Afrika inaelekea kutawala uchumi wa dunia (2)

 

Nianze kwa kuomba radhi wasomaji kwa makosa ya kiuchapishaji katika kichwa cha makala haya sehemu ya kwanza: Afrika inaelekea kutawala uchumi wa Afrika (1), badala ya Afrika inaelekea kutawala uchumi wa dunia (1).

 

Nimepata mirejesho mingi kuhusu makala ya sehemu ya kwanza lakini sehemu kubwa ya mirejesho imejikita katika hisia za kisiasa. Msomaji mmoja kutoka Katavi ameniandikia hivi:

“Sanga unaota ndoto za mchana! Afrika kuendelea ipo ndoto kwa sababu ya ufisadi, uroho wa madaraka, upendeleo na udikteta.”

 

Ningependa niseme kitu kabla sijaendelea na sehemu ya pili. Wale wanaonifahamu tangu nilipoanza kuandika makala, wanatambua kuwa nilikuwa na bidii kubwa katika uandishi wa makala za siasa.

 

Ingawa mimi ni mfuasi wa siasa za mrengo wa kulia ambazo zinaegemea upande wa serikali; nimejifunza kuwa kunakuwa na mushkeli tunapojaribu kulitazama kila jambo kwa lensi ya kisiasa. Tatizo kubwa la kutumia lensi za kisiasa kwa kila jambo ni kujivua nafasi ya uwajibikaji hata kwa mambo yetu binafsi.

 

Watanzania wengi tumejenga utamaduni mbaya wa kulalamika kulikopitiliza kwa kila jambo. Tunailalamikia serikali kwa kila jambo, tunahisi inawajibika kwa kila jambo, tunaamini imeshikilia maendeleo yetu binafsi na hatimaye tunajilalamikia hadi nafasi zetu.

 

Tatizo la kulalamika ni kuwa kadiri unavyolalamika ndivyo sababu za kulalamika kwako zinavyoongezeka.

 

Kulalamika na kunung’unika kunakufanya usione jema sasa katika wakati ujao. Na hili ndilo linalofanya Waafrika wengi tuendelee kuhisi kuwa sisi ni wa kushindwa.

 

Wiki jana nilisema kuwa tunaitazama Afrika inayoumbika upya si kwa ajili ya yaliyotokea jana, isipokuwa tunaitazama Afrika mpya kwa kuangalia yanayotokea leo duniani kote na kule tunakoona Afrika ikielekea kesho.

 

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, nilikupitisha msomaji katika mtiririko wa hali ya kiuchumi duniani, na namna mabadiliko yanavyopindua nafasi za mataifa yenye nguvu duniani. Tuliona namna ukombozi wa nchi za Afrika unavyochukuliwa kama ujio wa kwanza wa Mungu kwa Afrika (First God’s visitation in Africa).

 

Vile vile nilieleza namna Afrika ilivyoshindwa kutumia fursa ya uhuru wake. Katika sehemu hii ya pili leo nitachambua dhana ya ujio wa pili wa Mungu kwa Afrika (Second God’s visitation in Africa).

 

Hata hivyo, niharakishe kusema kuwa si rahisi kueleza kwa kina, undani, kirefu na kwa kimo dhana hii ya kuinuka upya kwa Afrika katika makala haya kutokana na nafasi. Hata hivyo, nitaendelea kujitahidi kueleza kadiri tupatavyo nafasi.

 

Hadi muda huu, mataifa mengi kutoka nchi zilizoendelea ambayo yamekuwa yakizisaidia nchi nyingi za Afrika kibajeti; yanapunguza kwa kasi usaidizi wao. Msomaji unatakiwa uelewe kuwa mataifa haya si kwamba yanapunguza usaidizi wao kwa hiyari; la hasha!

 

Ukweli ni kwamba hali zao kiuchumi zimeyumba mno na nyingi chumi zao zinapumulia mashine. Taifa jeuri na lenye kiburi la Ugiriki hadi sasa ‘kwisha’ habari yake kiuchumi. Italia ambayo imo ndani ya G-8 hali yake kiuchumi imo katika misukosuko.

 

Umoja wa Ulaya wote unahaha kwa sababu wanachama wake kadha wa kadha wamefika hatua ambayo hawawezi tena kugharamia bajeti zao kwa asilimia kubwa (kama walivyozoea). Umoja wa Ulaya hadi sasa kutwa kucha unahangaika kuyanusuru mataifa wanachama ambayo chumi zake zinaogelea kwenye mstari mwekundu.

 

Hata baba lao Marekani haimo katika hali ya kujivunia kama zama za kale; kwa sababu ni taifa linalokimbilia madeni makubwa yanayotishia uchumi wake achilia mbali nakisi ya kutisha ya bajeti yake. Ubabe wa hapa na pale ilionao Marekani hadi sasa unazamishwa kwa kasi mno na uhalisia wa hali inayopitia nchi hiyo kuchumi.

 

Adui yako mwombee njaa! Mataifa makubwa yaliweza kuinyanyasa Afrika kwa sababu ya nguvu zao kiuchumi na kijeshi, lakini kwa sababu chumi zao zinahorojeka automatically yanajikuta hayana sauti za kuikoromea Afrika kama zamani.

 

Wakati hayo yakiendelea duniani, mambo yanaonekana kuliendea vyema Bara la Afrika na kimsingi binafsi ninajiridhisha kuwa Afrika imeanza kuzikata pingu zake moja baada ya nyingine. Zamani haikuwa rahisi kusikia kuwa lipo taifa la Afrika linaloweza kuikopesha ama kuisaidia Marekani ama nchi zilizoendelea.

 

Lakini hadi wakati huu baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kuzipa misaada ama kuzikopesha nchi zilizoendelea. Tunaona mfano mmoja ambapo Angola hadi sasa inamwaga misaada mingi kwa Ureno, ambayo imewahi kuitawala!

 

Ile hali ya bara hili kuwa na vita kila kona inatoweka kwa sababu Waafrika wanajitambua na hawataki tena kuuana kwa manufaa ya wageni. Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa Afrika ina maeneo yenye vita chini ya kumi kutoka maeneo zaidi ya 30 huko zamani. Hii ina maana kuwa Waafrika sasa wanajitambua na wameamua kuacha kugombana na kuamua kuzijenga nchi zao na bara lao.

 

Wakoloni walikuja na dini zao kutoka Ulaya. Jambo la kufurahisha kwa sasa ni kuwa yapo makanisa na taasisi za kidini ambazo zimeanzia Afrika na sasa zipo Ulaya na mataifa mengine zikiendeleza harakati za “kuwakomboa” hao Wazungu! Hili si jambo dogo, ni ishara ya hatua kubwa kwa Afrika na Waafrika.

 

Katika suala hilo hilo la imani, zipo rekodi nyingine lukuki ambazo Afrika imezivunja. Takriban miaka mitatu iliyopita Huduma ya Kiinjili ya Faith Terbanacle maarufu kama Winners Chapel imefanikiwa kujenga kanisa kubwa kuliko yote duniani. Kanisa hilo limeingia kwenye rekodi za kitabu cha Guinness.

 

Kitu cha kufurahisha ni kuwa kanisa hilo limejengwa kwa kutumia fedha na rasilimali kwa asilimia 100 kutoka ndani ya Afrika. Wenye kufahamu wanaelewa kuwa tulizoea kuona majengo ya ibada yakijengwa kwa misaada kutoka ng’ambo. Afrika ilitawaliwa hadi kiimani lakini sasa imeanza kujitawala kiimani. Kujitawala kiimani ni mwanzo wa kujifungua vifungo vya kifikra.

 

Wale watawala walafi wa madaraka, wasiozingatia demokrasia na utawala bora wanaisha-isha Afrika. Bara hili limeendelea kupata viongozi wanaojitambua, wenye kujali na kulinda maslahi ya mataifa yao. Kizazi kipya cha viongozi kinachipuka karibu kila nchi ya Afrika.

 

Hebu Waafrika tuchangamke, historia isitunyong’onyeze kiasi kwamba tuendelee kutembea na vivuli vya watawala wa kale tukiamini kuwa kila mtawala anayeingia atafuata nyayo za waliotunyanyasa. Ukitaka kuona mema yanayoliijia Bara la Afrika, jaribu kufananisha ilivyokuwa miaka ya zamani na ilivyo sasa ukiipachika kinafasi katika duru za mataifa mengine duniani.

 

Mataifa makubwa kwa miaka mingi yalidaiwa kudhulumu rasilimali za Afrika kwa sababu ya nguvu zao kiuchumi na kijeshi; lakini kwa sababu sasa mataifa hayo yanayumba kiuchumi; mambo yamebadilika! Mataifa hayo yanajikuta katika wakati mgumu kuiibia na kuidhulumu Afrika kupitia vita, migogoro ama watawala vibaraka.

 

Mataifa hayo yanaendelea kusalimu amri, kwani sasa hayana ujanja tena zaidi ya kufanya biashara zenye usawa na Afrika (trading with mutual benefits). Nafahamu kuwa hapa na pale bado kuna mataifa tajiri yanahaha kuturubuni Waafrika, lakini janja yao ndiyo inaishia-ishia; Afrika imeamka! Ni wakati wa Afrika!

 

Sasa hivi kumekuwa na ushindani wa mataifa makubwa yakipigana vikumbo kujadiliana na Afrika kuhusu biashara na rasilimali. Nchi nyingi zimezinduka na sasa zinataka mtindo wa “nipe nikupe” badala ya mtindo wa “chukueni tu”. Mataifa makubwa yanagongana Afrika yakipigania kukubaliwa na Wana-Afrika.

 

Hivi ninavyoandika makala haya wapo Waafrika wengi ambao wamethubutu kuanzisha biashara na kampuni katika nchi zilizoendelea na huko wanawaajiri “walioendelea” wengi tu. Yale mambo ya kudhani kuwa Waafrika wakienda Ulaya kazi yao ni kusafisha vyoo na kuwatunza wazee, sasa yanazidi kupotea kwa kasi.

 

Hata wanadamu wenzetu kutoka mataifa yaliyoendelea, waliokuwa wanawadharau Waafrika, kwa sasa wanaendelea kurudisha heshima kwa Waafrika. Waafrika wengi wameanza kuacha kujikunyata na sasa wanachangamkia fursa, wanasimama nje ya mazoea ya kushindwa, wanajaribu, wanafanikiwa na wanang’aa.

 

Nikija kule kwenye jicho la kisosholojia na kiimani, tunaona kuwa maonevu na mahangaiko ya Afrika yamekoma; na sasa kwa maendeleo ambayo Afrika inaonesha tunaamini kuwa sasa ni Ujio wa pili wa Mungu kwa Afrika (Second visitation of God in Africa).

 

Kiramani tunaamini kuwa kipindi cha mateso na mahangaiko ya Afrika kimekoma kuanzia katikati ya miaka ya 2000, ikiwa ni miaka 50 baada ya uhuru kwa mataifa mengi.

 

Wanahistoria wa kale hukiita kipindi hiki kama Jubilei ikiwa na maana kuwa ni kuachiliwa, kuijiwa upya, kusamehewa, kuanza upya, kupata mema na kuumbika upya.  Ukichunguza mataifa mengi ya Afrika kuanzia miaka hiyo yameendelea kupata mageuzi makubwa kisiasa, kiuchumi na kiimani.

 

Idadi kubwa ya Waafrika sasa wanajitambua, wanajitutumua na hawakubali kuburuzwa kirahisi. Ni wale tu wasiofuatilia hali ya mambo ndiyo wanaoweza kuendelea na biashara ya kukata tamaa kuhusu Afrika, lakini ninapiga mbiu leo ya kwamba tutazame, tukaone, mioyo yetu iburudike kwa sababu Afrika inaenda kutawala uchumi wa dunia.

 

Tofauti na First visitation of God in Africa, katika ujio huu wa pili tunaona kuwa Afrika na Waafrika wenyewe “hatujalazia damu”, tumechangamkia na mwanga unaonekana. Kwa leo nihitimishe kwa kusema: “Naiona Afrika ikienda kuutawala uchumi wa dunia”. Wakati mwingine nipatapo wasaa nitaendelea kuchambua tumaini la Afrika kuutawala uchumi wa duniani miaka michache ijayo. Waafrika ni wakati wetu wa kung’aa kiuchumi.

 

0719 127 901

[email protected]