Ukosefu wa ajira kwa vijana wenye elimu ya juu ni miongoni mwa sababu zinazochangia uchumi wa nchi kuporomoka, huku vitendo vya uhalifu vikiongezeka katika jamii.

Akizungumza na JAMHURI, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, amesema ukosefu wa ajira kwa vijana unaweza kusababisha kurudi nyuma kimaendeleo pamoja na kuchangia vitendo vya uhalifu kuongezeka.

“Unakuta vijana wanaingia katika uvutaji bangi na kusababisha uhalifu kuongezeka katika jamii,” amesema Prof. Moshi.

Amesema ajira kwa vijana hasa wenye elimu ya juu, ni jambo la muhimu kwa sababu wanasoma kwa ajili ya kulitumikia Taifa kupitia taaluma zao.

“Yapo madhara ya kiuchumi kama kuna ukosefu wa ajira kwa vijana, kwani vijana ndiyo nguvukazi ya Taifa na wanapaswa kufanya kazi ili kuleta maendeleo,” amesema Prof. Moshi.

Profesa huyo wa uchumi amesema ili kutatua tatizo la ukosefu wa ajira, Serikali inatakiwa kutengeneza mazingira rafiki kuwa na kilimo cha umwagiliaji, jambo linaloweza kupanua wigo wa upatikanaji wa ajira.

“Kuna na mito na maziwa ambayo hutiririsha maji mwaka mzima, maji hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji, kwani kufanya hivyo kunaweza kusaidia katika masuala ya kiuchumi katika upatikanaji wa ajira, maana sekta ya kilimo huajiri watu wengi zaidi,” amesema Prof. Moshi.

Amesema wapo vijana wanaofanya shughuli ya kilimo na kupata mafanikio makubwa, kwa sababu asilimia kubwa wanapenda kilimo  kinachoweza kuwaingizia kipato kila siku.

Mchumi huyo anaeleza kuwa vijana wanaofanya shughuli za kilimo asilimia kubwa mashamba yao yapo karibu na vyanzo vya maji, ili kuepuka mazao yao yasikauke.

“Vijana wanapenda kilimo kinacholipa hasa kilimo cha umwagiliaji, ili kuepuka changamoto ya ukame na kusababisha mazao yao kukauka na kupata hasara,” amesema Prof. Moshi.

Amesema jambo la msingi ni kuhakikisha kunakuwa na maji ya kuaminika pamoja kwa miundombinu rafiki ya umeme sambamba na gharama ndogo ya huduma ya umeme itakayosaidia kuhamasisha wawekezaji katika sekta ya kilimo.

“Kufanya hivyo kutasaidia kufikia malengo ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda kwa kufuata sera ya kuboresha miundombinu ya kilimo na kuhakikisha uchumi unakua,” amesema Prof. Moshi.

Hata hivyo, amebainisha kuwa viongozi waliopo madarakani wanatakiwa kuelekeza nguvu zao maeneo ya vijijini kwa sababu kuna ardhi kubwa ambayo bado haijafanyiwa kazi.

“Nimefika vijiji vilivyopo mikoa ya Mwanza na Mara ambako asilimia kubwa ardhi yake ni mapori na haifanyiwi kazi na mtu yeyote katika kilimo,” anasema Prof. Moshi.

Hata hivyo, ametoa mwito kwa vijana kubadilika na kuachana na tamaa ya kupata mafanikio kwa kipindi kifupi badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa bidii hasa pale wanapopata fursa.

Madhara kwa Bodi ya Mikopo

Mkurugenzi Msaidizi, Urejeshaji wa Mikopo Elimu ya Juu (HESLB), Dk. Abdul Mussa, amesema endapo wadaiwa watachelewa kuanza kulipa madeni, wanapata madhara katika utendaji wao.

Amesema fedha zinazotumika kuwasomesha Watanzania ni mkopo ambapo baada ya kumaliza masomo yao ndani ya miaka miwili wanapaswa kuanza kurejesha.

Dk. Mussa amesema kuwa kuchelewa kuanza kurejesha fedha hizo kunaweza kupunguza idadi ya wasomi  waliokuwa wanategemea kusoma kupitia fedha za Bodi ya Mkopo.

