1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliNimekuwa nikisikia, nimesoma katika magazeti na hatimaye ninajiuliza hivi ni kweli viongozi hawa wanalingana?

Ulinganisho mara nyingi unakuwa kwa vitu vya aina moja. Katika ulinganisho kuna vigezo vinavyokubalika. Inapokuja kulinganisha utawala wa viongozi mbalimbali hapo kunatakiwa uangalifu wa hali ya juu sana. Kwanza kila mtu yu wa kipekee kadiri alivyoumbwa na Mungu (unique). Pili kila mtu ana vionjo vyake na hivyo anatenda tofauti na kiongozi mwingine. Hapo ulinganisho huwa mgumu.

 Lakini kimapokeo hapa duniani watu wanawalinganisha viongozi wao kutokana na namna walivyoyakabili matatizo katika nchi. Kama mwelekeo umekuwa kuwasaidia walala hoi hapo jamii kubwa ikanufaika, wananchi wanaweza kusema utawala huu au ule umekuwa mzuri. La hasha kama kumekuwa na mwelekeo wa unyonyaji na ukandamizaji hapo wananchi watasema utawala mbaya.

Tumesoma juu ya VIATU vya Nyerere kumtosha Magufuli, tumesoma, maraisi wachekechwa, tumesoma Demokrasia inavyopindishwa, tumesoma viongozi ng’ang’anizi wa madaraka na kadhalika.

Sasa basi tunajiuliza kwani kuna fomula ya utawala wa kidemokrasia hapa duniani? Mimi najua ziko fomula katika kukokotoa hesabu au katika fizikia au katika kemia. Pale ukipewa fomula yaπr2 (pai ara skweadi) unaweza kutumia fomula ile kutafuta eneo lolote la mzunguko wowote. Ukiona H2O mara moja unajua maana yake nini na ukatolea ufafanuzi wa kisayansi. Lakini hili la kwenye siasa mimi sijaona wala kusikia fomula ya kitu “Demokrasia”. Nchi za ulimwengu wa kwanza neno hili linaeleweka namna yake.

Hapa Afrika nchi za ulimwengu wa tatu kwa mtazamo wangu, mimi neno hili linaeleweka kivyake. Basi kwa hali hiyo kila nchi huru, inaweza kusemekana kuna Demoksaria ya nchi ile na kamwe isilinganishwe na demokrasia ya nchi nyingine, kwa kuwa mazingira ya nchi ni tofauti kabisa. Kwa hali hiyo basi siyo sahihi nchi moja kuhoji demokrasia ya nchi huru nyingine. Hakuna fomula ya Demokrasia moja duniani hapa.

Mimi binafsi ninawahusudu sana marais John F Kennedy wa Marekani (USA), Mzee Baba wa Taifa Mwl. JK Nyerere. Mzee Madiba – Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini na sasa huyu Rais wa awamu ya tano katika nchi yetu Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Huko nyuma nilibahatika kumuona (katika Luninga) na kumsikia huyo Rais John Kennedy, hapa nchini nimefanya kazi chini ya Mwalimu Nyerere na hivi sasa niko chini ya utawala wa Rais Magufuli. Hii naita ni bahati ya pekee kuona tawala za wana siasa shupavu hawa.

Kuhusu Rais John F Kennedy ningesema tu alinivutia kwa matamshi yake toka siku alipoapishwa kule Marekani tarehe 20 Januari 1961. Nilikuwa masomoni Hull University kule Uingereza katika ukumbi wa Chuo Kikuu. Ile ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona Luninga. Tulikuwa wanafunzi kibao mbele ya Luninga ile tukisikiliza hotuba yake ya kwanza.

 Miongoni mwa waliokuwepo pale White House Marekani siku ile ni Marais wastaafu Bwana (Generali mstaafu) Dwight David Eisenhower (1953 – 1961) na pia alikuwepo Bwana Harry S. Truman (1945 – 1953) na wageni kibao kule Marekani. Mie nayakumbuka matamshi fulani fulani aliyatoa siku ile mpaka leo hii naona hata viongozi wangu kama Mwalimu Nyerere au huyu wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli wanayatamka. Mathalani Rais John Kennedy alisema namkunuu “….yote haya, hayatamalizika kwa siku 100 wala hayatamalizika kwa siku 1000 wala katika maisha ya Serikali hii, na pengine hayatamalizika katika uhai wetu. Lakini na tuanze…” (J.F Kennedy, inaugural speech, White House, USA tarehe 20/01/1961 tazama uk. 11 – 12 kitabu cha Noor Jehan H Zaidi).

