Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, anachunguzwa na vyombo vya dola kuhusiana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, JAMHURI linathibitisha.

Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI na kuthibishwa na mamlaka mbalimbali, jina la mbunge huyo ambaye ni mtoto wa Rais (mstaafu), Jakaya Kikwete, limo katika orodha ya majina 97 aliyoikabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Siyanga.

Orodha ambayo JAMHURI imeiona, inaonesha kuwa Ridhiwani ni mmoja wa watu wanaochunguzwa na taarifa za uhakika zinaonesha kuwa wakati wowote atawekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa.

“Kaka nakwambia Serikali hii imebadilika, na mambo yamebadilika. Rais [John] Magufuli hana simile katika vita ya dawa za kulevya. Hata huyo Siyanga aliyemteua, itabidi afanye kazi bila woga maana Rais Magufuli hana woga wala nia ya kumwonea mtu, ila anasema katika vita hii hana simile,” anasema mtoa habari wetu.

Jumatatu, Februari 13, wakati Rogers William Siyanga anakabidhiwa orodha ya watu  hao 97, alisema hataacha jiwe lolote bila kugeuzwa.

Siyanga alipoulizwa na JAMHURI juu ya Ridhiwani kuchunguzwa alisema kwa ufupi: “Kila taarifa tunayoipata tunaifanyia kazi kwa kina.”

Rais John Magufuli naye ameunga mkono vita hii iliyoanza wiki ya Februari, 2017 kwa kusema: “Hakuna cha umaarufu, ukishika hawa wote wanaovuta madawa ya kulevya wote, wakaeleza nani aliwauzia, na huyo aliyewauzia mkimshika atawaeleza aliyapata wapi, na huyo naye mkimshika atawaeleza ameyapata wapi.

“Lazima mtengeneze hiyo chain (mnyororo) yote ya kuhakikisha watu wanaohusika na madawa ya kulevya wanashughulikiwa kikamilifu. Ninajua mtapata vipingamizi vingi, hata IGP ulipigiwapigiwa simu. Wengine wakawa wanakupa advice (ushauri) fulani, ninajua na nashukuru hukuwasikiliza. Ungewasikiliza ningejua na wewe unahusika, na leo usingekuwa IGP.

“Kwa hiyo, nakupongeza sana, umesimama imara, maana uharibifu wa madhara ya madawa ya kulevya, unaliangamiza Taifa hili. Katika vita hii ya madawa ya kulevya, hakuna cha mtu aliye maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri au mtoto wa fulani, ambaye akijihusisha aachwe. Hata angekuwa mke wangu, Janeth hapa, hata akijihusisha wewe shika tu mpeleke.

“Kwa sababu… kwa sababu madhara ya madawa ya kulevya kwa Taifa letu sasa yamefikia mahali pabaya. Haiwezekani watu wanakuwa wanauza kama njugu. Si siri, sisi wote hapa tuliopo tunafahamu kwamba madawa ya kulevya yanapoteza nguvukazi ya Watanzania wengi, na hasa vijana. Kwa hiyo, naagiza vyombo vyote, Jeshi la Polisi na wengine wote wanaohusika, endeleeni kufanya kazi zenu. Hii kazi si ya Makonda tu, ni ya Watanzania wote. Shika yoyote. Peleka mahakamani.”

JAMHURI limezungumza na Ridhiwani Jumamosi, Febuari 18, jijini Dar es Salaam kuhusiana na tuhuma hizo na iwapo amejiandaa kuhojiwa na vyombo vya dola ikiwamo polisi au Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, na amesema yeye yuko tayari muda wote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, ila akasema:

“Tuwaache waendelee na kuchunguza watakapojiridhisha sheria ichukue mkondo wake. Lakini pia, watakapoona hatuhusiki, wawe tayari kutusafisha.”

Alipoulizwa iwapo anazo taarifa zozote juu ya kuchunguzwa kwake na jina lake kuwamo kwenye orodha, amesema; “Sina taarifa na wala sina hofu yoyote. Acha wachunguze tu. Sina cha kuficha, niko safi kabisa.”

JAMHURI lilipomuuliza juu ya taarifa zilizosambaa mitandaoni kuwa amewahi kukamatwa nchini China na ‘unga’ hadi baba yake, Rais (mstaafu) Kikwete akaingilia pamoja na utajiri mkubwa anaodaiwa kuumiliki, akasema: “JAMHURI  tulihojiana mwaka 2014. Nilijibu maswali haya na majibu yangu ndiyo hayohayo, mkawafikishie wananchi, hakuna kilichobadilika.”

Mahojiano kati ya JAMHURI na Ridhiwani, Aprili, 2014 yalikuwa hivi:

JAMHURI: Hivi karibuni zilisambaa taarifa kuwa ulikamatwa nchini China ukiwa na dawa za kulevya. Likoje hili?

