Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu Hassan, amepongeza wafanyakazi hodari ambao wamepata zawadi katika maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani(Mei Mosi) 2026 huku Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA) kikitoa zawadi kwa wanahabari sita.
Katika maadhimisho ya kitaifa ambayo yamefanyika Uwanja wa Halmashauri ya Njombe, Rais Samia alikabidhi zawadi ya mmoja wa washindi wa Kitaifa waandishi bora ambao ni wanachama wa JOWUTA,Idda Mushi kutoka ITV na Radio One.
Mwingine ambaye alishinda tuzo ya kitaifa ni mwandishi mwandamizi Lucy Ngowi ambaye anaandikia gazeti la mfanyakazi awali alikuwa mwandishi wa Habari Leo.
Wanahabari wengine ambao wametambuliwa na JOWUTA kwa uhodari wao na kupewa zawadi ni waandishi Alfred Zakaria wa the respondents na Tamali Vullu wa gazeti la mwananchi kutoka mkoa.wa Dar es salaam
Kwa mkoa wa Morogoro waandisbi wanachama wa JOWUTA waliopewa zawadi ni Ashura Ibrahim Kazinja wa Mtanzania Digital na Rashid Mtagaluka wa gazeti la Pambazuko.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, leo Mei Mosi mkoani Njombe,Rais Dkt Samia aliwataka wafanyakazi nchini kuendelea kuchapa kazi ili kuinua uchumi wa nchi.
Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi kadri uchumi utakavyoruhusu. Pia Serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi za kuimarisha ustawi wa wafanyakazi.
“Ndugu zangu chapeni kazi Serikali ipo, inawasilikiza inawathamini,” amesema na kuongeza kuwa:
“Sote kwa pamoja hatuna budi kushirikiana, kuamianiana na kutanguliza maslahi ya Taifa letu, ninawahimiza tuendelea kufanya kazi kwa bidi, kwa uadilifu na weledi ili kujenga uchumi na ustawi wa jamii,” amesema.
Tofauti zisihatarishe amani
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaambia wafanyakazi kuwa, tofauti zisigeuke kuwa sababu ya kuhatarisha misingi ya amani, umoja na mshikamo iliyoachwa na waasisi wa Taifa.
Dkt Samia amejenga hoja hiyo akirejea kauli mbiu ya Mei Mosi kuwa kazi haiwezi kuwa na staha bila na amani, hakuna ustawi wa mfanyakazi bila utulivu wa Taifa.
“Tushikamamaneni, tufanye kazi, tujenge Taifa letu na tujenge heshima ya nchi yetu,” amesisitiza .
Awali ,Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini(TUCTA) Tumaini Nyamuhokya alisema wafanyakazi nchini wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanyakazi katika mazingira bora.
Nyamuhokya alimshukuru Rais Dkt Samia kwa kuongeza mishahara mwaka jana na pia kutatua kero za wafanyakazi za malimbikizo ya madeni na kutopandishwa vyeo.
Amesema kero ya malimbikizo ya madai kwa wafanyakazi wa TAZARA imefanyiwa kazi na serikali imetoa fedha zaidi ya sh 2 bilioni ili kusaidia kulipa madeni.
“TUCTA inakuhakikishia Mh Rais wafanyakazi wanakuunga mkono na ndio sababu huwakuti katika migogoro”amesema
Akizungumza katika sherehe hizo,Waziri Mkuu Mwingulu Nchemba amewataka wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi na kuwa wavumilivu kwa changamoto zinazowakili kwani zinaendelea kufanyiwa kazi na serikali.
Nchemba amesema serikali inaendelea kufanyakazi kubwa kuboresha uchumi wa nchi na kutatua kero za wananchi katika sekta mbalimbali.
Mwenyekiti wa JOWUTA ,Mussa Juma akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Mei Mosi Njombe, amesema JOWUTA mwaka huu imeshiriki kwa mara ya kwanza Mei Mosi na imeweza kutoa zawadi na kushiriki vikao vya maandalizi ya Mei Mosi kitaifa.
Juma amesema mwakani JOWUTA imejipanga itaongeza zawadi kwa wanahabari mikoa mingine ili kutambua michango yao lakini pia kutoa mafunzo ikiwepo masuala ya Bima ya Afya,kujiwekea akiba ,Kujua utendaji wa Taasisi mbalimbali za umma na binafsi na ameshukuru Taasisi za Serikali,Binafsi na Viongozi mbalimbali ambao wamewasaidia kushiriki Mei Mosi kwa mara ya kwanza.