 Hayati-Baba-wa-Taifa-Julias-K.-NyerereHapo Rais aliwaambia wananchi wake kuwa yeye hatamaliza matatizo ya kiutawala kule Marekani kwa kipindi chake kile tangu cha siku 100 au miaka 4 ya utawala wake. Kumbe kuna ugumu  kutawala.

 Hatimaye Rais Kennedy aliwaomba wananchi wenzake wafanye juhudi kuondoa ulimwenguni maadui kama udhalimu, umaskini, ugonjwa na vita. Mwishoni akihitimisha hotuba yale ile akayatamka maneno yale muhimu kuwa “….msiniulize ni mambo gani nchi yenu inaweza kuwafanyia. Jiulizeni ni mambo gani nyinyi mnaweza kuifanyia nchi yenu”. Usemi huu hata maraisi wa nchi yetu wamewahi kutueleza.

Huku kwetu, wakati Baba wa Taifa anaanza kutawala kama Rais wa Tanganyika aliongea hivi siku ya tarehe 10 Desemba 1962. Hapo aliwahi kutamka haya “anybody with intelligence will know that we are far from joking…. one would find no parallel to the slaughter of our people which has stemmed from poverty, ignorance and disease. I have mentioned these problems so as to give you some idea at least of how different is this Tanganyika which we have inherited from the new Tanganyika we are determined to build. Our second duty is to understand the problems facing us and to realize that there is no short cut to their solution….our third duty is to avoid the temptation of blaming others for our difficulties. There is no one among our fellow Tanganyikans on whom we could seize and say that it was he who intended all these problems for us. Our final duty, therefore is for all of us to pool our resources and work together in trust and friendship in order to build a Tanganyikans in which there are no longer any such problems as those I have been taking about. …….. My friends, let every one of us put all he has into the work of building a Tanganyika in which there will be no more such distinctions and divisions (Nyerere: Uhuru na Umoja sura ya 40 uk. 181).

Inaonekana upo ulingano wa kutosha katika mitazamo ya viongozi hawa wawili kule Marekani Rais kijana Kennedy alitaja matatizo ya nchini mwake kamwe hayamalizwi katika kipindi cha siku mia moja wala siku elfu moja wala mhula mmoja wa utawala. Hapo akawaomba wananchi wenzake waungane naye kila mmoja kwa jitihada na mchango wake walijenge Taifa lao lile la Marekani. 

Mwalimu naye huku kwetu wakati akitoa hotuba yake ya kwanza kama Rais alisema wazi wazi hali ya nchi aliyorithi kuitawala. Kwamba ilikuwa duni sana, imejawa na ufukara, wananchi wake wajinga na kuna magonjwa tele. Ndipo alipoomba wananchi wake walitambue hilo, washikamane kwa umoja na wajenge Taifa jipya la Tanganyika wanayoitamani iwe, isiyo na matabaka miongoni mwa wananchi wake.

 Hapo ndipo tunaweza kusema tuwe na ulinganisho wa tamaa ya maendeleo kwa wananchi wote. Malengo ya viongozi hawa yalikuwa kuondoa dhuluma miongoni mwa wananchi wao kuondoa ujinga, na kuondoa magonjwa.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli hayuko mbali au hayuko tofauti na hao Marais wawili niliowataja. Rais Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kuapishwa pale Uwanja wa Uhuru siku ya Alhamisi Novemba 5, 2015 basi jioni ya siku ya Ijumaa Novemba 20, 2015 alitoa hotuba yake ya kwanza wakati akilizindua bunge jipya kule Dodoma. Rais Magufuli katika uzinduzi wake wa bunge hili jipya na la wasomi alitoa DIRA ya namna Serikali yake itakavyoendesha nchi yetu

Kwa kifupi sana alisema, namnukuu “niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 91, ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili…. aidha niwapongeze wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili. ….Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali ya umma na rasilimali za Taifa na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki….

Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa waheshimiwa wabunge. Bunge hili linayo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka maslahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha ya vijembe, mipasho na ushabiki wa vyama Bungeni. Kwanza tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu, sisi sote ni kitu kimoja, na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu”!! (Hotuba ya Rais Bungeni tarehe 20/11/2015).

 Lugha hii ya kiongozi wetu haikutofauti na lugha ile ya Baba wa Taifa pale alipowahutubia wabunge Mei 12, 1964 hapa Karimjee. Baba wa Taifa alitamka hivi. “Na ipo kazi kwa kila mmoja wetu, …. mwanasiasa, mtumishi wa Serikali, mfanyakazi viwandani au mashambani imebidi kufanya kazi bila kuchoka na ukumbuke kwamba matendo ya kizembe au hata maneno ya ovyo yanaweza kuharibu jitihada ya maelfu ya watu” (Nyerere: Bunge la Tarehe 12/05/1964 uk. 23).

 Kila msomaji ataona namna viongozi watatu hawa wanavyolingana kimtazamo wao kwa maendeleo ya wananchi wa mataifa yao. Hawalingani kwa sura, kimo, rangi au umri lakini kupitia karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu, wote wanalingana katika namna ya kuhudumia wananchi wenzao.Wanachukia matabaka miongoni mwa wananchi wao ndipo wanaamua kujitolea sadaka kuwahudumia kwa moyo mkunjufu.

 Kennedy sisi wazee tunakumbuka, mapema mwaka ule wa 1963 yalipotokea mafuriko kule Rufiji na Kilwa alileta msaada wa mahindi yale ya njano, kutuokoa watanzania. Kennedy alibuni mpango wa kuleta vijana kusaidia kufuta ujinga. Mpango ule uliitwa walimu wa “Peace Corps”

mpango uliowezesha shule zetu nyingi kupata walimu, wakati ule tulipokuwa na upungufu mkubwa wa walimu wa shule za Sekondari.

 Nafikiri mpaka sasa mpango ule bado unanufaisha mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki kwa kupata “volunteers” kutoka Marekani. Hapa Tanzania bado makundi ya Peace Corps hawa wanakuja kutoa huduma.

 Baba wa Taifa, alijitolea mhanga katika kudai Uhuru wa Taifa hili. Sote tunajua sadaka kubwa aliyotoa ni pale alipojiuzulu kazi ya ualimu (Jumapili tarehe 23/03/1955) na kutoka Pugu kuja kukaa Magomeni.

 Ikumbukwe alishakuwa mtu wa familia alikuwa na mke na watoto. Wote walihitaji kula na kuvaa. Yeye akasema potelea mbali.“Naingia siasa niokoe watu wanchi hii mikononi mwa wakoloni Waingereza”. Hapo inafaa sana wananchi kutafakari moyo ule wa sadaka na uzalendo mkubwa aliokuwa nao Mwalimu kwa nchi hii.

 Huyu Dkt. Magufuli, si tunamjua? Yeye alipokuwa akifanya kampeni alisisitiza anataka kuwasaidia wanyonge wa hali ya chini angalau nao wainuke kidogo. Katika hotuba yake wakati anafungua rasmi Bunge pale Dodoma tarehe 20/11/2015 alilenga kupiga vita rushwa, ufisadi, dawa za kulevya na kadhalika.

Wakati anaongea na wazee wa Dar pale Diamond tarehe 13 Februari 2016 alisema “tuliahidi kufanya kazi ili kuwa na Tanzania mpya. Changamoto tunazozipata zingine zinawagusa baadhi ya watu, lakini watakaoguswa ni wachache sana kwa faida ya Watanzania walio wengi hasa masikini. Tanzania hii haitakiwi kuwa na wanafunzi wanakaa chini, wala haitakiwi kuwa na watu wanakosa maji, au haitakiwi unapoenda Muhimbili au kwenye hospitali zetu unakuta watu wamelala kwenye kitanda watu watano na wengine chini. Tanzania hii ni yenye neema. Haiwezekani Watanzania kila mahali unapokwenda unawakuta wanalia, wakati Tanzania ina rasilimali za kila aina….

