Naomi Marijani (36), mama wa mtoto mmoja, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ametoweka katika mazingira yenye utata kiasi cha kujengeka hisia kuwa ameuawa, JAMHURI linaripoti.

Hadi leo zimetimia siku 63 tangu Naomi ametoweka katika mazingira yenye kuacha maswali mengi huku polisi wa Kigamboni wakionekana kutolipa kipaumbele suala la kupotea kwake, japo ushahidi wa mazingira unabainisha wazi mtuhumiwa wa kwanza ni nani.

Uchgunguzi uliofanywa na JAMHURI umebainisha kuwa kabla ya kutoweka kwake familia ilikuwa na mtafauruku usioelezwa chanzo chake. Pia baada ya kutoweka Naomi zinadaiwa kutengenezwa ‘meseji’ kupitia simu yake zikionyesha anamuaga mumewe na ‘kutimkia’ nje ya nchi kwenda kuanza maisha mapya.

Hata hivyo, kazi iliyofanywa na timu ya JAMHURI imebainisha kuwa Naomi hajawahi kumiliki hati ya kusafiria, Mei 15, 2019 na mwezi mmoja baadaye hajapita mpaka wowote wa Tanzania, wala uwanja wa ndege wowote kwenda nje ya nchi.

Naomi, mtu anayedaiwa kuwa amesafiri nje ya nchi katika nyumba alipokuwa anaishi na mumewe kuna nguo zake zote, kadi za benki na vitambulisho vyake vyote vipo nyumbani kwa mumewe.

Naomi, kwa jina jingine Sandra, ametoweka kwenye mazingira hayo ya kutatanisha kuanzia Mei 15, 2019 akiwa nyumbani kwake Gezaulole, Kigamboni ambako alikuwa anaishi na mumewe, Khamis Said Luwongo (38) kwa jina jingine Meshack, pamoja na mtoto wao, Grecious mwenye umri wa miaka saba.

Hakuna taarifa yoyote ya kupotea kwa Naomi iliyotolewa na mumewe au mtu yeyote anayeishi au kufanya naye kazi, hadi siku tatu baada ya kutoweka kwake Mei 18, 2019 ndipo mume wa Naomi, Meshack alikwenda nyumbani kwa mzee Robert Mchome, Mabibo (Dar es Salaam) na kutoa taarifa kuwa Mei 15, 2019 saa 01:30 jioni alipokea ‘meseji’ kutoka kwa mkewe kupitia namba 0655 527 203 (namba aliyokuwa akiitumia Naomi mke wake) ikisema: “Naondoka na mtoto namwacha nyumbani peke yake na kesho nasafiri nje ya Tanzania.”

Luwongo alidai kuwa baada ya takriban dakika 10 baadaye, saa 01:41 pia alipokea ‘meseji’ ya pili ikisema: “Na hutonipata kwa namba hii tena, hudumia mtoto vizuri,” ujumbe uliotumwa kwenda namba zake (Luwongo) 0685043374 na 0714812530.

Aliongeza kuwa, alirudi nyumbani kwake (siku hiyo ya Mei 15) saa tatu usiku na kukuta mtoto akiwa peke yake, akaenda kumnunulia chakula akala, siku iliyofuata akamwandaa mtoto kwa ajili ya kwenda shuleni.

Katika mazingira hayo, baadhi ya ndugu wa Naomi wamejiuliza maswali mengi baada ya Meshack (Luwongo) kutoa maelezo hayo kwa mzee Mchome. Miongoni mwa maswali wanayojiuliza ni: “Mkewe kadai kamtaarifu ameondoka na kamwacha mtoto siku ya Jumatano, Mei 15, 2019; na kweli akakuta mtoto yuko peke yake, kwa nini hakupiga simu kokote kumuulizia mke wake siku hiyo?

