Al-Shabaab fightersSerikali imetakiwa iwe makini kuhakikisha inavitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na wananchi kukabiliana na tishio la makundi ya kigaidi, hasa al-Shaabab kutoka Somalia.
Mbunge wa Kigoma Kusini – NCCR-Mageuzi, David Kafulila ameliambia JAMHURI kwamba Tanzania inapaswa kuwa makini.
Anasema suala la ugaidi linalozungumzwa kila mahali nchini linaweza kufanyika kutokana na magaidi kutekeleza uhalifu huo bila kujulikana kirahisi.


Kwa mtazamo wake, magaidi wanaweza kuwa ndani na nje kwa kuwa waandaaji, watekelezaji na wafadhili wa vitendo hivyo inawezekana wanatoka ndani na nje ya nchi; tofauti na ilivyo nchini Kenya ambako inafahamika kuwa magaidi wa al- Shaabab wanatoka Somalia.
Kafulila anasema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushirikiana na wananchi kuwabaini watu ambao hawaeleweki wanafanya shughuli gani katika maeneo mbalimbali nchini.


Anasema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) zinapaswa kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na magaidi wa al- Shabab badala ya kuiachia Kenya pekee, kwa kupeleka majeshi yake Somalia kukomesha kundi hilo hatari.
“Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda zinazounda Jumuiya hii, kama zitashirikiana na kulichukua tatizo hili la ugaidi kwamba limeleta athari kwa nchi hizo zote inawezekana kuliondosha kabisa,” anasema.
Kafulila anaungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, anayesema kuwa hizi ni dalili mbaya kwa nchi maana suala la ugaidi haliangalii dini ya mtu wala kabila, bali ni kuchafuka kwa dunia.


Anaeleza kuwa ni vyema kila Mtanzania akajitazama na kujitathmini kutokana na mchafuko uliopo ambao umekuwa tishio la amani ya dunia huku nchi nyingi duniani zikikumbwa na tishio la ugaidi na kupoteza watu wake.
Anasema ni dhima ya kila Mtanzania kuhakikisha nchi inakuwa na amani. Anawashauri wananchi watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi linapobainika jambo lisilo la kawaida.
Anasema ugaidi kuhusishwa na masuala ya kisiasa ni vigumu kuubainisha ila ndani ya vyama hivyo wamo wanachama wachache ambao hawapendi kuona nchi ikiwa na amani.


“Dunia nzima ni lazima tujiulize tunakoelekea ni wapi? Mfano mzuri ni nchi jirani ya Kenya na hata Ulaya.
“Ni lazima kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu wake katika kukumbushana umuhimu wa amani duniani. Amani yako ni amani ya kizazi chako na cha baadaye. Amani inatengenezwa na binadamu ingawa vipo vichocheo vya kuharibu amani; hivyo tuipiganie, tuihubiri tusiipoteze,” anasisistiza Jaji Mutungi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ametoa tahadhari kwenye maeneo yenye mikusanyiko kama vile shule, misikiti, makanisa na kwenye sherehe.


“Serikali wawe makini katika hili, na raia wawe na ushirikiano wa kutoa taarifa. Hata jirani yako sasa hivi usimwamini kutokana na jambo lolote na Serikali inatakiwa itimize jukumu lake kwa maana ya ulinzi,” anasema Mgeja.
Mgeja anasema jitihada za mazungumzo zifanyike hata katika Uchaguzi Mkuu ili uwe huru na wa haki.


Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, anasema matishio ya ugaidi nchini ni hatari, lakini haamini kama mpango wa Tanzania kuwa na uhusiano na Marekani unaweza kuwa sababu za magaidi kutushambulia.
“Marekani imekuwa na urafiki mzuri na Tanzania kwa muda mrefu sasa, na magaidi hao wamekuwa wakifanya matukio katika nchi mbalimbali duniani,” anasema Zambi ambaye ni Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika; na kuongeza:


“Ugaidi huu unaofanyika ni kutokana na imani za watu fulani kuamini ya kuwa wakifanya vitendo hivyo viovu vya kuua binadamu wenzako watakwenda peponi. Hizi ni falsafa za watu na imani za watu wenye chuki ndani ya mioyo yao, si vinginevyo.”
Kuna hoja kwamba wakati Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu mwaka huu huenda chama tawala kikatumia suala la ugaidi kujenga hofu ya kiusalama kwa wapigakura.


Mbali ya al-Shaabab makundi mengine yanayoongoza kwa ugaidi kwa muda huu ni ISIS, al-Qaeda na Boko Haram la Nigeria.
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Aljazeera, mawasiliano ya hivi karibuni ya ISIS yanabainisha kuwa inajaribu kujijenga Afrika Mashariki, eneo ambalo limekuwa ngome ya al-Shabaab na al-Qaeda.


Hivi karibuni, kikundi cha kigaidi cha Boko Haram cha Nigeria kimetoa ahadi ya utiifu kwa ISIS, hatua iliyotafsiriwa na wachunguzi wa masuala ya ugaidi kuwa inaweza kuongeza nguvu za ISIS katika maeneo mbalimbali barani Afrika.
Kitendo cha Boko Haram kuonyesha utii wa ISIS kilitanguliwa na ujumbe uliotumwa kwa kiongozi wa al-Shabaab, Abu Ubaidah, kumwomba afanye kama walivyofanya Boko Haram (kutangaza utii kwa ISIS).
Ujumbe huo uliwasilishwa na Hamil al-Bushra, jina linaloaminika kutumiwa na vyanzo viwili vya habari vinavyohusishwa na ISIS.
Katika ujumbe huo, Bushra aliwapongeza al-Shabaab na kuwahamasisha wafanye mashambulizi Kenya, Ethiopia na Tanzania.


