Licha ya ukweli kuwa uoto wa asili wa Kisiwa cha Mafia unafanana kwa kiasi kikubwa na uoto wa asili wa visiwa jirani vya Pemba na Unguja na maeneo ya Bara yaliyopo jirani kama Kisiju na Rufiji, watafiti Rogers na Greenaway (1988) waliokuwa wakidurusu uoto wa Kisiwa cha Mafia walishangazwa mno na kiwango kikubwa cha upekee (endemism) wa mimea ya kisiwa hiki.

Waligundua mimea minne isiyopatikana pengine popote duniani isipokuwa Mafia (Complete Endemic to Mafia Island). Mimea hiyo ni Oldenlandia aegialodes, Xyris parvula, Spermacoce species na Eriocaulo ciliipetalum.

Mimea mingine mitatu ikiwa karibu kuwa ya kipekee (near endemic) nayo ni Tristemma schliebenii na Diospyros mafiensis (mkuremba) ikipatikana Mafia na maeneo jirani ya Bara. Mti mwingine ni Philippia mafiensis (mchati) uliokuwa ukipatikana Mafia na Pemba pekee.

Uwepo wa mti wa mchati (Philippia mafiensis) kisiwani Mafia kuliwastaajabisha kidogo, hii ilitokana na ukweli kuwa miti mingi katika familia ya Eracaceae (family eracaceae) inapatikana katika maeneo ya milima na sehemu za baridi kali zenye mwinuko wa mita 2,700 kutoka usawa wa bahari. Ni mchati pekee katika family eracaceae unaopatikana maeneo ya pwani tambarare, tena Bahari ya Hindi.

Kwa mara ya kwanza mchati ulitambuliwa na kupangwa (verified and classified) na Greenaway mwaka 1948 baada ya kuwa umerekodiwa Kinazini – Pemba (1679, 1981) na maeneo tofauti kisiwani Mafia. Kwa kawaida mchati hukua kama kichaka (shrub) cha mashina mengi na hukua kufikia urefu wa mita 1-5. Lakini baadhi ya sehemu zenye rutuba huweza kufika urefu hadi wa mita 8. Majani ya mchati ni madogo, yenye ukubwa wa milimita 0.5-4.5 na hutoa maua madogo yanayokaa kwa vishada na kila kishada kina maya kati ya 7 mpaka 15.

Mchati hukua katika maeneo yasiyo na rutuba nyingi, yanayohusisha udongo wa kichanga. Hadi mwaka 1988 mchati ulikuwa umeenea na kuchukua ardhi kubwa katika maeneo ya Kilindoni, Dongo mpaka Ras Mbizi, kisiwani Mafia.

Wakati kuna taarifa kuwa mchati ulishamalizika Kinazini – Pemba na haupo tena, huku Mafia mchati unaelekea kufutika kabisa. Maeneo yaliyokuwa na mchati Kilindoni yote yamekuwa makazi ya watu na mchati kufyekwa kuanzia Mabati mpaka Suni Kigamboni kuelekea Dongo. Licha ya kuwa mchati umebaki katika maeneo machache mno ya Mwambae, njia ya Marimbani na eneo dogo njia ya Usewe karibu na Mwembe Mtu, lakini bado mti huu adimu unakatwa katika kiwango cha kutisha kinachohatarisha uwepo wake Mafia na duniani kwa ujumla (extinction).

Kwanini mchati unakatwa sana?

Ukiacha ukataji unaosababishwa na ongezeko la watu wanaohitaji makazi mapya, bado kuna sababu mbili hatarishi zinazoongoza kuumaliza mti wa mchati kisiwani Mafia.

Mosi, ukataji kwa ajili ya kuni za kupikia: Kuni za mchati hazihitaji kukaushwa ili ziwake. Huwaka vizuri hata zikiwa mbichi. Maana yake unaukata mchati sasa hivi na kuutumia kwa kuni za kupikia muda huo huo. Tabia hii ya mchati imeufanya upendwe kama kuni namba moja au mbili kwa matumizi ya nyumbani. Si hivyo tu, bali biashara ya dagaa ambayo inahitaji dagaa wachemshwe kabla ya kuanikwa inapeleka kilio kwa michati kila siku. Biashara hii inahitaji kuni nyingi kuchemshia dagaa na mchati ndio mti unaopendwa sana kwa kuwa una kuni nzuri. Ni kusema mchati unaponzwa na uzuri wake.

Pili, mtazamo wa jamii kuwa ilipo michati basi mikorosho hustawi vizuri: Mtazamo huu umesababisha wananchi wengi kuikata michati kisha kuotesha mikorosho kwa ajili ya biashara. Ni kawaida ukipita Dongo kukuta mtu kuchoma moto michati ili aoteshe mikorosho.

Kwanini ni muhimu kuhifadhi na kuulinda mchati?

Ndugu msomaji, unaweza ukawa unajiuliza, hivi ni kwanini tusiikate miti ya michati wakati inajiotea tu maporini?

1. Kulipo na mchati kuna maji: Uzoefu unaonyesha kuwa mahali ambako michati iko mingi ni rahisi kupata maji. Huenda mti wa mchati unatunza maji ardhini. Katika dunia ambayo inakwenda kuwa maji bidhaa adimu, mchati unaweza kutusaidia siku za usoni kutunza vyanzo vya maji.

2. Mchati ni zawadi kutoka kwa Mungu: Upekee wa mchati na uwepo wake Pemba na Mafia na kukosekana maeneo mengine duniani unaweza kuiita ni zawadi ya Mungu kwa watu wa maeneo husika. Kwanini watu washiriki katika kufuja neema za Mungu alizozitoa bure?

3. Ni kumbukumbu na urithi kwa vizazi vijavyo: Mchati tumerithi kutoka kwa mababu zetu, mchati umekuwa nasi ukitusaidia kwa miaka mingi, kwanini tuumalize bila wajukuu zetu kuuona? Kwanini tusiutunze vizazi vyetu vitushukuru kwa zawadi ya mti huu wa kipekee?

4. Ni alama na utambulisho wa Kisiwa cha Mafia: Kisayansi kama tulivyosema hapo juu, mchati huitwa Philippia mafiensis, neno mafiensis linatokana na jina la Kisiwa cha Mafia. Popote unapotajwa mchati duniani, Mafia nayo inatajwa. Ni mti unaoitangaza Mafia duniani. Mchati kwao ni Mafia na Mafia ni nyumbani kwa mchati.

5. Mungu ametutaka tutunze mazingira: Jamii kubwa ya watu wa Mafia wanaamini katika Uislamu na Qur’an Tukufu. Hivyo kujiepusha na ufujaji wa mazingira (ukataji ovyo wa michati) ni wajibu kwa watu wote. Kwa mfano Qur’an (17:27), Allah amekataza uharibifu aliposema: “Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani. Na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake.”

Pia Qur’an 7:56 Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha kutengenezwa.”

 

Hitimisho

Mwishoni mwa mwaka jana (2017) Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kupitia Idara ya Maliasili ilipiga marufuku ukataji mti wa michati kwa matumizi ya kuni.

Marufuku hii ama haitekelezwi au haisimamiwi ipasavyo, kwa kuwa mchati bado unakatwa. Ni muda muafaka sasa kwa serikali kuisimamia marufuku hii ili kuilinda michati iliyo hatarini kutoweka.

Usimamizi wa marufuku hii sharti uende sambamba na upandaji wa michati upya katika maeneo yaliyokatwa kwa mustakabali mwema wa mimea hii adimu.

Mwandishi wa makala hii, Juma Salum, ni mwana mazingira, msomi wa masuala ya maliasili aliyehitimu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka. Anapatikana kwa simu:

0657 972723.

By Jamhuri