Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ameshiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zilizofanyika kitaifa mkoani Njombe, yaliyobeba kaulimbiu: “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imeeleza kuwa Rais Dkt. Samia ametambua mchango mkubwa na muhimu wa wafanyakazi katika uchumi wa nchi na maendeleo ya Taifa, na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi, maslahi na ustawi wa wafanyakazi nchini kadri uchumi utakavyoimarika.
Ameongeza kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ni matokeo ya jitihada za pamoja baina ya Serikali, wafanyakazi, waajiri na wadau wengine wa maendeleo, hususan sekta binafsi, na hivyo kusisitiza wajibu wa kila mmoja kutimiza nafasi yake kwa weledi, uadilifu na uzalendo.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya kazi kupitia nyongeza za mishahara, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii, kuboresha usalama na afya mahali pa kazi, pamoja na kuendeleza majadiliano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi.
Halikadhalika, amewataka wafanyakazi kuendelea kuwa chachu ya uzalishaji, ufanisi na nidhamu kazini, akiongeza kuwa Serikali itaendelea kusikiliza hoja za wafanyakazi kwa utaratibu, kwa kuzingatia uwezo wa uchumi, sheria za nchi na maslahi mapana ya Taifa.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kukuza ujuzi, hususan kwa vijana, ili kuwaandaa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaohitaji maarifa, teknolojia na ubunifu.
“Dhamira ya Serikali ni kuona kila mfanyakazi anafanya kazi katika mazingira salama, yenye heshima, haki na yanayomwezesha kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” amesema Rais Dkt. Samia.
Akiwasilisha Risala kwa niaba ya Wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Ndugu Herry Mkunda, amepongeza jitihada za Serikali katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo nyongeza ya mishahara, kuboresha mazingira ya kazi na majadiliano ya wadau wa utatu, huku akiiomba Serikali kuendelea kuimarisha hifadhi ya jamii, usalama kazini na fursa za ajira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zimeimarisha huduma za jamii na mazingira ya uzalishaji, ikiwemo uwekezaji katika afya, elimu, miundombinu na sekta za kiuchumi zinazogusa moja kwa moja maisha ya wafanyakazi na wananchi.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dkt. Oscar Mgaya, amepongeza hatua za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na ajira, ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, akisema hatua hiyo itaongeza uwekezaji wa sekta binafsi na kutengeneza fursa zaidi za ajira zenye staha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala, ameipongeza Tanzania kwa kuimarisha ajenda ya kazi zenye staha, haki za kijamii na majadiliano ya wadau wa utatu katika sekta ya kazi.
Ameongeza kuwa, ILO itaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kazi zenye Staha, kuimarisha sheria na viwango vya kazi, kukuza ujuzi kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha mifumo salama ya ajira kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.