“Siku iliyofuata – Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi asubuhi ndiyo anafunga safari kwenda Mabibo kutoa taarifa. Je, ni kitu gani kilikuwa kinaendelea ndani ya hizi siku tatu; Jumatano, Alhamisi na Ijumaa?” anahoji mmoja wa wanandugu aliyeongeza kuwa hadi Mei 18, Meshack alikuwa hajatoa taarifa polisi.

Ndugu wa Naomi, Wiseman Marijani, ameliambia JAMHURI kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo, sehemu ya wanafamilia walikwenda Kigamboni kutafuta ukweli, na wakaanzia kwa muuzaji wa duka la dawa ambalo ni mali ya Naomi, anayejulikana kwa jina la Anna.

Anasema walipomuuliza Anna ni lini mara ya mwisho alimuona Naomi, aliwajibu kuwa Jumanne ya Mei 14, 2019 na kwamba siku hiyo walishinda wote dukani na aliondoka saa mbili usiku, na ilipofika saa tatu na nusu usiku Anna alifunga duka na kumpelekea mauzo ya siku hiyo Naomi, ambapo alimkuta nyumbani na kumkabidhi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Mei 15, 2019, saa 01:44 hadi saa 01:50 asubuhi simu ya Naomi iliwasiliana kwa ujumbe mfupi na dada mmoja anayefanya biashara ya huduma ya pesa kupitia mitandao ya simu. Katika mawasiliano hayo, simu hiyo ya Naomi ilimwomba “Dada wa Tigo-Pesa” amtumie Sh 75,000.

Hapa ndugu mwingine wa Naomi, Salma Marijani, anasema: “Huyo dada (wa Tigo – Pesa) tulipomhoji alidai kuwa walipokuwa wakiwasiliana kwa ujumbe mfupi na simu hiyo ya Naomi, yeye hakuwepo dukani, kwa hiyo akamuahidi

kumtumia kiasi hicho cha fedha baadaye kidogo. Ilipofika saa 04:13 asubuhi alimtumia Sh 75,000.

“Baadaye, saa mbili usiku Anna (wa duka la dawa) alifuatwa na dada wa Tigo – Pesa na kumwambia kuwa nyakati za asubuhi ‘alimrushia’ Naomi Sh 75,000 kwa makubaliano kuwa atarudishiwa fedha hizo na Anna jioni ya siku hiyo, Mei 15, 2019.

“Ili kujiridhisha, Anna naye alimpigia simu Naomi kwenye namba 0655527203, simu iliita, lakini haikupokewa, akatuma ‘meseji’ – haikujibiwa, alipojaribu kuipiga tena kwa mara nyingine haikupatikana.”

Anna alipoulizwa na ndugu hao kama alilipa kiasi kile cha fedha, alijibu kuwa, kwa kuwa si mara ya kwanza kuomba kurushiwa pesa na dada wa Tigo – Pesa, alikubali na kulipa.

Uchunguzi zaidi wa JAMHURI, simu ya Naomi, 0655527203, ilitumika kumpigia Meshack na kumtumia ‘meseji’ saa 07:37 mchana kwenye namba 0677009128. Meshack alipohojiwa na vyombo vya dola amekiri kumiliki namba hii, ila akasema alikuwa hajaisajili na akasema Naomi haijui hiyo namba. Kwa kauli hiyo ndugu wa Naomi wanajiuliza: “Aliijuaje namba ambayo ilikuwa haijasajiliwa mpaka akaipigia, hatujui?”

Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa kimtandao umebaini kuwa fedha hiyo Sh 75,000 bado haikutolewa katika namba husika, na hapo kunazua maswali mengi zaidi, kwa mfano: “Kwa nini (pesa hiyo) haijatolewa kama mtumiaji wa hiyo simu muda wa mchana alikuwa ni Naomi? Hatujui,” anasema mwanandugu.

Ndugu hao wanasema Meshack alipoulizwa kuhusu ‘line’ yenye namba 0677009128 ni ya nani, aliwajibu kuwa “ni ya kwake isipokuwa hakuisajili na alikuwa akiitumia kuwapigia watu ambao hataki waijue namba yake halisi.” JAMHURI, kwa njia zake za kiuchunguzi, limejiridhisha kuwa ni kweli namba hiyo haikuwa imesajiliwa.

