Si kila kinacholiwa kina faida mwilini. Kuna vyakula vya kujaza tumbo na vingine vya kujenga mwili.

Inaelezwa chakula bora ni kile kinachojenga mwili, ambacho ndani yake kunakuwa na virutubisho vya kutosha.

Hili ni jambo ambalo limethibitishwa kupitia maisha ya Rachel Mwita Massana, aliyefariki dunia na kuzikwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 111.

Ndugu wa karibu wa marehemu Rachel wamelieleza JAMHURI kuwa ndugu yao ameishi maisha marefu namna hiyo kutokana na kuzingatia masuala ya mlo.

Wataalamu wa lishe pia wanasema kuwa chakula bora husaidia mwili kuboresha kinga ya kujilinda na magonjwa pamoja na kuuwezesha mwili kuwa na uwiano sawa na uzito wake.

Daniel Massana (70), mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam na ambaye ni mtoto wa nne wa marehemu Rachel, ameliamba gazeti hili kuwa mama yake alifariki dunia Januari 30, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 111.

Daniel anasema marehemu mama yake alizaliwa kijijini Majimweli, Bunda, Mara mwaka 1909 na kwamba tangu amezaliwa hadi anafariki dunia hakuwahi kuugua.

Chanzo cha kutougua kwa mama yake anakitaja kuwa ni ulaji wa vyakula vya asili na aina ya maisha aliyokuwa akiyaishi ya kufanya kazi ya kilimo bila kuchoka.

Anasema shughuli za kilimo alizokuwa akizifanya marehemu mama yake kabla hawajahamia jijini Dar es Salaam zilimfanya kuwa na afya njema na mwili imara.

Kabla ya kumhamisha kutoka Bunda na kuja naye jijini Dar es Salaam mwaka 2000, Daniel anasema mama yake alikuwa hawezi kula chakula kisichokuwa na maziwa au mafuta ya ng’ombe.

Daniel anasema awali hawakuwa wanaufahamu umri wa mama yao kwa ufasaha.

“Tulipata umri wake kwa uhakika baada ya kukokotoa kutoka kwenye umri wa mdogo wake,” anafafanua.

Marehemu Rachel  Massana alifunga ndoa na Mwita Massana mwaka 1944 na kujaliwa kupata watoto sita. Wawili kati yao wamekwisha kufariki dunia.

Mpaka mauti yanamkuta, Rachel alikuwa amekwisha kupata wajukuu zaidi ya 70 na idadi kubwa ya vitukuu na vining’ina.

Daniel anaeleza kuwa marehemu mama yake alifariki dunia katika Hospitali ya Amana, Manispaa ya Ilala alikokuwa amepelekwa kwa matibabu baada ya afya yake kudhoofika.

Siku aliyofariki dunia alikuwa amekaa siku nne bila kula, kwa mujibu wa Daniel.

Hata hivyo, anasema kuwa ripoti ya kitabibu ya madaktari katika Hospitali ya Amana inaonyesha kifo chake kimesababishwa na shinikizo la damu la siku nyingi, lililosababisha mishipa yake ya damu kushindwa kufanya kazi vizuri.

Kwa mujibu wa Daniel, miaka miwili iliyopita mama yake alianza kushindwa kuwatambua baadhi ya watu, na kwamba akili yake ilianza kuwa kama ya mtoto mdogo.

Aidha, anasema mwaka 2004 mama yake aliteleza na kuanguka na kuvunjika mguu na kufikishwa hospitalini, ikiwa ni mara ya kwanza katika maisha yake.

“Mama alipenda kilimo, hata chakula alichokipenda sana ulikuwa ugali wa mtama… hiyo ndiyo siri ya kuishi miaka hii 111,” anasema Daniel.

Anavitaja vyakula vingine ambavyo mama yake alikuwa anavipenda ni ugali wa muhogo, dona, uji wa ulezi na mboga zilizoungwa kwa kutumia maziwa au mafuta ya ng’ombe.

“Mwaka 2000 nilipohamia kikazi huku jijini Dar es Salaam niliona mama hana mtu mwingine wa kumtunza kule kijijini nikaamua kumleta huku. Mara baada ya kufika alinisumbua sana kwamba vyakula vya huku vimemshinda. Akanilazimisha nimrudishe kijijini kwa sababu huku anakaa tu bila kufanya kazi,” anasimulia Daniel.

Aidha, anasema alivyofikisha miaka 90 na kuendelea alianza kubagua vyakula na kuanza kulalamika kwa nini asife kama walivyofariki dunia wenzake wenye umri Akama wake.

Anaongeza kuwa mwaka 2012 walianza kumlisha chakula kwa kumlazimisha huku yeye akiwaeleza kuwa hajisikii hamu ya kula chakula cha aina yoyote.

Hilo lilimfanya aanze kudhoofika na kwamba alivyofikisha miaka 108 alidhoofika zaidi hadi kushindwa kunyanyuka.

Cecilia Simon (65) ambaye alikuwa jirani yake huko kijijini Majimweli, Bunda, anaeleza kuwa enzi za uhai wake Rachel alipenda sana kulima.

“Alikuwa anashinda shambani akilima. Kuna kinywaji cha kienyeji kinaitwa togwa alikuwa akiipenda kuinywa hadi shambani alikuwa anakwenda nayo,” anasema Cecilia.

Naye, Samweli Kiyungi (55) mkazi wa Kitunda anasema kufanya kazi za kutumia nguvu kunasaidia mwili kuzalisha kinga ya kutosha dhidi ya magonjwa.

Akitolea mfano wa historia ya marehemu Rachel Massana, yeye anasema kuna kipindi alikuwa anafanya kazi ya kuuza mkaa akiutoa Kisarawe kuuleta Gongolamboto na kwamba kwa kipindi hicho alikuwa hapati magonjwa.

Kwa upande mwingine, baada ya ndugu kuafikiana kutosafirisha mwili wa marehemu Rachel, walimzika bibi huyo Januari 31, mwaka huu Kitunda Mwanagati.

280 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!