Wiki mbili zilizopita, magaidi wa al-Shabaab walifanya shambulio kubwa la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa, mpakani mwa Kenya na Somalia. Watu 148 waliuawa katika shambulio hilo.
“Hii ni kutokana na uzembe wa Kenya yenyewe,” anadai Abu Ubaidah ambaye anasema kwamba alitahadharisha Kenya kwa kuitaka ihamishe ‘base’ yake ya kijeshi iliyoko Manda Bay.
Machi 25 mwaka huu, Marekani ilitoa tahadhari kwa Uganda kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi nchini humo.
Kama ilivyo kwa Kenya, Marekani ina maslahi yake nchini Uganda ambako inarusha ndege zake za upelelezi (PC 12) kutoka Entebbe.


Hapa nchini, hivi karibuni mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kaisi bin Abdallah alidai kuwa kundi lao la kigaidi limekuwa na mafanikio kwa kudhuru kujeruhi na kuua polisi.
 
Wasemavyo wananchi
Jijini Dar es Salaam, Respicius Mboya (40) ambaye ni mkazi wa Tegeta, anasema vitisho vya ugaidi nchini visipuuzwe hata kidogo. Hofu yake ni kwamba wanasiasa wanahusika kwenye sakata hili.


Anasema suala la usalama nchini liko vizuri na anavyosikia matukio ya kigaidi nchini kama lile la Amboni, Tanga halieleweki.
“Inaonekana hili lilisukwa kufanikisha matakwa ya kisiasa ya baadhi ya watawala na kuyahamisha mawazo ya wananchi kutoka kwenye sakata la Escrow, Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu; kuwapeleka kwenye ugaidi.


“Serikali hii ni dhaifu mno, inapaswa kufanya mambo kwa uwazi na kuzingatia sheria badala ya kuwahadaa wananchi kwa namna yoyote ile; vinginevyo inaleta mgawanyiko ambao utaitowesha amani ya nchi,” anasema Mboya.
Prosper Temba (32) mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, anasema tishio la ugaidi nchini haliwezi kukwepeka licha ya kuonekana ni mbinu zinazopangwa kutekeleza masuala ya kisiasa kwa wanasiasa walioishiwa hoja, kutokana na uzembe na ubabaishaji uliopo kwenye idara za Serikali, ikiwamo Idara ya Uhamiaji ambayo baadhi ya watumishi wake wamekithiri kwa rushwa.


Temba anasema kwa utawala wa awamu hii ya nne inayotuhumiwa kwa rushwa na ubadhilifu wa kila namna, mgeni anathaminiwa zaidi kuliko Mtanzania mzawa, jambo ambalo anasema limewakatisha tamaa wananchi wengi.
Anasema nchini hakuna ajira, wananchi wanaishi kwa shida, vyakula vinapanda bei kila kukicha na sasa Serikali imezuia ajira kwa madai ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.
“Jambo hili linaonesha wazi kwamba uongozi wa awamu hii umeyumba. Heri ya utawala wa awamu ya tatu, chini ya Benjamin Mkapa, bei za vyakula zilikuwa za chini na nidhamu ilikuwapo serikalini,” anasema.


Kwa upande mwingine, Joyce Moses (30), mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, anasema vitisho vya Tanzania kushambuliwa na magaidi visifanyiwe mzaha na viongozi kama wanavyopuuzia masuala mengine, bali vichukuliwe kwa uzito mkubwa kwa kuvishirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wananchi.
Anasema matukio ya ugaidi yanaweza kutengenezwa na baadhi ya watu kwa lengo la kutekeleza siasa uchwara ambazo hazina nia ya kuwaletea wananchi maendeleo, bali machafuko.
Mhandisi Ngagani Simon wa Manispaa ya Shinyanga, anasema suala la ugaidi linakosesha amani.


“Mimi siamini kwenye uislamu kuhujumu ukristo au ukristo kuhujumu uislamu kwa sababu wanaachana kwenye kuabudu ila tunayemwamini ni mmoja tu,” anasema na kuongeza: “Kinachotakiwa ni kuheshimiana tu ili amani ipatikane na kuheshimu imani za watu.” Anasema kwamba Serikali ina wajibu wa kuwalinda wananchi wake kwa kutumia vyombo yote vya ulinzi na usalama kuhakisha amani inaendelea kustawi.


Mkazi wa Mbeya, Joshua Edward (25) anasema amesikia na kusoma kwa kina juu ya Tanzania kuvamiwa hasa katika baadhi ya mitandao ya jamii, hivyo ametoa mwito kwa kutaka hatua madhubuti za usalama ziimarishwe.
Anasema usalama uimarishwe kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa na kuwapatia wananchi elimu waelewe madhara ya kujihusisha na ugaidi.
Oscar Mwenda (30) wa Mbeya naye anaiomba Serikali iongeze ulinzi vyuoni, hasa vyuo vikuu ambako kuna mikusanyiko mikubwa ya wana vyuo.

 

5132 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!