Salma anasema: “Alipoulizwa hii ‘line’ iko wapi? Alijibu; Ameiharibu. Kwa nini? Eti baada ya haya matatizo kutokea alihisi itamletea matatizo kutumia ‘line’ ambayo haijasajiliwa.”

  

Siku aliyotoweka Naomi

Uchunguzi wa JAMHURI kwa kushirikiana na ndugu wa Naomi unabainisha kuwa Mei 15, 2019 siku ambayo Naomi alitoweka, simu yake haikupokea simu yoyote bali  ilipiga simu moja tu saa 07:26 mchana kwenda namba ya mume wake, Meshack na ‘iliongea’ kwa sekunde 15 tu. Baada ya Naomi kutoweka simu zake 0655527203 na 0679463985 ziliendelea kutumiwa.

Simcard ya Naomi kuanzia tarehe 13/01/2019 ilianza kusoma kwenye simu yenye IMEI Na. 357544080102102/357544080102094. Line hiyo imetolewa Mei 15, 2019 muda wa saa 07:18 mchana na kuingizwa kwenye simu ndogo (kitochi) aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI 354289073319500.

Mei 15, 2019 saa 07:18 mchana siku ambayo Naomi alitoweka, simcard yake yenye namba 0655527203 ilitolewa kwenye handset yake aina ya ICE- C 3G FREETEL yenye IMEI Na. 357544080102090 na kuingizwa kwenye simu ndogo (kitochi) aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI: 354289073319510, simu ambayo askari walipokwenda kumpekua mumewe Naomi, yaani Meshack (Khamis) S. Luwongo siku ya Julai 03, 2019 walimkuta nayo.

Muda huohuo simcard iliyokuwemo kwenye simu hiyo ya kitochi kwa takriban siku 86 yenye namba 0677009128 ilihamishiwa kwenye simu nyingine aina ya ITEL IT2130 yenye IMEI 355209084172530 ikakaa siku moja tu (tarehe 15/5/2019), kabla ya kurejeshwa kwenye ITEL IT5600 yenye IMEI: 354289073319510 siku ya Ijumaa, Mei 17, 2019 ambako ilikaa kwa siku 3 hadi Mei 19, 2019 na kutolewa.

Askari walipokwenda kumpekua Meshack (Khamis) Julai 3, 2019 simu zote 2 za ITEL IT2130 yenye IMEI 355209084172530 na ITEL IT5600 yenye IMEI 354289073319510 walimkuta nazo Meshack (Khamis) mume wa Naomi aliyetoweka.

Kuhusu line ya 0677009128 iliyokuwemo alipoulizwa iko wapi? Alijibu: “Nimeiharibu.” Alipoulizwa kwa nini? Akajibu: “Kwa kuwa nimegundua itaniletea matatizo kwa vile nimekuwa nikiitumia bila kuisajili.”

Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa dakika 2 baada ya line ya Naomi yenye namba 0655527203 kuhamishiwa kwenye ITEL IT5600, iliipigia simu laini ya Meshack yenye nambari 0677009128.

Mei 16, 2019 saa 12:49 jioni siku moja baada ya Naomi kutoweka, simcard yake yenye nambari 0679463985 aliyoisajili tangu Novemba 3, 2017 iliingizwa kwenye simu (handset) inayomilikiwa na mumewe Meshack (Khamis) aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI 3542890733195009.

Mei 17, 2019 simcard hiyo ilituma meseji kwenda kwenye namba za Meshack (Khamis) ya 0685043374 (muda wa saa 12:24 asubuhi) na 0714812530 (muda wa saa 12:26 asubuhi) mtawalia. Mitambo ya mtandao inaonyesha mtumaji na mtumiwaji wa meseji hizo wote wakiwa sehemu moja (same location).

