Mazishi ya watu 20 waliofariki dunia katika tukio linalotajwa kuwa baya kuwahi kutokea katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa kukanyagana wakati wakigombea mafuta ya magonjwa mbalimbali yameanza.

Watu hao walifariki dunia Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Majengo baada ya ibada iliyoendeshwa na Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God Calvary, Mtume Boniface Mwamposa.

Baadhi ya watu walionusurika katika tukio hilo wanasema mkanyagano huo ulitokea mwishoni mwa ibada, baada ya watu kutangaziwa kuwa mafuta hayo yalikuwa getini.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro imeeleza kuwa kati ya waliofariki dunia watano ni watoto, 14 ni wanawake na mmoja ni mwanamume.

Mtu mmoja aliyefariki dunia ametambuliwa kuwa ni muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, Joyce Togoray (58).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salum Hamduni, amesema katika taarifa hiyo kuwa tukio hilo lilitokea wakati muda uliotolewa kwa ajili ya ibada hiyo ukiwa umemalizika.

“Askofi Boniface Mwamposa, maarufu kama ‘Bulldozer’, aliomba kibali cha kufanya mkutano wa Injili kuanzia tarehe 01/1/2020 hadi tarehe1/2/2020. Mkutano uliruhusiwa kuanza saa sita mchana hadi saa 12 jioni, lakini katika siku ya mwisho, askofu huyo alipitiliza muda na ilipofika majira ya saa moja na nusu jioni ndipo aliwatangazia waumini wake kuwa wapite kwenye mafuta yaliyokuwa yamemwagwa kwenye turubai getini,” anasema Kamanda Hamduni katika taarifa hiyo.

Aidha, imetolewa orodha ya watu waliojeruhiwa katika tukio hilo huku hali za watu wawili zikielezwa kuwa ni mbaya, kwani hawawezi kuzungumza.

Orodha ya majeruhi inajumuisha: Glory  James Kisanga (16) mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Rau; Suzana Mianga (71) mkazi wa Nyumba ya Mungu Wilaya ya Mwanga; Agnes  Linus (75) mkazi wa Kibosho Kindi; Thomas  Erabison (47) mkazi wa Masama Wilaya ya Siha; Rozina  Steven; Mary  Macha (45) mkazi wa Kibosho Road; Elizabeth Peter Tarimo (42) mkazi wa Majengo; Janeth Daniel (22); Junior  Paulo, mtoto wa miaka miwili na miezi miwili; Anjela  Sinyangwa (36) mkazi wa  Pasua mjini Moshi; Morin  Julius (24) mkazi wa Mererani mkoani Manyara; Mary  Paulo (23) mkazi wa Old Moshi; Grace Nderelio (42) mkazi wa Kikavu Chini na Elizabeth Peter (42) mkazi wa Majengo.

Kauli ya Serikali

Akizungumza na mamia ya watu waliofika hospitalini kuwatambua watu waliofariki dunia katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amesema kuanzia sasa serikali itaanza kudhibiti mahubiri yenye mwelekeo wa upotoshaji, ikiwamo watu kuelezwa wataponywa magonjwa yao, kupata utajiri, mafanikio kibiashara pamoja na kupata ajira.

Mghwira amesema watu hao 20 walifariki dunia kutokana na kukanyagana katika harakati za kutaka kukanyaga mafuta ya upako kwenye kongamano hilo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, miili ya marehemu waliofariki dunia katika tukio hilo ilitarajiwa kuagwa jana katika uwanja huo huo wa mpira wa Majengo, katika ibada maalumu.

Amesema miili ya watu ambao hawatatambuliwa nayo itapelekwa uwanjani hapo na baada ya ibada miili hiyo itarudishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi ili ikitambuliwa shughuli za mazishi ziendelee.

Aidha, amesema tayari uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kufanyika, ambapo tayari watu wanane, akiwamo Mwamposa, wamekamatwa na wanahojiwa.

By Jamhuri