Wiki iliyopita nilizungumzia tamko la serikali ya Marekani kupitia Shirika lake Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), la kukata msaada wa dola milioni 472.8 za Marekani sawa na shilingi trilioni moja kwa Serikali ya Tanzania katika miradi ya mfuko huo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Maelezo na sababu zilizotolewa na mfuko huo ni kuwa Tanzania imeshindwa kutoa hoja za kufutwa Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka jana,  na pili, kushindwa kutoa uthibitisho  wa Sheria ya Makosa ya Mtandao kama walivyotaka Marekani. Leo, nazungumzia sehemu ya pili na ya mwisho katika makala yangu.

Taifa la Marekani lina tabia ya kutoa misaada au mikopo yenye masharti kwa nchi changa na masikini; zikiwamo za Afrika. Nchi yoyote masikini isipozingatia masharti hayo yenye manufaa mazuri na makubwa kwa Marekani, hupata manyanyaso na udhalilishaji katika utekelezaji wa miradi yake chini ya rungu la ‘demokrasia haikufuatwa’ ilhali Marekani ndiyo mvunjaji mkubwa wa demokrasia na haki za binadamu duniani.

Nchi masikini (ikiwamo Tanzania) zisipoukuna vema ‘upele wa demokrasia ya ubeberu’ wenye vimelea vya uonevu, unyonyaji, dhuluma na unafiki huwa mashakani. Tanzania imenyimwa fedha kwa sababu imekataa kuukuna upele huo kama alivyotaka mkunwaji.

Siamini kama kweli Marekani inaipenda, inaihusudu na ina mahaba makubwa na watu wa Zanzibar chini ya misingi ya demokrasia ya kweli. Kwa sababu Marekani haina mahaba ya dhati wala mahaba ya kudumu kwa nchi changa na masikini kama ilivyo Zanzibar. Hapa pana kitu. Ni kweli  Zanzibar ina kitu na kitu hiki ndicho akitakacho mbabe huyu Marekani.

Uhusiano mzuri kati ya Zanzibar na China ni jambo linalopasua kichwa Marekani. Mafuta asilia yaliyomo nchini Zanzibar yanamtia kiwewe. Anajikomba huenda akapewa pande la ardhi atimize azma yake ya miaka mingi ya kutaka kuweka kituo cha kijeshi na kughilibu viongozi wa siasa. Hayo ni baadhi ya mambo yanayomtia jakamoyo huenda akayakosa.

Lakini, kuomba ni kuomba. Isipokuwa kuna mbinu za kuomba. Iwe kwa kupiga magoti na kusema, kwa kusikitika na kulialia, kwa kutangaza hadharani au kwa kutembeza bakuli bila kusahau kujifanya mnyenyekevu, mwenye huruma na kadhalika – kote huko ni kuomba tu.

Si mdogo au masikini tu ndiye anayeomba msaada au mkopo. Hata mkubwa na tajiri huomba pia kwa mkubwa au tajiri mwenzake. Tena mkubwa anapokwenda kombo humwomba hata mdogo. Leo Marekani anaomba, uchumi wake si mzuri. Ameshakwenda Cuba, India, China, Urusi na kwingineko. Kote huko anaomba kwa mitindo tofauti. Huenda ndiyo anaiomba Zanzibar kwa mtindo huu.

Hivi, kipi kiliwasukuma Marekani na wenzake kuweza kupeleka  waangalizi  wakati wa kampeni na baadaye kushindwa kupeleka tena waangalizi wakati wa kupiga na kuhesabu kura katika Uchaguzi Mkuu kisiwani Pemba mwaka jana? Yapo mengi ya kuhoji.

Ikumbukwe mwaka jana wakubwa hao kabla ya Uchaguzi Mkuu walitishia kuinyima misaada Tanzania ilipokataa kuunga mkono ndoa ya jinsia moja; ushoga na usagaji. Wakubwa hawa wana dhamira ya muda mrefu kuendeleza ubabe na uporaji wa mali za nchi yetu kwa kisingizio cha demokrasia.

Tanzania ni nchi tajiri, umasikini kwa ukweli tuliukaribisha wenyewe pale tulipowaweka na kushindwa kuwakemea baadhi ya viongozi ambao walithamini nafsi zao na kupuuza nafsi za wananchi. Ndiyo maana hadi sasa viongozi hao tuliowatoa madarakani eti wanasema utawala huu mpya hautafika popote. Si bure wana vijiba vya roho.

Iwe tulipenda au tulilazimishwa kuwa masikini, ukweli Watanzania tulikubali kuwamo katika madhila hayo. Kwa sababu tulikataa kufuata masharti ya kujitawala na kujitegemea ambayo ni maarifa na juhudi kuwa ni shina la maendeleo yetu. Tulidhani misaada na mikopo ya chapuchapu ni njia ya kujikomboa kutoka ndani ya lindi la umasikini.

Hata hivyo, nafurahi kuona Watanzania wengi wapo makini na hawataharuki na tamko hilo la Marekani. Serikali ndiyo haina joto. Kwa sababu uwezo wa kupata shilingi trilioni moja na zaidi upo. Miradi yetu itakwenda kama ilivyopangwa kwani bajeti mpya ya mwaka 2016/2017 inajitegemea kwa asilimia 62 fedha kutoka ndani ya nchi yetu, asilimia iliyobaki ni tegemezi.

Mwendo wa Serikali ya Awamu ya Tano inamshangaza mbabe huyu. Hata vikaragosi wake hapa nchini wanaota ndoto za mchana watashika dola kabla 2020 kwa vipi sijui! Lakini Watanzania tusijeshangaa siku moja mbabe huyu akaanza peke peke na kurubuni viongozi uchwara. Wala si shida kwake kuwa kama mbwamwitu na mwanakondoo walipokutana mtoni kunywa maji.

Mbwamwitu alitamani kumla mwanakondoo. Akatafuta sababu ya kumpata na kumla. Akasema, “Mbona unachafua maji?” Mwanakondoo akajibu, “Nachafuaje maji wakati wewe uko juu na mimi niko chini ya mto? Wewe ndiye unayechafua maji.” Mbwamwitu akasema, “Kwanza mwaka jana ulinitukana.” Mwanakondoo akajibu, “Nilikuwa bado sijazaliwa.”

Mbwamwitu akasema, “Kama si wewe ni mjomba wako au mzazi wako.” Mwanakondoo akamjibu, “Kosa la mjomba au mzazi wangu mimi linanihusu vipi?” 

Mbwamwitu alipokosa hila, na alipokuwa akijiandaa kumvamia, yule mwanakondoo zamani alikwishakimbia. Na huko ndiko aendako Marekani na wenzake.

Marekani kufuta misaada kwa Tanzania wakati huu ni kama mtu kumpiga teke chura, ni sawa na kumwongezea mwendo au hatua. Aidha, Marekani ametuzindua kutoka kwenye usingizi mzito wa tegemezi na kuturudisha kwenye kujitegemea. 

Hiki ni kipindi cha mpito. Asante mbabe, Watanzania tumekufahamu.

1156 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!