LEO ni siku ya nne ya mwaka mpya wa 2018. Ni wakati wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujalia afya, uhai, nguvu, akili na ubunifu, miongoni mwa vingine  vinavyochangia kuharakisha maendeleo na ustawi wa watu.

Watanzania wameungana na watu wa mataifa mengine kuupokea mwaka mpya, kujitafakarisha kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika nyanja tofauti kwa kipindi cha mwaka 2017 na kukabiliana navyo.

Tunaungana na Watanzania katika tafakari hiyo, tukijielekeza zaidi kwenye mtazamo kwa taifa lenye jamii inayopaswa kuwa pamoja kutekeleza wajibu tofauti kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Tunatambua kwamba mazingira ya sasa yana viashiria vya kuwagawa Watanzania( kugawanyika) kwa misingi ya tofauti za itikadi, imani, jiografia, mtazamo, fikra nakadhalika.

Lakini wote wana wajibu mkubwa wa kuijenga Tanzania na kuweka mazingira bora ya kisiasa, kiutamaduni na kijamii, yafae kwa kizazi cha sasa na kinachokuja.

Ndio maana tunaamini kwamba ipo haja kwa Watanzania ‘kuutendea haki’ mwaka 2018 kwa kujikita katika mambo mema, kuyaepuka yanayowatenganisha ama kurudisha nyuma maendeleo ya nchi na ustawi wa watu.

Miongoni mwa mambo yasiyofaa yaliyotokea 2017 na yanayopaswa kuepukwa mwaka huu ni yale yenye kuleta mafarakano na kuwatenganisha watu.

Mwaka 2017 Taifa limeshuhudia matukio yenye mwelekeo wa kuligawa taifa  na kushuhudia matukio kama , utekaji watu (japo ni kwa idadi ndogo katika hesabu yake), kujeruhi hasa wakati wa uchaguzi nakadhalika.

Tumeshuhudia matukio yanayoibuliwa na kuwahusu `watu’, yanayopewa nafasi kubwa ya mjadala kwa jamii licha ya kutokuwa na mantiki katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa watu.

Tumeshuhudia kauli hasa za wanasiasa zikichangia kuwatenganisha na kuwafarakisha watu, badala ya kuwaunganisha katika umoja wenye maslahi mapana ya nchi.

Tunapoingia mwaka mpya, inafaa Watanzania watambue na kutumia kipindi cha mwaka huu kujadili masuala ya msingi, miongoni mwa hayo ikiwa ni yanayoipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Zipo fursa nyingi zilizokuwapo na zinazoibuliwa katika maeneo tofauti ya nchi, ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kwamba kama zikipewa kipaumbele kwa mwaka 2018, nchi itasonga mbele na ustawi wa watu utapatikana.

Kwa bahati nzuri, Serikali ya Rais John Magufuli imejiimarisha kuhakikisha kwamba nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda.

Jamii inapaswa kuijadili sekta ya viwanda nchini, historia yake, changamoto zilizojitokeza, namna ya kukabiliana nazo na fursa zilizopo sasa, ili azma hiyo ifikiwe kwa haraka na ufanisi.

Kuijadili sekta hiyo kunahusisha pia mjadala wa uzalishaji malighafi ambao ni sehemu muhimu kwa ushiriki wa wananchi wengi

Kuendelea kuwazungumzia ‘watu’ na matukio wanayoyaibua, yawe ya kupangwa ama vinginevyo, hakutaisaidia sana jamii kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Ndio maana tunapowatakia Watanzania heri ya mwaka mpya wa 2018, tunawajibika kuwasihi kwamba ushiriki mpana wa hoja za watu ujielekeze katika masuala yanayowaunganisha katikati ya tofauti zao, ili kuzitafuta na kuzitumia ipasavyo fursa zenye kuharakisha maendeleo ya nchi na ustawi wa watu.

By Jamhuri