hauna masilahi yoyote kwa wakulima wala taifa kama inavyodaiwa, bali ni kwa masilahi ya makampuni yaliyobuni na yanayomiliki teknolojia hiyo, yaani Bayer ambayo ni mmiliki wa Kampuni ya Monsanto.

“Kwa kuelewa kwamba mradi wa uhandisi jeni wa WEMA na majaribio mengine ya aina hiyo yanayoendelea nchini si kwa masilahi ya wakulima wala taifa, sisi kama wakulima tumekuwa mstari wa mbele kuishauri serikali yetu kutoruhusu mbegu zilizobadilishwa vinasaba kutumika nchini, ikiwemo kuwasilisha pingamizi rasmi la kutaka majaribio hayo ya WEMA yasipewe kibali na serikali.

“Ni dhahiri kwamba mradi huo wa mazao ya uhandisijeni wa WEMA ni sehemu ya mtandao wa kidunia wa kutengeneza utegemezi wa mbegu kwa masilahi ya kibiashara ya makampuni yaliyobuni na kumiliki teknolojia na jeni inayotumika katika mbegu hizo huku wakulima wakifukarishwa.

“Kwa hiyo, marufuku ya serikali ya kusitisha majaribio ya mahindi ya WEMA kwa mara nyingine inathibitisha dhamira ya kimapinduzi ya serikali yetu ya kujinasua katika mfumo wa kiuchumi wa kibeberu sambamba na hatua ya awali ya kutunga sheria ya madini inayohakikisha kwamba taifa letu linanufaika na masilahi ya rasilimali.

“Propaganda na kampeni kubwa za watafiti wakisaidiwa na baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wao za kuuaminisha umma juu ya uzuri wa mbegu za mahindi zilizobadilishwa vinasaba ilikuwa ni uthibitisho wa wazi wa msemo wa Kiswahili kwamba ‘Chema chajiuza, kibaya chajitembeza’. Hatukuwa na shaka yoyote kwamba hatimaye ukweli ungesimama na kushinda licha ya propaganda iliyokuwa inaendelea.

“Tumejiuliza fedha za kuendesha kampeni hii kubwa zinatoka wapi na kama kuna mapenzi ya dhati kwa taifa letu kwa nini wafadhili hao wasielekeze fedha hizo katika kuendeleza mbegu zilizo rafiki kwa wakulima wa Tanzania na ambazo hazitawafanya wakulima wa Tanzania kuwa watumwa na wategemezi kwa makampuni ya nje au pia katika miradi mikubwa ambayo taifa limeichagua kama kipaumbele chake, hususan ujenzi wa reli na mradi wa kufua umeme wa Stigler’s Gorge.

“Tunaishauri serikali ipanue marufuku hii kwa tafiti nyingine zote zinazohusu mbegu zilizobadilishwa vinasaba na kwa vyakula vyote vya binadamu vinavyotokana na mazao yaliyobadilishwa vinasaba, ambapo licha ya sheria kuzuia usambazaji wake kabla ya kupata kibali kutoka National Biosafety Focal Point (NBFP) bado tunashuhudia vipo kwa wingi madukani.

“Sambamba na hilo, tunapenda kuchukua fursa hii kuipongeza serikali, hususan Rais John Magufuli kwa hatua yake ya kuamuru serikali inunue korosho. Tunaungana na wanachama wenzetu, wakulima wa korosho nchini hususan katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani katika kutoa shukrani za dhati kwa hatua hii ambayo inarejesha matumaini kwa wakulima wavuja jasho ambao aghalabu wamekuwa hawanufaiki na jasho lao. Ni matumaini yetu kwamba serikali itatafuta ufumbuzi wa kudumu wa masoko kwa mazao ambayo bado yana changamoto kubwa ya masoko.

“Mwisho, tunatambua na kuunga mkono mwelekeo mpya na jitihada zinazofanywa na serikali za kutambua umuhimu wa wakulima na wafanyakazi katika kujenga uchumi wa taifa letu,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa MVIWATA, Abdul Gea.