RIDHIWANI: Mimi siwezi kujisemea, rekodi zangu zipo. airport Sijawahi kufika China, India, Israel, wala Palestina. Kwa Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati nchi pekee niliyokwenda ni Dubai tu. Tarehe inayosemwa kuwa nilikamatwa China, ilikuwa ni siku ya Uhuru wa Burundi au Rwanda. Siku hiyo mzee [Kikwete] alikuwa in one of those countries (katika moja ya nchi hizo).

Kwamba mimi nilikuwa nimekamatwa China na mzee wangu akaitwa, ni upuuzi mtupu. Kwanza China si safari ya nusu saa, ni safari ya zaidi ya siku mbili. Sasa wamechonga habari hii eti mzee akaenda kunikomboa China nikiwa nimeshikiliwa… Yote haya ni kampeni za kujaribu kuchafua jina langu. Sijawahi kufanya biashara hiyo [ya dawa za kulevya], na siweza kufanya hivyo.

JAMHURI: Kuna taarifa kuwa wewe ni tajiri mkubwa hapa nchini na umepata utajiri usioelezeka ndani ya muda mfupi. Ukweli ukoje?

RIDHIWANI: Maneno haya nimeyasikia kila kona. Nimesingiziwa ninamiliki mali nyingi ajabu. Kila kampuni inayoanzishwa naambiwa ni yangu. Kila jengo kubwa na refu hapa nchini wanasema ni la Ridhiwani. Na sasa nadhani kimebaki kitu kimoja –  kunikabidhi wake za watu – maana nchi hii kila kampuni naambiwa ya kwangu. Kila kitu, jamaani!

Pamoja na maneno mengi sana, sitetereki kwa sababu moja kubwa ni kwamba niliandaliwa kukabiliana na hali hii. Wakati mzee wangu anaingia kwenye siasa (kuwania urais) nilikutana na Abdallah Mwinyi (mtoto wa Rais mtaafu Mzee Mwinyi), akaniambia changamoto nitakazokutana nazo kama mtoto wa rais, na sasa nazishuhudia vilivyo.

Hivi sasa nasingiziwa kampuni ya ASAS (ya Iringa). Mwenye ASAS namfahamu, watoto wake akina Salim Abri nawafahamu na nilikutana nao nikiwa Iringa shuleni. Nilipofuatilia historia ya kampuni yao, kampuni ile ilianzishwa mwaka 1939. Miaka hiyo hakukuwapo na wazo la mimi kuzaliwa.

 Nilipoenda eneo la Ipogolo nikakuta kuna petrol station ya ASAS, sasa cha kushangaza, watu wanasema mimi nahusika kwenye ile kampuni. Nashindwa kuelewa mimi nahusikaje? Ila kibaya zaidi ukisema, kwenye memorandum za kampuni ninazosingiziwa kumiliki huwezi kukuta Ridhiwani ni sehemu ya umiliki. Watanzania wamejenga utamaduni wa kusema sana, siyo ASAS peke yake, wanasema kila kampuni ni yangu hapa nchini. Kila jengo refu wanasema ni langu. Mimi nasema sina biashara hizo. Labda baadaye Mungu akipenda.

Lakini ifahamike kuwa kufanya biashara si dhambi. Dhambi ni kufanya biashara ukawa na mali zisizoelezeka chimbuko lake. Kwa mfano, ipo siku nilisikia habari eti Mzee [Reginald] Mengi anadaiwa benki. Nikasema hawa wa ajabu kweli. Wanadhani huyu ana mwembe wa kupukutisha fedha, mfanyabiashara lazima akope na alipe. Kudaiwa benki si tatizo.

Njia mojawapo ni kuweza kuona opportunity (fursa) nzuri ambazo hazina migogoro ukafanikisha na kupatiwa kipato. Mojawapo ni hiyo kukopa fedha benki au kukopa kwa watu binafsi. Lakini wanaposema Ridhiwani ana hili, tuulizane, je, ni kweli anavyo hivi vitu? Hizi ni fitina tu.

Kinachonisikitisha, wanasiasa wanasikia mambo haya, wanayabeba na kuyachukua kwenye majukwaa ya kisiasa. Kipindi fulani Bwana [Dr. Wilbrod] Slaa akaenda kwenye mikutano akasema nina utajiri wa kutisha. Anataja kuwa nina magari mengi mno, ukimuuliza gari aina gani namiliki, hata rangi hajui.

Nimempeleka mahakamani na hivi karibuni hukumu itatolewa. Hatuwezi kumwachia. Mimi siwezi kumpiga ngumi – ni mzee wangu namheshimu sana. Sehemu pekee inayoweza kunipatia haki yangu ni Mahakama, ndiyo maana nimepeleka kesi mahakamani.

