Wajumbe kamati za ardhi waaswa

Wajumbe wa kamati za Urasimishaji Ardhi Kata ya Vikindu, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kupunguza migogoro ya ardhi maeneo ya vijijini.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Fillberto Sanga, wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo kuhusiana na suala la urasimishaji ardhi.

Anasema wajumbe wa kamati hizo na watendaji wengine wakifanya kazi kwa weledi kuna uwezekano wa migogoro ya ardhi kumalizika kabisa.

Sanga anasema kwamba lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha inasimamia suala zima la urasimishaji wa ardhi kwa wananchi wote ili kuondoa migogoro ya ardhi.

Anasema katika mpango huo kata hiyo imeingia katika uboreshaji wa makazi ili kuifanya ardhi hiyo iwe na thamani na faida kwa wananchi.

Anasema kuwa vijiji vyote vya kata hiyo vitaingia katika mpango wa kupimiwa ardhi na kurasimishiwa makazi chini ya kampuni iliyopitishwa na Wilaya ya Land Survey and Consultancy Service, kwa kuzishirikisha kamati zilizopo.

Anasema kuwa upimaji wa ardhi utakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma za kijamii kama shule na hospitali ili kuinua maendeleo ya kata na vijiji vyake.

Katika mpango huo kamati zitashirikiana na serikali pamoja na wananchi kuhakikisha watu wote wanapimiwa maeneo yao na kupewa nyaraka wanazoweza kuzitumia kama dhamana wanapotaka kukopa fedha benki au kwenye taasisi nyingine za fedha.

Anawaasa wananchi kutokwepa kushiriki katika zoezi hilo kwani kufanya hivyo kutahesabika ni sawa na kupinga maendeleo.

Baadhi ya wananchi waliunga mkono mpango huo wakisema kuwa utawasaidia kuongeza thamani ya ardhi na kukopesheka kirahisi.

Tanya Manda, mkazi wa Kijiji cha Picha ya Ndege, Kata ya Vikindu, anasema pamoja na kuongeza thamani ya ardhi, mpango huo utawahakikishia wananchi umiliki wa maeneo yao, hivyo kuepusha migogoro ya mara kwa mara.

Zaidi ya wananchi 5,000 wameingia katika mpango wa urasimishaji ardhi katika Kata ya Vikindu.