Yah: Kuna viongozi wanayabananga kwa hofu ya ‘hapa kazi tu’

Nianze kwa kuwapongeza wale wote waliomwelewa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwamba anataka watu wasibweteke wafanye kazi, na kufanya kazi siyo lazima uonekane kwa kukemea kila kitu hata ambacho hukijui.

Hii dharura iliyojitokeza ya kukurupuka kutoka usingizini kwa baadhi ya viongozi na kuanza kufanya mambo ambayo zamani walikuwa hawafanyi, inaonesha uvivu wao waliokuwa nao na kuanza kuvamia utimilifu wa uwajibikaji wa watu wengine waliokuwa na mantiki ya kazi tangu awali.

Hii dharura imewafanya watumishi wa kada ya chini waliokuwa wakifanya kazi kwa uadilifu, kuwa katika kikaango cha kuonekana kama sasa wanafundishwa kazi  na kusababisha kutokuwa na uwezo wa kujiamini wanachokifanya, na wakati mwingine kuhojiwa na kiongozi aliyetoka usingizini na kusababisha ukiritimba  unaosababisha utendaji wa Serikali kuwa unahodhiwa na mtu mmoja.

Rais wetu alisema kila mtu afanye kazi sehemu yake ya kazi, afanye kazi kwa madaraka aliyonayo, haimaanishi kuwa kiongozi wa shirika afanye kazi zote za shirika bila kukasimu madaraka kwa watu wengine, kiongozi wa shirika hawezi kuwa mlinzi, mfagizi, dereva, katibu muhtasi, karani, ofisa wa kawaida, mkuu wa idara na kadhalika, wapo wenye nafasi hizo nao wapewe uhuru wa kufanya kile  wanachokiamini na kukijua katika nafasi zao.

Hiki kiwewe ambacho kipo kimetokana na kulala kwa viongozi wakubwa wengi na matokeo yake nchi kwenda mrama kwa usingizi wao. Kilichofanywa na Rais ni kuwaamsha viongozi na baadhi ya watumishi wengine waliolala kutokana na uvivu na kutowajibika kwa wananchi wanaopaswa kupata huduma zao.

Tumeshuhudia sasa baadhi ya viongozi wakitafuta uhalali wa kuwapo madarakani kwa kuwasulubu watumishi wa chini yao, dhana hii inakuja baada ya wao kuanza kusulubiwa na kiongozi tuliyempa dhamana ya kuwasimamia. Ni dhahiri kuwa hakuna asiyejua jinsi viongozi hawa walivyojigeuza kuwa wafalme badala ya kuwa watumishi, ugeukaji wao kuwa watumishi unawafanya wawaumize walio chini yao.

Sina hakika kama dhana ya ‘hapa kazi tu’ ya Mheshimiwa Rais inataka kubadili mfumo wa utendaji kimadaraka, kusudio lake ni kama lile la nguvu kazi wakati ule wa vijiji vya Ujamaa. Hapa kazi tu inataka kuondoa tabaka la watu tegemezi na kulifanya Taifa liwe na maendeleo. Hapa kazi tu tunataka kundi la watu wanaozurura na kufanya vijikazi ambavyo vingefanywa na watoto au wazee waache na wafanye kazi za umri wao.

Hapa kazi tu inataka kuondoa dhana ya kubabaisha katika uwajibikaji kwa ngazi zote, haijapangwa kwa ajili ya viongozi bali ni kwa wananchi wote kuanzia ofisini, mijini hadi shambani kijijini. Ili mtu uweze kuishi ni lazima ufanye kazi na kazi ni heshima ya mtwana yeyote mwenye utashi.

Kukurupuka kwa baadhi ya viongozi na kuanza kuingilia madaraka ya wengine ni kukengeuka kwa maadili, na matokeo yake watu wa chini kimadaraka watakuwa wakifanya kazi kwa woga na wasiwasi kiasi cha kufanya ufanisi kuwa mdogo katika utendaji serikalini na sehemu nyingine.

Utumishi katika Serikali yetu ulikuwa umepwaya sana kutokana na imani kwamba waliopo madarakani ndiyo waliokabidhiwa fimbo ya kuwatandika wengine na hata wananchi wenyewe kwa kuyatumia vibaya madaraka yao, wapo walioleta udini, uvivu, wizi, ubadhirifu, ukabilia, undugu na mambo mengine mengi.

Utumishi serikalini ulikuwa ni uchifu wa kurithishana, watu walisahau kwamba wao ni waajiriwa wa wananchi wenye nchi yao, waligeuza ni ofisi zao binafsi na hawakutaka kuhojiwa wanafanya nini, walifika mahali hawataki  kuondoka ofisini na hata wakiondoka waliacha utawala ndani ya himaya yao na kuendeleza yale waliokuwa wakiyafanya.

Hapa kazi tu imekuja ili kuleta tija kwa Taifa, iwapo kiongozi unazembea huna sababu ya kuwapo mahali pa kazi ukipokea mshahara kutoka kwa mwajiri. Hapa kazi tu inapunguza ukiritimba na maendeleo ya Taifa, ikumbukwe kuwa mwaka 1961 uchumi wa Tanzania na China ulikuwa ukilingana lakini kutokana na uvivu wetu leo Tanzania bado ni masikini.

Matumizi mabaya ya fedha kwa ofisi ndiyo yaliyotufikisha hapa, matumizi mabaya ya madaraka yamelifilisi Taifa, matumizi mabaya ya muda yanatufanya tuendelee kuwa maskini kila siku. Dhana ya Mheshimiwa Rais isibebwe kwa maana nyingine,  kinachotakiwa ni kufanya kazi.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.