JAMHURI: Unasema unasingiziwa kumiliki mali. Hebu wewe eleza unamiliki nini?

RIDHIWANI: Mimi namiliki gari moja, nyumba moja, na hii nyumba nimepewa na Mzee [Rais Kikwete]. Nina viwanja viwili Bagamoyo, shamba jingine liko Chalinze na jingine Lugoba, basi. Sijawahi kutamani kufanya biashara ya mafuta, sina kiwanda, labda kampuni yangu ya sheria – GRK. Familia haina kiwanda cha mifuko ya karatasi kama inavyosemwa. Sisi tunalima mananasi tunauza.

JAMHURI: Kwa nini usingiziwe?

RIDHIWANI: Hii ni hulka tu imeibuka hapa nchini. Kwa hapa Dar es Salaam kitu pekee kilichobaki ni kukabidhiwa wake za watu. Mimi siwezi kufanya kitu chochote bila kumshirikisha mzee wangu. Hata kwenye kampuni yetu, tunapopata biashara kubwa siikubali hivi hivi. Maana najiuliza mtu asije kwa sababu Ridhiwani ni mwanasheria, akatumia jina langu, la mzee (Rais Kikwete). Hilo hatulifanyi.

JAMHURI: Katika kusingiziwa huko, ni lipi ulilosingizwa ambalo likakukera sana?

RIDHIWANI: Katika maisha yangu nilikerwa sana na stori iliyochapishwa na gazeti [jina linahifadhiwa] eti mimi nashiriki kwenye mpango wa kumpindua baba yangu. Hili liliniuma na kunikera sana. Yaani mimi nishiriki mpango wa kumpindua baba? Du, hii ni hatari.

JAMHURI: Ukiacha hizo mali unazosema unasingizwa, hivi kwenye akaunti wewe una fedha kiasi gani kwa sasa?

RIDHIWANI: Sina cha kuficha, na mimi sijapiga hesabu kwenye akaunti zangu kujua kuna kiasi gani, lakini sidhani kama ninaweza kuzidi shilingi milioni 20.

JAMHURI: Hivi maisha ya kuwa mtoto wa Rais yakoje?

RIDHIWANI: Ni maisha magumu sana. Mimi nadhani Rais ajaye ni vyema asiwe na watoto. Labda wawe kama mapapa. Unakuwa kardinali halafu ndiyo uwe Rais. Ukiangalia jinsi watu wanavyojaribu kuportray (kuonesha) picha ya mtu, ni tofauti.

Baba, ni mtu ambaye hana tamaa ya mali. Ni mtu anayeweza kufanikisha miradi ya mabilioni, lakini asitamani kuwa na senti tano. Ila nikiangalia jinsi watu wanavyomsema, mpaka mimi najiuliza kuwa huyu ndiye mzee wangu ninayemjua?

Yeye anasema ‘sina tamaa ya mali. Nina nyumba, shamba langu la Msoga, ng’ombe wangu, na nikistaafu wataendelea kunipa ulinzi na kunilipa pensheni, inatosha.’ Sisi hatuko huru hivyo. Watu wanakunyooshea vidole, wanasema huyu kafanya hivi, mara vile hadi inachosha. Juzi nimekwenda kwenye maziko Arusha, nimekutana na mtu akanisalimia kisha akaniuliza, ‘Ridhiwani ndiyo wewe? Nimeambiwa una fedha nyingi sana.’

Mimi nasema inawezekana watu hawanifahamu maisha yangu niliyozaliwa nayo, niliyokua nayo. Jamii ya Watanzania inalishwa maneno, hata kama jambo hujalifanya wanasema ama anatufanyia sinema, au anatulaghai. Nchi hii kwa sasa kila mtu ana tafsiri yake kwa kila jambo.

Tangu wiki ya kwanza ya Februari, Watanzania wapatao 400 wamekamatwa, wengine wamefunguliwa mashitaka na baadhi wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza au kutumia dawa za kulevya.

Kati ya watu mashuhusi waliohojiwa na polisi ni pamoja na Yusuf Manji, aliyefunguliwa mashitaka ya kosa la kutumia dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Mwingine aliyehojiwa na polisi ni Askofu wa Kanisa za Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, wasanii na watu mbalimbali wanaoendelea kuhojiwa.

Watendaji kadhaa wa Serikali walioshiriki kuruhusu uingizaji au upitishaji wa dawa za kulevya nchini tayari wameanza kukamatwa pia. Kwa sasa, kuna mapambano ya kila aina ya dawa za kulevya nchi nzima ikiwamo bangi, mirungi, heroin, cocaine, mandrax na dawa za kulevya aina nyingine zote.

4414 Total Views 3 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons