Hali inaonesha kuwa timu za Arsenal na Manchester City huenda zikapata wakati mgumu kufuzu katika michuano ya hatua ya makundi ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) kutokana na muundo wa makundi yanayozijumuisha timu hizo.

Katika mechi za makundi, vijana wa Arsene Wenger wamepangwa kundi moja na timu za Borussia Dortmund ya Ujerumani, Olympic Marseille ya Ufaransa na Napoli ya Italy.

 

Arsenal walifuzu katika hatua ya makundi baada ya kuichapa bila huruma timu ya Fenerbahce magoli 5-0 katika mechi za mchujo zilizochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

 

Manchester City nao watalazimika kupepetana na bingwa wa kombe hilo, Bayern Munich, CSKA Moscow na Viktoria Plzen.  Kwa Manchester City, huu utakuwa ni kama mtihani kwa kocha mpya, Manuel Pellegrini.

 

Timu nyingine ya Uingereza itakayokuwa na wakati mgumu katika mechi hizo za makundi ni Celtic ya Scotland kwani imepangwa kucheza na wakali wa soka Barcelona, AC Milan ya Italy na Ajax ya Uholanzi.

 

Kwa upande mwingine kocha mpya wa Manchester United, David Moyes hatakuwa na kazi kubwa kwani watapepetana na Shakhtar Donetsk, Bayer Leverkusen ya Ujerumani na Real Sociedad ya Uhispania.

 

Miongoni mwa timu za Uingereza ni Chelsea peke yake inaonekana kuwa ndiyo yenye njia nyepesi kwani katika kundi lao watamenyana na Schalke ya Ujerumani, FC Basel na Steaua Bucharest.

 

Mechi za kwanza za makundi katika michuano hiyo zitachezwa kati ya Septemba17-18, mwaka huu.

 

 

By Jamhuri