vurugu-1

 

 

 

 

 

 

 

Kwa muda sasa nimefuatilia matukio yanayoendelea nchini. Nimesoma habari mbalimbali zinazoonesha askari polisi wakiuawa kwa risasi na kunyang’anywa bunduki katika maeneo kadhaa hapa nchini.
Tumesikia ‘magaidi’ katika mapango ya Amboni Tanga.  Vituo vya polisi vimetekwa. Tumeshuhudia wafanyabiashara wakigoma na kuipa amri Serikali.


Nikumbushie kidogo tu kuwa mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Ndogondogo, Joseph Minja, alikamatwa na kuwekwa ndani. Vyombo vya dola vikadai Minja amekiuka masharti ya dhamana, hivyo vikamfutia dhamana. Wafanyabiashara wakagoma nchi nzima. Bunge likajadili kwa dharura, muda mfupi baadaye Minja akaachiwa, badala ya kufuata taratibu za kisheria za kutumia mawakili kumpatia dhamana.


Ijumaa wiki hii, madereva wakagoma. Wakaishinikiza polisi kuachia wenzao 25. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, akatoa tamko nje ya mamlaka yake. Nikamsikia Kova, ambaye mamlaka yake yanaishia Dar es Salaam, akitoa maagizo kwa makamanda wa mikoa yote nchini kuwaachia madereva waliowakamata.


Kova akaingilia mamlaka ya Naibu Kamishna Mohamed Mpinga, ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani. Akaagiza kamera zote za kudhibiti mwendo barabarani nchini zisitishwe. Madereva wakashangilia. Kwa kutoa mfano wakaondoa magari kwa kasi ya ajabu kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo. Wananchi wakawashangilia madereva kwa ushindi dhidi ya dola.


Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, naye akaingilia mamlaka ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta. Akatoa tangazo la kufuta kanuni mpya iliyopaswa kuanza kutumika Aprili mwaka huu. Akawaambia hata mawaziri ambao hawapo atawafikishia salamu. Madereva wakashangilia, wakaimba “Mama, mama, mama!”
Kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, vijana wakaamua kuchukua sheria mkononi siku ya mgomo. Mtu anayemiliki gari kama Noah, akiwa amepakia ndugu zake ikawa anashushwa na kupekuliwa. Wakaporwa mali walizokuwa nazo. Wasafiri hawakuwa wengi pale Ubungo, ila umati wa vijana wenye hamu ya kupora ndiyo uliofurika.


Vurugu za madereva zimetokana na uamuzi wa pupa. Kanuni zilikuwa zinabadilishwa; kila baada ya miaka mitatu madereva watakapotaka kubadili leseni basi walazimike kulipa Sh 560,000. Kosa moja la barabarani likawa faini Sh 300,000, vituo vya ukaguzi visivyo na idadi barabarani na tabia ya trafiki kuwavizia maeneo yasiyo na vibao vya kasi ya 50.
Matukio haya ni mwendelezo wa vituko hapa nchini. Utakumbuka Serikali ilivyolazimisha yasiyowezekana! Ikasema Katiba Inayopendekezwa itapigiwa kura Aprili 30, leo Tume ya Uchaguzi (NEC) imekwishatangaza kuwa kura hizo hazipo. Sitashangaa tukiambiwa hata uchaguzi haupo, ikiwa daftari la wapigakura halitakamilika.


Jumamosi iliyopita kule Iringa eneo la Ipogolo, inadaiwa mtoto aligongwa na gari. Mara wananchi wakafunga barabara. Pale Ipogolo mlimani kama zinavyoonesha picha, kuna matuta. Yasingekuwapo, badala ya kufundisha watoto matumizi ya barabara, wananchi wangedai matuta na Serikali ingetii amri, kama ilivyofanya kwa wafanyabiashara na madereva.


Eneo la Kigogo, Dar es Salaam kama unatokea Tabata Dampo, barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. Cha ajabu, kila baada ya mita mbili, wananchi wameamua kuichimba barabara inayojengwa na kujiwekea matuta. Matuta yenyewe hayana viwango, ila kwa kiburi tu, wananchi kila mtu ameweka tuta nyumbani kwake na Serikali imesalimu amri.
Dar es Salaam chini ya himaya ya Kova, waendesha pikipiki wanapita hadi ofisini kwake kinyume na mwelekeo wa barabara. Wanatoka Posta Baharini kwenda Central Police, wakati barabara hiyo haipandishi. Wanafanya hivyo Barabara ya Nyerere na hakuna anayewakamata. Wakimgonga dereva wa gari wanaungana kama kunguru na kumshambulia.


Sitanii, nafahamu yapo mambo mengi katika nchi yetu, ila tunayo tunu moja ya Taifa, na hapa naiandika kwa herufi kubwa AMANI. Ni kwa viongozi wetu kutenda nje ya utaratibu wa kisheria nchi yetu inaelekea kusiko. Tumerejea enzi za ujima. Amani yetu inapotea kwa kasi. Leo watu hawaogopi tena dola. Wanaishinikiza Serikali kuvunja sheria.
Kova kicheo ni bosi wake Mpinga kwamba yeye ni Kamishna, Mpinga ni Naibu Kamishna. Inaweza ikawa hivyo pia kwa makamanda wengine wa polisi wa mikoa kwamba kicheo Kova ni bosi wao, ila kimamlaka hahusiki nao hata chembe. Mpinga ndiye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchi nzima, si Dar es Salaam tu na wala kimamlaka hayupo chini ya Kova.


Agizo la Kova kuondoa kamera zote za kupima mwendo barabarani, inawezekana alilitoa kufurahisha madereva, lakini ni kiama. Leo wakati kamera zipo angalia ajali zinazotokana na mabasi. Inawezekana Kova hafuatilii, ila aniambie ni siku gani amesikia lori limegongana na lori. Ajali karibu zote zinazochukua roho za Watanzania ni basi kugonga lori, basi kuparamia magari madogo au basi kuacha njia.
Sitanii, inawezekana hata hao matrafiki wanafanya makosa kuvizia magari njiani na wakati mwingine hizo kamera tayari zimewekewa ‘speed’ ya kufatutia hela. Unakuta madereva wengi wakikamatwa na kamera za mwendo wanaambiwa walikuwa kasi 62. Hii 62 karibu kila dereva ndiyo anayoambiwa. Inaonekana huu ni mtego. Ni kitanzi kwa madereva.


Kama kanuni ya kosa ingepandishwa na kuwa Sh 300,000 ilikuwa ni kuwaongezea kiwango cha rushwa matrafiki. Madereva wangesumbuliwa hadi wakakoma. Suala la kurudi shule kwangu si tatizo, ila hatukuelezwa iwapo wamefanya utafiti na kubaini kuwa dereva anapoendesha gari kwa muda mrefu ujuzi unazeeka! Vinginevyo hawa Chuo cha Usafirishaji (NIT) walikuwa wanabuni mradi wa kujipatia fedha!
Ndugu zangu Watanzania, nchi imemwagiwa petroli. Enzi za ujima watu walikuwa wanalinda haki zao kwa makundi, na hilo ndilo lililokuwa chimbuko la koo na makabila. Ukoo au kabila lilikuwa na wajibu wa kulinda haki za mtu wao. Walifanya hivyo hata kama ingebidi kwenda vitani. Walijua bila kupigania haki za ndugu yao katika kundi, baadaye wangemalizwa wote.


Leo nchi yetu imerejea katika ujima. Wafanyabiashara wanapigania haki zao kwa makundi, madereva wanapigania haki zao kama kundi, wananchi wanaishurutisha Serikali kuweka matuta barabarani, wanachoma moto matairi, kwa maana kuwa hawana tena hofu na Serikali. Vituo vya polisi vinatekwa. Wanakaa katika makundi, wanatunga sheria na kuzitekeleza bila kupitia bungeni.
Sitanii, najiuliza mbona enzi za Mwalimu Nyerere wananchi hawakuthubutu kumteka polisi au kituo cha polisi? Mbona barabarani hakukuwapo speed governor na ajali hazikutokea nyingi kiasi hiki? Mbona watoto na watu wazima walikuwa hawagongwi kwa wingi kiasi hiki barabarani? Mbona polisi waliheshimika kwa kiwango cha kuogopwa na leo wanachukuliwa kama ombaomba?


Jibu lipo. Tumefanya makosa. Polisi wameacha kusimamia haki. Enzi za Mwalimu Nyerere polisi asingeweza kumbambikia kesi mwananchi. Leo ukifika polisi utafikiri hawalipwi mshahara. Utadhani idara hiyo haitengewi fungu lolote. Mpaka nakala ya fomu kama PF3 mtu aliyeumizwa ndiye anayepewa akaitoe.
Trafiki kumbambikizia kesi dereva wala hajisikii vibaya. Maadili yameshuka kwa kiwango kikubwa. Nimeshuhudia eneo kama Majumba Sita pale Pugu Road katika njia panda ya Segerea, Dar es Salaam matrafiki wakionea watu mchana kweupe. Wanatengeneza msongamano wa magari makusudi kwenye taa hadi dereva taa ya kijana inazimika na kuwaka nyekundu akiwa amesimama katikati ya mlingoti wa taa kisha wanamwandikia faini Sh 30,000 au ‘wanaelewana’.


Yupo trafiki mwanamama amekaa kwenye kibanda, kila wakiishatengeneza msongamano wa kuchonga, magari yote yaliyoshindwa kutembea yakiwa katikati ya mlingoti wa taa anaagiza yatozwe fani.
Jumapili ya Machi 28, saa 7:03 mchana, alinitengenezea mazingira ya hivyo, nikampiga neno lenye upako na kumwambia aseme kweli kama yeye anamwogopa Mungu iwapo hawatengenezi makusudi foleni kuumiza madereva. Alipoona nazidi kumbana akaishia kusema: “Inye ndi Muhaya, abahaya muli bakorofi toina kukunda.”


Tafsiri ya maneno hayo ni kuwa mimi ni Mhaya, Wahaya ni wakorofi huwezi kukubali (kuwa umepita taa nyekundu). Baada ya hapo akaona nachelewesha mtego wao akaniambia nenda. Niliondoka nikiumia moyoni, na sasa nimepanga, na hili nalisema wazi. Nimeweka kamera ya video kwenye gari langu. Nikifika kwenye taa hizo nitaanza kurekodi wakati wanatengeneza foleni bandia, baada ya hapo tutaishia mahakamani na kudai fidia ya kupotezeana muda.
Najiuliza, ni Watanzania wangapi baada ya uonevu wa aina hii hawataona ulazima wa kuungana kama makundi na kuishinikiza Serikali kutenda watakayo? Binafsi sikubaliani na uendeshaji wa madereva wa mabasi. Wanakimbiza mno magari na hawaheshimu sheria za barabarani. Hata hivyo, sikubaliani na utaratibu wa kuwaonea.


Sijapata kuona sehemu yoyote duniani, ukiacha semina na kozi za muda mfupi zinazoweza kutolewa na hata vyama vya madereva wenyewe, ambako dereva anarudishwa darasani kuanza kufundishwa jinsi ya kuwasha gari. Nasema kama NIT walidhani huu ni wakati wa kuvuna fedha, basi wabuni mradi mwingine!


Sitanii, Serikali yetu imepoteza misingi ya haki. Mahakamani kesi zinasikilizwa kwa utaratibu unaolalamikiwa kwamba asiye nacho hana haki. Kwenye siasa wewe kama si mtoto au ndugu wa kiongozi basi ujue huwezi kupata nafasi. Wale walioko serikalini biashara wanapeana kwa ukoo. Wakihisi wewe una itikadi fulani au ni mfuasi wa wasiyetaka apate nafasi siku za usoni, hupewi biashara.


Yapata miaka minne iliyopita, Jenerali Ulimwengu aliandika makala akaipa kichwa cha habari kisemacho ‘Kila mtu na kamuhogo kake’. Makala hiyo sasa ndipo inathibitika pasi shaka. Kila mtu anapaswa kuchagua. Ama tujiunge makundi kudai haki zetu sawa na wanavyofanya Watanzania walio wengi kwa sasa, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa Taifa au tukubali kuonewa.


Serikali inapaswa kusoma alama za nyakati. Kama ni mafunzo, wakati umefika kuwarejesha polisi darasani wakaelezwe ukweli huu: “Kwamba msipowatendea haki wananchi, wananchi wakiendelea kuzoea mabomu ya machozi, na wakiona kwa kujiunga makundi kama walivyofanya madereva na wafanyabiashara haki yao inapatikana, kama nchi tuelekeze mawazo yetu na kufikiri kilichowakuta watawala huko Tunisia na Misri miaka miwili iliyopita.” Huu ni mwaka wa uchaguzi. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri