Nimemsikia hii hivi karibuni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, akielezea ugumu wa kubadilisha Sheria ya Ndoa ya 1971. Alitaja mila na desturi, dini, na itikadi kama masuala yanayosababisha ugumu wa kuleta mabadiliko katika sheria hiyo. Kwa kifupi, haupo msimamo mmoja unaokubalika na pande hizi zote.

Tatizo kama hilo lipo pia kwenye suala la hukumu ya kifo. Tumemsikia pia Rais John Magufuli akitamka kuwa hana mpango wowote wa kuidhinisha kifo kwa wahalifu waliohukumiwa kifo. Hatufahamu msukumo anaoupata Rais Magufuli unaguswa na imani ya dini au la, lakini suala la hukumu ya kifo ni suala linalochukua nafasi kubwa katika maandiko ya dini mbalimbali.

Wakritsu hawana msimamo unaofanana juu ya hukumu ya kifo. Na wakati mwingine hata ndani ya madhehebu hayo hayo inajitokeza misimamo isiyofanana. Katika nyakati tofauti za historia ya Kanisa Katoliki msimamo juu ya hukumu hiyo umebadilika badilika. Umeanza kwa kuonekana kuwa ni mauaji halali kwa mujibu wa mtawa na mwanafalsafa mashuhuri Thomas Aquinas katika mazingira ambako, mathalani, kifo kinaweza kuzuia au kupunguza uhalifu.

Kwa sasa msimamo unaegemea zaidi katika kupinga adhabu ya kifo. Kanisa Katoliki linaunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa (UN) za kufuta adhabu ya kifo.

Lakini ni muhimu kusema pia kuwa hata maandiko ndani ya Biblia yanakuwa na misimamo tofauti yenye kuunga mkono na kupinga adhabu ya kifo.

Historia za madhehebu mengi Kikristu zinafanana na ile ya Kanisa Katoliki, kwamba msimamo umebadilika kutoka kukubali hukumu ya kifo hapo zamani, na kuipinga kwa sasa. Ni madhehebu moja ambayo inaelekea kushikilia msimamo wa kuikubali: Southern Baptist Convention ya nchini Marekani. Hawa wana imani kuwa ni wajibu wa dola kuwanyonga wanaokutwa na hatia ya mauaji.

Katika dini ya Kiislamu, hukumu ya kifo inaelekezwa kutolewa kwa wahalifu wa aina kadhaa, ikiwa ni pamoja na wanaoua kwa makusudi, na majasusi.

Kwa namna moja, unaweza kusema kuwa hukumu ya kifo katika mfumo wa sheria wa Tanzania unaoelekeza kutolewa kwa adhabu ya kifo kwa wauaji na wahaini, unalenga kundi lile lile la wahalifu linalolengwa kwenye hukumu ya kifo kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.

Zipo dini ambazo, kiitikadi, zinapinga kabisa adhabu ya kifo. Waumini wa Buddha wanaokadiriwa kufikia milioni 520 wanaelekezwa yafuatayo katika maandiko ya kiongozi wao, Buddha:

“Tendo lolote, hata kama linaleta manufaa kwako mwenyewe, haliwezi kuhesabiwa kuwa ni tendo jema kama litasababisha maumivu ya kimwili au ya kisaikolojia kwa kiumbe mwingine.”

Kimsingi ni dini ambayo inasisitiza kuzingatia kulinda kuliko kukatisha maisha ya wengine. Lakini pamoja na hali hii zipo nchi zenye waumini wengi wa dini hii ambazo zinatekeleza adhabu ya kifo.

Dini ya Hindu haina msimamo ulio wazi juu ya hukumu ya kifo, lakini ndani ya mafundisho yake unajitokeza msimamo ambao unadhoofisha hatua zozote zinazounga mkono hukumu ya kifo. Dini hii inahimiza dhana ya ahimsa, au kutodhuru mwingine pamoja na kuzingatia huruma. Lakini, muhimu zaidi, waumini wa dini hii wanafundishwa kuwa roho haiwezi kufa na kwamba kifo kinaambatana na mwili tu.

Imani hii inaweza kuwa na matokeo ya kuwapa wanajamii msimamo kuwa kuua binadamu ni sawa na kupoteza muda. Labda si ajabu kuwa India, ambayo asilimia 80 ya wakazi wake ni waumini wa dini hii, ndiyo nchi ambayo inaongoza duniani kwa kuwa na hukumu kidogo kabisa za kifo.

Nchini Tanzania, msimamo wa Rais Magufuli unakinzana na matokeo ya tafiti tatu ambazo zimefanyika nchini kubaini maoni ya wananchi juu ya hukumu ya kifo. Sehemu kubwa ya waliotoa maoni kwenye tafiti hizo wametaka kuendelea kuwapo kwa hukumu ya kifo.

Ni rahisi kujenga hoja kuwa mazingira ya kikatiba na sheria yanayounda utekelezaji wa hukumu ya kifo Tanzania yameandaliwa kwa manufaa ya rais na imani yoyote ambayo anaweza kuwa anafuata. Katika ubishi wa kupinga au kuunga mkono adhabu ya kifo, tunasahau kuwa tunambebesha mzigo mkubwa mtu mmoja ambaye, kwa sababu tu ameshika vyeo vikubwa vyenye kumpa uwezo wa kuokoa au kukatisha uhai wa binadamu wenzake, basi tunaamini itakuwa rahisi kwake kutumia uwezo huo.

Ni yeye anayepewa uamuzi wa mwisho wa kuamua iwapo anatoa idhini ya kunyongwa wale wanaokutwa hatiani na waliohukumiwa kunyongwa. Hatimaye, siku ya siku, ni yeye atakayesimama peke yake mbele ya Muumba wake na kuulizwa iwapo alifuata maelekezo sahihi ya dini yake. Wale waliokuwa wanampigia makelele mengi ya kunyonga au kuacha hawatakuwapo kujibu maswali.

Tunapenda kusema kuwa serikali haina dini, lakini tunaweza kuondoa kabisa hofu ya rais anayeamini kuwa kuna siku atafika mbele ya Muumba wake na kuhojiwa juu ya matendo yake duniani kwa mujibu wa tafsiri ya imani yake?

Hata tukizingatia rais ambaye hana imani ya dini yoyote, bado tunatarajia kuwa uamuzi wa kuidhinisha au kutoidhinisha kunyongwa kwa binadamu mwenzake bado utakuwa ni mzigo mzito utakaomwandama wakati wote.

Anayeidhinisha kifo, au kuokoa maisha ni mtu mmoja tu, wengine wote ni watazamaji. Hii sheria haihitaji mabadiliko hata kidogo, kwa sababu inampa nafasi mweka sahihi kufanya uamuzi ambao anaamini unafaa.

1378 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!