Ikumbukwe  hii ni baada ya simu aliyokuwa akiitumia Naomi kuzimwa siku ya Mei 15, 2019 saa 07:18 mchana, line ya Naomi ikatolewa na kutumika kwenye simu ya Meshack (Khamis) Said Luwongo ITEL IT5600 yenye IMEI 3542890733195009.

Muda mfupi baadaye saa 07:20 simu (handset) ya ITEL IT5600 iliyokuwa ina line ya Khamis (Meshack) Said Luwongo yenye namba 0677009128 ilitolewa na badala yake ikaingizwa line ya Naomi yenye namba 0655527203; Na line yenye namba 0677009128 ikaingizwa kwenye simu nyingine ya ITEL IT2130 yenye IMEI Na. 355209084172530.

Dakika 6 baadaye saa 07:26 line ya Naomi yenye namba 0655527203 iliipigia simu ya mume wake (Khamis (Meshack) Said Luwongo) kwenye namba yake ambayo hajaisajili ya 0677009128, ambayo Naomi alikuwa haijui.

Hata kama angeijua, Naomi angeipigia simu kutokea kwenye simu (handset) yake ya FREETEL yenye IMEI Na. 357544080102090. Hapa kuna dhana kuwa huenda aliyetumia simcard ya Naomi alishindwa kuitumia FREETEL yake kwa kuwa hakuwa na nywila (password) yake hivyo kumlazimu kuihamishia kwenye simu ya kitochi.

Ikumbukwe katika mahojiano Meshack alikiri kuwa namba 0677009128 alikuwa akiitumia kwa siri, hivyo Naomi alikuwa haijui, na akili ya kawaida inaonyesha kuwa Naomi asingeweza kuipigia muda ule wa mchana siku alipotoweka kutokea kwenye handset ya ITEL IT5600 inayomilikiwa na mumewe.

Saa 07:37 line ya Naomi yenye namba 0655527203 ilituma meseji kwenye line ya mume wake (Khamis (Meshack) Said Luwongo) kwenye namba yake ambayo hajaisajili ya 0677009128. Mtumaji na mtumiwaji wote wanaonekana walikuwa sehemu moja (same cellID/ gps).

Kati ya saa 01:29 usiku na saa 01:42 simu ya Naomi inaonekana ilituma jumla ya meseji 8 kwenye namba za mumewe Meshack – za 0685043374 na 0714812530. Pia mtumaji na mtumiwaji wote wakiwa sehemu moja.

Majira ya 02:00 usiku Anna wa duka la dawa alimpigia simu Naomi kwenye namba yake 0655527203. Iliita bila kupokewa. Haijulikani ilikuwa mikononi mwa nani.

Uchunguzi unaonyesha Khamis (Meshack) Said Luwongo alipoulizwa ana simu ngapi anazomiliki, alijibu kuwa ana simu zaidi ya tano, zikiwemo simu aina ya ITEL IT2130 na ITEL IT5600 alizokutwa nazo siku polisi walipokwenda kumfanyia ukaguzi. Simu hizo inaonekana zilitumika kuingizwa linei aliyokiri kuimiliki bila kuwa na usajili, yenye nambari 0677009128 na kuitoa kwenye mojawapo ya simu hizo Mei 19, 2019 kisha akaiharibu.

Ndugu wa Naomi wanauliza: “Naomi keshatoweka. Line za Naomi alizitoa wapi? Kwa nini mtumaji wa meseji na mtumiwaji walikuwa wote sehemu moja wakati Naomi amekwishatoweka?

Ilimchukua Khamis (Meshack) Said Luwongo siku 4 tangu tukio la kupotea Naomi lilipotokea hadi alipokwenda nyumbani kwa walezi wa Naomi kutoa taarifa. Wanasema hakuwahi kumpigia mtu yeyote simu – si kaka, dada wala mlezi wa Naomi kuulizia au kueleza kuwa haonekani.

