Ally Niyonzima ameachwa Azam!

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam wanakifanyia marekebisho kikosi chao. Wanasajili kila uchwao. Licha ya kufanya usajili mkubwa wa mastaa mbalimbali, lakini pia wameachana na baadhi ya mastaa. 

Mmoja wa mastaa walioachana nao ni kiungo raia wa Rwanda, Ally Niyonzima. Binafsi sijashituka na taarifa hizi za Niyonzima kuachwa na matajiri hao wa Chamazi! Huko nyuma niliwahi kutabiri hili jambo kuwa kuna kila dalili litakuja kutokea. Sasa limetokea. 

Niyonzima ni mmoja wa viungo mahiri na maridadi wawapo uwanjani. Katika timu za Kitanzania, hakuna timu inayoweza kukataa kuwa naye kikosini kwao, lakini ana shida moja inayommaliza. 

Shida hiyo ndiyo iliyofanya aachane na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.

Shida yenyewe ni kwamba, Ally hataki kuminyana akiwa uwanjani. Anapenda kucheza soka laini. Hapo ndipo yeye na Azam FC wamepishana na kufikia uamuzi wa kumuonyesha mlango wa kikatili ulioandikwa ‘Exit’. 

Kile kilichowahi kumuondoa Richard Djodi, yule raia wa Ivory Coast Azam FC, ndicho kilichomuondoa Niyonzima sasa katika klabu hiyo hiyo. 

Mpira ni mchezo wa kuminyana na kukimbia kilomita nyingi uwanjani bila kuchoka. Niyonzima hakuwa hivi na hakuzitaka kabisa kazi ngumu. Unachezaje mpira katika mtindo huu?

Djodi na Niyonzima walikuwa wanacheza kama nje ya uwanja wamepaki magari ya kifahari na akaunti zao zina Bil. 100 kila mmoja. Soka la kileo haliko hivyo. Soka la kileo ni ‘vita’.

Wanaume 22 wanaingia uwanjani kuminyana, kupambana, kuusaka ushindi kwa juhudi na maarifa. Kama hauwezi kuminyana na kupambana, unaondolewa kazini. Ndivyo ilivyo.

Soka la siku hizi linahitaji watu wanaoweza kupambana bila kuchoka.

Kuanzia Djodi wakati ule hadi sasa Niyonzima, hawa wote wawili wamejipiga wenyewe vitanzi. Wana vipaji vikubwa miguuni, lakini hawataki kuishughulisha miili yao katika kupambana. 

Wanacheza kistarehe uwanjani. Hawataki kujihangaisha au walau kuonekana wakijihangaisha. Wakipambana. Wakiipambania timu na nafasi zao kwenye timu. 

Sijui kama wengi tunawatazama viungo Mukoko Tonombe, raia wa DRC anayeichezea Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na Mhandisi Thadeo Lwanga, raia wa Uganda anayeichezea Simba pia ya Dar es Salaam. 

Hawa jamaa wanavyojitolea uwanjani ni kama vile kesho hawachezi tena soka. Kwamba wanamaliza kila kitu leo leo!

Mishahara wanayopokea wanaimwagikia jasho la kihalali kabisa. Hawaji uwanjani kutapeli kisha wakaenda kufanya kazi nyingine! 

Hawa mpira kwao ni vita. Wanapambana hadi tone lao la mwisho la jasho. 

Mimi binafsi sijashituka wala kushangaa Niyonzima kuachwa na Azam FC. Niyonzima ametuonyesha kitu kidogo sana kati ya vile vitu vingi alivyonavyo katika mwili wake. 

Ana mwili na kimo kinachomwezesha  kuminyana na kutunishiana msuli na kiungo yeyote nchi hii na akamshinda. Lakini hakuwa hivyo, au hayuko hivyo. Alikuwa kiungo goigoi aliyejipenda zaidi yeye binafsi kuliko kuipigania timu yake, Azam FC, akiwa uwanjani. 

Chirwa ni miongoni mwa mastaa walioachwa, lakini Chirwa anaondoka kama shujaa. Kuna vitu vya kukumbukwa ameviacha pale Chamazi. Hajaondoka mtupu kama Niyonzima aliyetuachia staili za mitindo ya nywele na michoro ya ‘tattoo’ katika mwili wake. 

Kama Niyonzima ataamua kuacha vitu vingi kisha akaamua kucheza mpira, atanufaika na kipaji kikubwa alichonacho, lakini kama hataacha kucheza kwa kujitolea atahesabika kama mmoja wa wachezaji mwenye vipaji vikubwa, lakini hawajanufaika na vipaji vyao.