Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora kimepitisha majina ya makada wake wawili watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha kuwania udiwani katika Kata za Itilo na Ziba.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanya jana Mjini hapa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Nkumba ametaja makada walioteuliwa kuwa ni Themistocles Norbet atakayewania udiwani katika Kata ya Ziba Wilayani Igunga.
Mwingine ni Michael Sabi Kaswiza atakayewania udiwani katika Kata ya Itilo Wilayani Nzega nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nzega Mji Nzega aliyefariki kwa ajali ya gari.
‘Mchakato wa vikao vya chama kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa umekamilika, na hawa tunaowatangaza leo ndio wamekidhi vigezo na sifa za kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo ili kukabiliana na wagombea wa upinzani’, amesema.
Mwenyekiti ameeleza kuwa baada ya kuteuliwa, majina hayo yatawasilishwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (I-NEC) kwa ajili ya taratibu zingine za uchaguzi ili kujaza nafasi hizo zilizoachwa wazi na madiwani wa CCM waliofariki dunia.
Ameeleza bayana kuwa mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea umefanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia sifa na uwezo wa kila mgombea, hivyo akawataka wanaCCM, Viongozi wa chama na watia nia wengine wote kuwaunga mkono.
‘Mchakato wa uteuzi umemalizika, kazi iliyoko mbele yetu sasa ni kushikamana wanaCCM wote katika hatua zote za kampeni ili kuhakikisha Chama chetu kinaibuka kidedea katika uchaguzi huo, ili kurudisha Kata zetu’, amedokeza.
Akiongea katika Kikao hicho Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa huo (MNEC) Mohamed Nassoro Hamdan amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa mkutano huo kwa kuteua wagombea sahihi wa CCM.
Aidha amewataka wanaCCM waliomba kuteuliwa lakini wakakosa kutovunjika moyo, bali waungane kuwaombea kura wenzao ili wakati wao ukifika nao waungwe mkono huku akionya kuwa huu sio wakati wa kutengeneza makundi ndani ya chama.