Changamoto zilizoikabili familia

Baada ya familia kwenda Kigamboni kutafuta taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwa Naomi kutozaa matunda, walijaribu bila mafanikio kumuomba Mkuu wa Kituo cha Polisi – Kigamboni awasaidie kufungua jalada la uchunguzi, lakini polisi waliwagomea.

“Mnamo tarehe 12/06/2019 changamoto hiyo iliripotiwa kwa Mpelelezi Mkuu wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam [Camilius Wambura] ambaye alitusaidia kwa kutoa maelekezo kwa Afande RCO – Chang’ombe kufungua jalada la uchunguzi. Kesho yake zoezi la kwenda kufanya ‘search’ nyumbani kwa Khamis (Meshack) lilifanyika, lakini Naomi hakupatikana,” anasema Marijani.

Changamoto za baada ya kufungua jalada

Taarifa ya “cyber” iliyoombwa Tigo iliombwa kwa utaratibu wa kawaida wa barua, hivyo ilichukua muda mrefu tangu Juni 17, 2019 hadi Julai 1, 2019. “Ilikuwa ni matarajio yetu kuwa, kwa kuwa anayetafutwa hatujui yuko kwenye hatari ipi, tulitegemea utaratibu wa upatikanaji wa taarifa wa dharua ungetumika kama upo, lakini hili halikutokea,” anasema Marijani.

Ndugu wanasema mashahidi muhimu akiwamo kijana aliyekuwa anampeleka na kumrudisha mtoto shuleni hawajahojiwa. “Kwa kuwa hakuna shaka yoyote kuwa usiku wa siku ya Jumanne Mei 14, 2019, Anna alileta mauzo kumkabidhi Naomi alimkuta nyumbani, yumkini shida ilitokea aidha usiku wa siku ya Jumanne, au asubuhi ya Jumatano au mchana wa Jumatano.

“Huyu kijana ambaye humpeleka mtoto shuleni apatikane ili atoe maelezo asubuhi alipompeleka mtoto shuleni alikuta hali gani? Ni Naomi au ni Meshack (Khamis), alimkabidhi mtoto? Je, huyo mtoto akirejea kutoka shuleni alimkabidhi kwa baba yake au mama yake? Kama siku ya Jumatano, Alhamisi na Ijumaa mtoto aliandaliwa na baba yake, huyu Meshack (Khamis) kwa nini hakumtafuta mke wake popote wala kumuulizia mtu yeyote alipo mke wake?

“Kijana wa Meshack anayetunza ‘guest’ yake amedai kukaririwa na askari aliyemhoji akisema kwa nini ahojiwe yeye ‘wakati makosa kafanya mjomba wake’ (yaani Meshack)?

“Ni imani ya wengi kuwa, huyu kijana akihojiwa kitaalamu anayo maelezo muhimu sana ya kusaidia kupatikana Naomi kwa kuwa ni vijana wa nyumbani kwa Meshack na Naomi,” amesema Marijani huku akitaka hata mbwa wa polisi na teknolojia ya vinasaba itumike kubaini alipo ndugu yao Naomi.

Ndugu hawafichi hisia zao, wanasema: “Mtuhumiwa namba moja ni mume wa Naomi. Kutoshikiliwa kolokoloni kupisha uchunguzi kunatia shaka nyingi. Hata baada ya ushahidi uliokusanywa polisi bado wanamwacha anaendelea kuishi mitaani?”

Mpaka Julai 11, 2019, JAMHURI limefahamishwa na wanandugu kuwa hakuna upelelezi wowote uliofanywa kupeleleza mwenendo wa mawasiliano ya mume wa Naomi kabla na baada ya tukio.

Pia wanaongeza: “Kutohojiwa kwa kijana aliyekuwa akiishi nyumbani kwa Meshack na Naomi anayedaiwa kumsafirisha na kumrudisha kwao Bukoba mara tu baada ya tukio ni upungufu mkubwa.”

