Mpendwa msomaji, natumaini hujambo na unaendelea na shughuli zako za kila siku, huku wengine nikiamini kuwa mmepigika mifukoni sawa na mimi.

Kwenye  Serikali ya Awamu ya Tatu tulikuwa tunazungumza ‘Ukapa’ lakini Awamu hii sijajua niuiteje. Ninaloweza kusema ni kuwa tutabanana hapahapa. Sijapata hamu ya kurudi kijijini na wala sitafanya hivyo.

 

Ukiacha hilo la ukapa, wiki hii yamekuwapo matukio makubwa mawili yaliyonitia shaka. Matukio haya si mengine bali ni kauli tata kutoka kwa viogozi wetu. La kwanza ni kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuwa wapinzani wananunua waandishi wa habari waandikwe vizuri.

 

Kauli ya pili ni hii iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa chama chake kimeanzisha makambi ya ukakamavu kwa nia ya kuzalisha vijana wa kulinda viongozi wao kwani polisi waliishajitoa kuwalinda. Kauli ya Mbowe imeungwa mkono na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbrod Slaa.

 

Sitanii, naanza na hii ya Makinda. Kwa uchungu nasema kauli hii ya Makinda inawezekana imemtoroka kutoka kinywani mwake, au alipata ajali akawa anaota ndoto mchana wakati mkutano na waandishi wa habari unaendelea. Hata kama ana kinga ya kuzungumza lolote, kinga hii inakomea katika kusema ukweli.

 

Ukiona kiongozi anaanza kubwabwaja na kutoa kauli zisizo na mashiko, basi unapaswa kujiuliza. Kwetu kuna msemo kuwa mbwa akikaribia kufa huwa anarefuka. Msemo huu nikiuweka katika siasa, inaonekana vyama vya siasa vikikaribia kufa huwa vinageuka sawa na mfa maji. Hata unyasi unaoeleka kwenye ziwa au bahari huukumbatia akidhani utamwokoa.

 

Sitanii, wakati Makinda analalamika juu ya waandishi kuandika ‘vizuri’ habari za wapinzani, anasahau kinachozungumzwa na wapinzani. Makinda anapaswa kufahamu kuwa wapinzani wanazungumza lugha ya wananchi, wakati wabunge wa CCM wanazungumza lugha ya watawala.

 

Imekuwa kawaida ndani ya Bunge wabunge wa CCM hawajui mipaka yao. Ukisikiliza michango ya wabunge wa CCM wanakuwa kama Serikali. Wabunge kazi yao ni moja ya kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba bila kujali wanatokea CCM au upinzani. Kinachotokea kwa wabunge wa CCM ni aibu.

 

Akimaliza kuchangia mbunge wa upinzani, mjibu hoja anapaswa kuwa Waziri mwenye dhamana na wizara iliyotuhumiwa. Kichekesho kinachokuja ni kuwa unakuta wabunge wa CCM wakisimama wanafanya kazi ya Serikali. Kwetu kuna msema kuwa mwizi akikutwa hata na mkungu wa ndizi, ukimuuliza atakwambia ‘eti nimeiba’.

 

Sitanii, siku zote na miaka yote majibu ya kujitetea hayana mashiko. Ni vyema Serikali au wabunge wa CCM wakajifunza haya mambo. Wakisikia kuna mambo yanaharibika huko Shinyanga, Tabora, Mtwara au Pemba si kazi yao kuwaambia wananchi wawe watulivu. Jukumu lao ni kwenda kuchunguza penye tatizo.

 

Baada ya uchunguzi binafsi wa wabunge au kupitia wasaidizi wao, wanapaswa kuja na majibu ya ufumbuzi wa tatizo lililokuwapo, kisha watambe kuwa wamemaliza matatizo ya wananchi. Kwa mfano, ikiwa tatizo la Jiji la Dar es Salaam ni uchafu na kuzagaa kwa wamachinga, si jukumu la wabunge kuisemea Serikali.

 

Wabunge wa Dar es Salaam wangekuwa wa kwanza kushinikiza matumizi ya Jengo la Machinga Complex lililojengwa kwa mabilioni ya shilingi,  lakini leo wamachinga wanapanga bidhaa nje ya ghorofa hilo badala ya ndani. Mitaani ndiyo usiseme.

 

Wamachinga wamezagaa kila kona ya Jiji la Dar es Salaam kwa kiwango ambacho hata kukusanya kodi ni tabu. Kilichosalia sasa, na nadhani si muda mrefu, kitaanza kutokea kwani viroba tayari vipo sokoni, wamachinga wataanza kuuza bia, konyagi, whisky na wine kwenye foleni za magari katika jiji hili, kisha baa zitahamia mikononi mwa wamachinga sawa na ilivyo Lubumbashi, DRC.

 

Sasa ikitokea wapinzani wakaishutumu Serikali kwa kushindwa kusimamia wamachinga kuingia kwenye jengo walilojengewa, akisimama mbunge wa CCM anapiga porojo za kuitetea Serikali huku akimpiga vijembe mpizani. Hata mawaziri wakisimama siku hizi hawajibu hoja za wananchi, badala yake wanaishia kupiga vijembe wapinzani.

 

Sitanii, bila hata kuambiwa, kinachotokea waandishi wanakumbuka msemo wa busara usemao ‘mti wenye matunda ndiyo urushiwao mawe’. Vyombo vya habari vinajiuliza, kuna matatizo ya maji, elimu, barabara, hospitali, ubabe wa polisi, rushwa, kodi bandia, riba kubwa za mikopo, ukosefu wa taarifa kwa kutumia mihuri ya siri na madhambi mengine mengi tu, lakini wabunge wa CCM kazi yao ni kutetea tu.

 

Hii inanitia shaka kuwa kama Makinda haoni tatizo hili, na kubaini kuwa wabunge wa upinzani wanazungumza lugha ya wananchi; kwa maana ya matatizo yanayowagusa wananchi na CCM wanazungumza lugha ya watawala, kwa maana ya Serikali kukemea na kuweka misimamo; basi kama hajafilisika kifikra, yuko njiani.

 

Narudia, hakuna mwandishi anayehongwa. Waandishi wanachapisha kitu kinachoitwa habari na si taarifa. Tunahitaji kumpeka shule Makinda afahamu tofauti kati ya habari na taarifa na tukifanikiwa hili, basi atakuwa anawanyamazisha wabunge wa CCM akiona wanapotoka na kuanza kujibu hoja za wapinzani badala ya kusema matatizo ya wananchi wao.

 

Sitanii, sehemu ya pili ya makala haya ni hili tamko la Chadema la kutaka kuanzisha makambi ya ukamamavu. Nafahamu pasi shaka, kuwa katika siasa wamo wanasiasa waliokuwa wafanyabiashara, wengine wapigadebe na wengine walikuwa watumishi katika vyombo vya dola – katika vyama vyote.  Hii si kwa Chadema pekee, bali hata CCM.

 

Anayebisha aniambie Jenerali Robert Mboma aliposimama kugombea ujumbe wa NEC kupitia CCM akashindwa, alikuwa yeye ni nani? Si ‘njagu’ mstaafu bwana? Hata Chadema wapo wa aina hiyo na si kosa kabisa. Ukiishastaafu jeshini au polisi una haki ya kuchagua chama au kuwa mgombea binafsi.

 

Tatizo langu, na watu hawa au vyama vyenyewe iwe CCM au Chadema, ni kuanza kutoa mafunzo ya kujeshi kwa vijana wao chini ya mwavuli wa UKAKAMAVU. Nimeyasoma mawazo ya Dk. Slaa kuwa analalamika jinsi CCM walivyoshiriki kwa hali na mali kupeleka vijana wao kwenye makambi kule Igunga na jinsi vijana hao walivyoshiriki kikamilifu kupiga watu.

 

Hapa ndipo ninapopata shida. Mbowe anasema polisi wameshindwa kuwalinda, Dk. Slaa anasema vijana waliopewa mafunzo kwenye kambi za CCM wametumika mno kupiga watu na wanapewa silaha. Kwa tafsiri rahisi Chadema sasa nao wameamua kuanzisha kambi yao itakayokiwezesha chama hicho kujilinda au kwa maana nyingine kujibu mapigo ikiwa wataguswa.

 

Ukamavu unaozungumzwa ni mafunzo ya kijeshi tu. Tusidanganyane. Nchi zote duniani zilizoendelea na zinazoendelea kama kuna jambo zinalikataa ni siasa za vyama kuingizwa kwenye vyombo vya dola, yaani majeshi. Tukifika mahali tukawa na polisi CCM au Chadema, tukawa na JWTZ CCM au Chadema, basi tujue tumeandaa makaburi yetu.

 

Vyombo hivi vinachukuliwa kama mwamuzi wa mpira wa miguu. Hapa Chadema ningeshauri watoe orodha ya aina ya ulinza wanaoutaka kwa polisi, kisha hili likishindikana ndipo polisi washutumiwe na kushinikizwa kufanya hivyo. Kauli ya jumla kuwa walikataa kuwalinda Chadema ina ukakasi. Inaleta hofu kuwa Chadema vijana wake wakiishawiva kijeshi, itakuwa sawa na simba aliyetoroka zizini.

 

Kwenye majeshi kuna amri. Kuna vyeo. Kuna taratibu. Chadema ikiwa wataanzisha kundi la ukakamavu, likafahamu medani za vita, siku kundi hili lililokusanywa mtaani bila mafunzo maalum yaliyopangiliwa kimkakati likiasi, na hasa ukitilia maanani kuwa halitakuwa na kiapo chochote cha utii, itakuwa hatari.

 

Wanajeshi, polisi, Usalama wa Taifa na wengine huwa wanaapishwa. Wanajulishwa adhabu yao ikitokea wakakataa kutii amri kwa maana ya uasi. Hata wewe msomaji unaijua. Kwa maana hiyo, adhabu husika inawafanya kabla hawajafikia uamuzi wa kuasi, wajue matokeo ya uamuzi wao. Lakini kwa vyama vya siasa, leo ni rahisi kutoka CCM ukahamia Chadema au Chadema ukarejea CCM.

 

Jeshini huwezi kutangaza kwenye mkutano wa hadhara kuwa unahama kutoka JWTZ na unakwenda Polisi au Usalama wa Taifa. Kuna taratibu zake na sheria zinazotawala uhamaji huo. Narudia, hili haliwezekani kwenye vyama vya siasa. Tunawashuhudia vijana waliokuwa wakihubiri utii kwenye vyama vyao sasa hivi wapo magerezani.

 

Kwa upande wa CCM nasema hatari ya CCM kuwa na kikundi chake ni kubwa mno. Ukubwa wa hatari hii unatokana na kwamba chama tawala kiko karibu na majeshi. Vijana hawa hawana kiapo sawa na nilivyosema kwa Chadema, wakipewa silaha hawa wanaweza kugeuka hatari sawa na simba aliyetoroka zizini.

 

Sitanii, hawa vijana wa CCM wakikutana na vijana wa Chadema na wote wakawa na mafunzo, mchezo wa siasa unageuka kuwa uwanja wa mapambano. Vijembe vya kisiasa tulivyokuwa tunavisikia enzi za Augustine Mrema akimtuhumu Mkapa kuwa alipewa rushwa ya Sh milioni 500 katika kashfa ya minofu ya samaki hatutavisikia tena.

 

Hoja za ukwapuzi wa fedha za EPA hatutazisikia tena, bali tutasikia majeshi yakisonga mbele sawa na ilivyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mashariki maeneo ya Kisangani na Mbujhimai. Si muda tutajikuta tuna makundi sawa na M23 ya Congo au LRA ya Uganda. Tukifika hapo, suala la maisha kuondolewa na Mungu litakuwa msamiati.

 

Vijana hawa watakuwa na tamaa ya kuingia Ikulu kwa gharama yoyote, bila kujali wanapoteza maisha ya nani au wanamdhuru nani. Nasema huko ndiko tunakoelekea mwaka 2015. Ikiwa tunayajua haya, kuwa yanaweza kuwa chimbuko la kuchimba makaburi kila kukicha na pengine tukaondoka duniani kabla ya wakati wetu, kwa nini tuelekee huko?

 

Sitanii, vyama vya siasa iwe CCM, CUF, Chadema, TLP, NCCR-Mageuzi visiruhusiwe na viongozi wao kuwa na vikundi vya kujilinda. Hata vikundi vilivyopo sasa kama Blue Guard, Green Guard na Red Brigade vifutwe mara moja. Tukichukua hatua hii, tutajenga imani kuwa uwanja wa mchezo kisiasa uko sawa.

 

Vikundi hivi vikishavunjwa, kazi ya kulinda usalama wa wananchi ibaki mikononi mwa polisi bila kujali itikadi. Haya yanaweza kupuuzwa leo, lakini nasema tukiyapuuza kwa watakaokuwa hai baada ya 2015 watayakumbuka maneno yangu na kujuta. Wahenga walisema majuto ni mjukuu. Tusiingize majeshi katika siasa.

Please follow and like us:
Pin Share