Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ofisi ya Msajili wa Hazina, Leo Ijumaa, Mei 1, 2026, imeshiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira 2050.”

Ushiriki wa Ofisi hiyo unaakisi dhamira ya Serikali katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza tija ndani ya taasisi na mashirika ya umma, ambazo ni mhimili muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Chacha Marigiri, aliwapongeza wafanyakazi wote wa Ofisi hiyo kwa mchango wao katika ujenzi wa Taifa, akisisitiza kuwa nidhamu kazini, uwajibikaji na uzalendo ni misingi muhimu ya kufikia maendeleo endelevu.

“Tunatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi, hususani wale wa taasisi na mashirika ya umma katika kuongeza ufanisi wa taasisi zao na hivyo kuongeza uchangiaji wao kwa Serikali kupitia mapato yasiyo ya kikodi,” alisema Bw. Marigiri.

Aliongeza: “Kazi zenye staha siyo tu haki ya mfanyakazi, bali ni wajibu unaochochea matokeo chanya kwa Taifa.’

Aidha, ameeleza kuwa matarajio ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa taasisi na mashirika ya umma ni kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kuzingatia misingi ya utawala bora, na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta thamani halisi kwa uchumi wa Taifa.

Ameongeza kuwa ubunifu, matumizi sahihi ya rasilimali na uwazi katika utoaji wa taarifa ni nguzo muhimu katika kuimarisha imani ya umma.

Katika muktadha wa utekelezaji wa Dira 2050, Ofisi ya Msajili wa Hazina imebainisha kuwa mashirika ya umma yanatarajiwa kuwa injini ya ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji wenye tija, utoaji wa michango na gawio stahiki Serikalini, pamoja na kuchangia ajira na maendeleo ya kijamii.

Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa la kutathmini mchango wa wafanyakazi na kuhimiza mazingira bora ya kazi, sambamba na kuongeza msukumo wa utekelezaji wa sera na mikakati inayolenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050.

Ofisi ya Msajili wa Hazina imehitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wote wa mashirika ya umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na maadili ya hali ya juu ili kuhakikisha malengo ya Taifa yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.