Ndugu wanasema kijana aliyetambulika kwa jina moja la Baraka inadaiwa alikuwepo siku ya tukio, ambapo Meshack amemrudisha nyumbani kwao Bukoba. “Kijana huyu tunaamini anao ushahidi muhimu uliosababisha Meshack kuingiwa hofu na kumrejesha nyumbani kwao Bukoba baada ya tukio la kupotea kwa Naomi. “Pia Meshack ameshanukuliwa mara kwa mara akisema kijana huyo alimuona Naomi siku ya tukio na baada ya tukio bila ufafanuzi zaidi ya hapo,” anasema Marijani.

Ndugu wanataka polisi wawahoji majirani wote wanaoishi kuzunguka nyumba ya Meshack na Naomi. Inadaiwa kuwa baadhi ya majirani wanashuhudia kuwa siku ya tarehe 14.05.2019 walisikia ugomvi nyumbani kwa Meshack. Hata hivyo, siku polisi walipokwenda kuhoji ulikuwa ni muda wa kazi, hivyo hawakuweza kuwapata majirani wote kutoa ushahidi.

Mafundi waliofanya ukarabati wa mabwawa ya samaki muda mfupi baada ya tukio katika familia ya Meshack nao hawajahojiwa. Hata hivyo, taarifa zilizopo Juni 13, 2019 Polisi walipokwenda kukagua nyumbani kwa Meshack walikuta kifusi kimesambazwa uani.

Alipoulizwa kwa nini kuna kifusi kilichosambazwa, taarifa zinaonyesha alijibu kuwa alisambaza kifusi hicho kwa lengo la baadaye kutaka kupiga sakafu. Fundi aliyepewa kazi ya kukarabati mabwawa ndugu walipompigia simu kueleza aina ya ukarabati alioufanya alijibu kuwa; kilinunuliwa kifusi na Meshack siku chache kabla ya Juni 13, 2019 ambacho kilitumika kupunguza kina cha mabwawa hayo ya samaki ambapo maji yote yalitolewa na baadaye kifusi kuingizwa na kisha kuchapiwa na kusakafiwa kabla ya kuyarudishia maji.

Pia yupo kijana (jina linahifadhiwa) ambaye katika simu na meseji za Naomi kupitia namba 0655527203 amewasiliana naye mara nyingi zaidi ikiwemo meseji ya mwisho siku alipotoweka, ambaye naye ndugu wanataka ahojiwe.

Kukutwa nyumbani kwa Meshack vitu muhimu vya Naomi kama kadi ya benki, kitambulisho cha kura, kadi ya bima ya afya, nguo, mabegi n.k kunatia shaka iwapo kweli Naomi amesafiri nje ya nchi.

Katika kikao cha Wazee wa Ukoo wa Naomi tarehe 16/06/2019 na 07/07/2019, wamesema: “Tukio la kupotea kwa mtoto wetu Naomi kwenye ukoo ni tukio la kwanza kutokea. Ni tukio kubwa na zito. Ni maono yetu kuwa kasi na mbinu za kumtafuta zingeendana na uzito wa jambo lenyewe tofauti na sasa kwamba ni muda mrefu umepita na hakuna aliyekamatwa.

“Mtuhumiwa anatumia “delaying technique” kufifisha upelelezi hivyo tunatoa rai kuliomba Jeshi la Polisi kwa weledi na mbinu anuai lilizonazo kuharakisha uchunguzi wa jambo hili ili ukweli ubainike.

“Mtuhumiwa anatumia nguvu zote kuhakikisha kama amemuua Naomi mwili haupatikani hivyo kitendo cha kuendelea kuachiwa huru kinahatarisha watuhumiwa kuharibu ushahidi.

“Ni ombi la Wazee wa Ukoo kuwa ni vema mhusika ashikiliwe na dola ili kupisha uchunguzi huru wa vyombo vyote vinavyohusika kwani uwepo wake huru unampa wasaha wa kuendelea kupangua mikakati ya ukusanyaji wa ushahidi wowote ule ikiwa yeye ni mshukiwa namba moja.

