Msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Hamis Kiyumbi ‘Amogolas’ ambaye kwa sasa ameachana na bendi yake ya zamani ya African Stars Twanga Pepeta, amesema anafurahia maisha ya kuanza kufanya muziki wa kujitegemea.

Hivi karibuni mwanamuziki huyo alitangaza kuachana na bendi ya Twanga Pepeta ambayo imeitumikia kwa takriban miaka 13.

 

Alisema kuwa kwa sasa anataka kufanya muziki wa kujitegemea na kwamba anafurahia uamuzi wake ambao ana imani kuwa utampa mafanikio ikiwa ni pamoja na kuendelea kujipatia mashabiki wengi.

 

Amesema kwamba kwa muda aliokaa na bendi ya Twanga Pepeta ameweza kupata uzoefu wa kutosha wa kumwezesha kumiliki bendi kama ilivyo kwa wasanii wengine waliothubutu kufanya hivyo baada ya kuwa na Twanga Pepeta kwa muda mrefu.

 

Wasanii ambao walipata kuachana na bendi ya Twanga Pepeta ni pamoja na Alidi Chokoraa aliyeungana na Jose Mara na Kalala Junior na kuanzisha bendi ya Mapacha Watatu. Baadaye Kalala Junior aliachana na bendi hiyo na kurejea Twanga Pepeta.

 

Msanii mwingine ambaye amekuwa na mafanikio baada ya kuachana na bendi ya Twanga Pepeta na kuanzisha bendi yake ni Ally Choki ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo.

By Jamhuri