Nitumie fursa hii kuwatakiwa Heri ya Mwaka Mpya Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na kuwapa pole wale wote waliopatwa na misukosuko ya hapa na pale.

Pamoja na salamu hizo za Mwaka Mpya, nasikitika kuanza mwaka huu mpya wa 2017 kwa machungu kwetu sote, kutokana na mzigo mkubwa tuliotwishwa na Serikali.

Mwaka huu Watanzania wasitarajie kupata unafuu wa maisha kama  wanasiasa wanavyokuwa wakiimba majukwaani. Sasa ndiyo tunaoingia kwenye jukumu kubwa la kufunga mkanda usio na kikomo.

Wenyewe wanasema kila siku afadhali ya jana.

Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), wiki iliyopita, Mkurugenzi wake, Felix Ngamlagosi, ilitangaza ongezeko la bei ya umeme iliyoanza kutumika jana Januari mosi.

Kupanda kwa bei ya umeme nchini ni moja ya miiba kwa Watanzania walioanza kulalamikia ugumu wa maisha mwaka uliopita.

Kutokana na kupanda huko kwa bei ya umeme nchini, natarajia kuona ongezeko la bei ya bidhaa nchini, hivyo kuongeza mzigo kwa mwananchi wa kipato cha chini na kuzidisha ugumu wa maisha huku wakikumbwa na giza la maendeleo yao binafsi.

Ikumbukwe mwaka 2016 sekta ya uchumi ilionekana kuwa ni kaa la moto, kutokana na Watanzania walio wengi kulalamikia hali ngumu ya maisha, jambo ambalo limezigharimu baadhi ya familia kupata mlo mmoja tena kwa kubahatisha.

Pamoja na mwaka huo kuwa wa machungu, baadhi ya viongozi walionekana wakiwapa faraja wananchi kwa kile walichodai kuwa mwaka huu Serikali italegeza ili kuleta unafuu wa maisha.

Pamoja na ahadi hizo, Serikali badala ya kulegeza ndiyo imezidi kumminya mwananchi wa kipato cha chini, kwa kuongeza bei ya umeme itakayosababisha mfumuko mkubwa wa bei kutokana na unyeti wa bidhaa hiyo.

Sitarajii kuona unafuu wa maisha katu. Ninachotarajia ni kuona ongezeko kubwa la tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho.

Kutokana na utaratibu huu wa Serikali, namuona masikini akizidi kutokomea katika lindi la umasikini, huku tajiri akiendelea kuchekelea na mali zake.

Watanzania tunalo jukumu la kujiandaa kisaikolojia kutokana na mapambano ya ugumu wa maisha yanawangojea, huku kila bidhaa ikiwa imepanda bei kwa kisingizio cha kupanda kwa bei ya umeme.

Maisha ya mwananchi wa kipato cha chini yatakuwa afadhali ya jana, kila iitwayo leo kitakuwa ni kilio na kusaga meno. Hakutokuwa na unafuu kwa masikini kama baadhi yetu tunavyofikiria.

Ni lazima kila mmoja wetu akatafakari jinsi ya kujikwamua na ugumu wa maisha utakaokolezwa na tangazo hili la Serikali.

Ni jukumu letu kujipanga upya ili kuyamudu maisha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hatukosi mlo wa kila siku kama ilivyoanza kujitokeza kwa baadhi ya ndugu zetu.

Naomba Serikali ya Awamu ya Tano ijaribu kutafakari upya wakati wa kuongeza gharama katika huduma zake, ili kuendana na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kipato cha chini.

Naamini ya kuwa Serikali inayo nia ya dhati katika kumkwamua mwananchi masikini, hivyo natarajia kuona juhudi za makusudi zikifanyika katika kutekeleza hili.

2170 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!