“Aidha, tunaomba vyombo vyote vya dola vinavyohusika kuwezesha kufanikisha upatikanaji wa taarifa, uchunguzi na utoaji wa msaada wa kisheria juu ya hili watoe ushirikiano wa kulifanikisha kwa usahihi pasipo kupindisha sheria, kanuni na taratibu za wajibu mkubwa waliokasimiwa dhidi ya uhai wa Naomi Marijani.

“Kwa kuwa asilimia kubwa ya ushahidi uliopatikana na unaoendelea kupatikana upo kwenye mitandao, ni ombi letu kuwa shauri hili lihamishiwe Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (Central Police Station) ambako ni imani yetu kuwa kuna utaalamu na mbinu zaidi kwenye eneo hilo.

“Ni vema mhusika ashikiliwe na dola ili kupisha uchunguzi huru wa vyombo vyote vinavyohusika kwani uwepo wake huru unampa wasaa wa kuendelea kupangua mikakati ya ukusanyaji wa ushahidi akiwa yeye ni mshukiwa namba moja.

“Aidha, tunaomba vyombo vyote vya dola vinavyohusika kuwezesha kufanikisha upatikanaji wa taarifa, uchunguzi na utoaji wa msaada wa kisheria juu ya hili, watoe ushirikiano wa kulifanikisha kwa usahihi pasipo kupindisha sheria, kanuni na taratibu za wajibu mkubwa waliokasimiwa dhidi ya uhai wa Naomi,” inaeleza taarifa ya wazee hao wa ukoo.

Mkuu wa Upelelezi Kanda

Mkuu wa Upelelelezi Kanda Maalumu ya  Dar es Salaam, Camilius Wambura, ameliambia JAMHURI kuwa tukio hilo ni la kweli na lipo, na akaongeza: “Mimi ninavyofahamu suala hili linafanyiwa uchuguzi kituo polisi, I mean (namaanisha) kwa ofisi ya RCO wa Temeke. Naaa, kuna uchunguzi unaendelea pale, ambao ukibaini ni nini kilifanyika, basi ndiyo tunaweza kuchukua hatua ya kuona kama kulikuwa kuna mauaji au kulikuwa kuna kitu kingine.

“Lakini kwanza tunaanza kuchunguza huyu mwanamke yuko wapi, amepotelea wapi na nini kimefanyika. Labda tu ambacho wewe unaniambia, unifanye sasa niendelee kusimamia na kufuatilia kwa karibu zaidi, kwamba ni, je, wale wamefikia hatua gani? Lakini nini ambacho kimekwama na kukitatua ili shughuli ziende mbele.

“Lakini kimsingi ni kwamba uchunguzi unafanyika… haya mengine naomba uache yako ndani ya uchunguzi, mimi labda kwako wewe nikwambie tu uchunguzi unafanywa, lakini maneno yako yanifanye niwe na ufuatiliaji wa karibu wa hili suala.”

JAMHURI limemtafuta Kamada wa Polisi Temeke, Amon Kakwale, ambaye msaidizi wake ameomba apigiwe simu baada ya nusu saa au dakika 45, lakini baada ya muda huo simu ikawa haipatikani. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, hakupatikana ofisini mwishoni mwa wiki kulizungumzia suala hili.

Meshack na JAMHURI

Julai 13, mwaka huu, JAMHURI limewasiliana na Meshack kupata maoni yake kuhusu tukio lililomfika mkewe, Naomi Marijani, aliyesema: “Hilo tukio ni kweli limetokea. Mke wangu ametoweka. Siwezi kulizungumzia kwa undani kwa kuwa bado linaendelea kuchunguzwa na kesho (Julai 14, 2019) natakiwa kufika Kituo cha Polisi Chang’ombe.” Ameahidi kutoa ufafanuzi zaidi atakapokuwa tayari kufanya hivyo.

4863 Total Views 1 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!