“Wadaiwa wakichelewa kuanza kulipa mikopo tutakuwa tunasomesha idadi ndogo ya Watanzania wenye uhiitaji wa kupata elimu ya juu,” amesema Dk. Mussa.

Amesema utaratibu wa urejeshaji wa mikopo unaendelea, huku akieleza kuwa sheria ya kwanza ya kurejesha mikopo ilikuwa inamtaka mnufaika kurudisha mkopo ndani ya miaka 10 baada ya kumaliza masomo yake.

Amesema kuwa baada ya kuona kuna malalamiko kuhusu sheria ya kurejesha mikopo, bodi iliamua kubadilisha sheria hiyo na kuanza kukata asilimia 8 ya mshahara wa mnufaika kwa kila mwezi.

Dk. Mussa anasema kuwa sasa kuna mabadiliko ya sheria mpya ya kurejesha mikopo, ambapo kuanzia Januari mwaka huu wameanza kukata asilimia 15 ya mshahara wa mnufaika kwa kila mwezi.

Hata hivyo, amefafanua kuwa mpaka sasa mikopo iliyopo nje ni Sh trilioni 2.595 ambayo ni sawa na wanufaika 379,179  wanaodaiwa na Bodi hiyo.

Dk. Mussa anasema kuwa hadi Septemba mwaka jana, mikopo iliyokuwa tayari inatakiwa kuanza kulipwa ni Sh trilioni 1.4 sawa na wanafunzi wanufaika 238,516 wanaopaswa kuanza kulipa madeni yao.

Hata hivyo, anaeleza kuwa mpaka sasa wamekusanya  Sh bilioni 146 kati ya bilioni 427 ambazo zimeiva katika mfumo wa kurejesha mikopo.

Dk Mussa amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa mikopo wa elimu ya juu haingiliani na suala la ajira, hivyo lazima mdaiwa alipe bila kuangalia kama amepata ajira.

Kwa mujibu wa sheria ya bodi ya mikopo, mtu anapaswa kuanza kulipa baada ya miaka miwili kumaliza masoko yake, hivo kama hajafanikiwa kuanza kulipa atawajibika kulipa faini ya asilimia 10 jumla ya fedha anazodaiwa.

“Watu wanapaswa kuwajibika kulipa mikopo hayo,” anasema Dk. Mussa.

Dk. Mussa amesema kuwa kadiri muda unavyozidi kwenda kuna uwezekano wadaiwa wakakosa baadhi ya huduma hapa nchini mpaka waanze kulipa mikopo.

 

Wanufaika wa Mkopo wa elimu ya juu.

JAMHURI imezungumza na baadhi ya wanufaika wa mikopo wa elimu ya juu ambao hawakutaka kutajwa gazetini, wameonekana kuwa na wakati mgumu kutokana na kuwepo kwa changamoto ya ukosefu  wa  ajira pamoja na kulipa deni kutoka bodi ya mikopo.

Wamesema kuwa upatikanaji wa ajira imekuwa changamoto hapa nchini hali inayosababisha kushindwa kuanza kulipa madeni yao.

Wanaeleza kuwa hata wale ambao wamefanikiwa kupata ajira wameanza kuwa katika wakati mgumu wa maisha kutokana wameanza kukatwa 15%  ya mishahara wao kila mwezi.

“Sasa wananikata asilimia 15 ya mshahara wangu na ukizingatia napokea mshahara mdogo na kusababisha niishi katika mazingira magumu kiuchumi” anasema mmoja wa wanufaika na mkopo.

Wamebainisha kuwa umakini unaitajika katika kuhakikisha kila mtu analipishwa kiasi anachodaiwa kwani baadhi yetu wamekuwa na malalamiko kuhusu kuanza kulipisha madeni ya watu wengine

Hata hivyo wameitaka bodi ya mikopo kufikiria kupunguza 15% ya makato mishahara kwa kila mwezi kwa wadaiwa  kutokana imekuwa kikwanzo kuhusu kulipa deni bodi ya mkopo

By Jamhuri