 Ndiyo maana nawaambia wazee wangu hawa wa Dar es Salaam, mimi na Serikali yangu tunajitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania.“Tunaomba muendelee kutuombea kwa Mwenyezi Mungu ili haya matamanio yetu tunayotaka kuyafanya kwa ajili ya nchi ya Tanzania tuyatimize kwa haraka na kwa speed kubwa sana”. (Hotuba ya Rais Diamond Jubilei tarehe 13 Februari, 2016).

 Mpaka hapo naona ulinganisho wangu kimatendo unaelekea kukubaliana na maoni ya wenzangu waliouliza swali “Viatu vya Nyerere kumtosha Magufuli?” Mzee John Samuel Malechela amesema kuwa mtindo wa uongozi wa Rais Magufuli haujapata kutokea tangu Mwalimu Nyerere alipong’atuka Urais mwaka 1985. Uongozi wa Rais Magufuli umelenga kumjengea nguvu mwananchi wa kawaida kama ambavyo Mwalimu Nyerere alifanya katika zama zake za utawala. (Jambo Leo No. 2363 la tarehe 26/02/2016 uk 4).

Profesa Isaa Shivji amekuwa muwazi kwa kusema ulinganifu mzuri usiangaliwe kwenye matukio, bali uzingatie zaidi kwenye misingi. Kwa kuangalia nukuu zao zenye hisia kutokana na kero zilizopo nchini Mwalimu Nyerere na lile Azimio lake la Arusha wakati Dk. Magufuli na ile hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Novemba 20, 2015. Basi tathmini sahihi katika kuweka sawa ulinganifu kuna vigezo 10 au mambo 10 yaliyoanzishwa na kutekelezwa kwa kiwango cha juu wakati wa awamu ile ya kwanza. Hivyo Dk. Magufuli akiyafuata yote hayo inawezekana akastahili heshima ya kutosha.

 Kwa jinsi Rais Magufuli anavyochanja mbuga katika kutumbua majipu hapa nchini, yaelekea kutosha kabisa kuvaa viatu vile vya Baba wa Taifa. Rushwa inapigwa, ufisadi unapigwa, madawa ya kulevya yanashambuliwa, kodi inakusanywa, huduma mahospitalini inaboreshwa, elimu bure inatolewa na kero nyingi za wananchi wanyonge zinasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi, huku sherehe na posho za masafari (per diem) ya nje sasa zimepunguzwa. Kuna mpango wa kufufua viwanda vyetu na hilo litaleta tija kwa uchumi wa nchi hii. Ajira zitazalishwa na bidhaa za viwandani zitaleta fedha za kigeni. Basi kwa matarajio namna hiyo, utawala wa awamu ya tano unategemewa kuleta matunda mema hapa nchini.

 Upo utaratibu katika Serikali au katika nchi hii, kwamba mtu akiajiriwa anapata muda wa matazamio kufanya kazi huku akiangaliwa tunaita “probation period” kwa muda wa miezi 6 na baada ya hapo anathibitishwa katika kazi au anaondolewa. Kwa mtazamo huo naona hii Serikali ya Awamu ya Tano ingali katika matazamio (probation) hata hiyo miezi 6 ya kuangaliwa haijatimia.

Hebu tuipe muda basi tuone katika miaka 5 ya utawala wa Dk. John Pombe Magufuli kiuchumi na kimaendeleo itatufikisha wapi?Kama hatukuridhika na utendaji wake si ndipo tutapata nafasi nzuri ya kuikataa? Tutawapigia kura wengine watakaotutimizia maoteo (our aspirations) yetu. Hawa walioshindwa tutawatupilia mbali. Lakini, tukiona utendaji wa hii Serikali ya awamu ya Tano ni mzuri, tutawathibitisha kwa kuwapa kura zetu waendeleze kutuletea maendeleo hayo tunayotazamia.

 Majipu ndiyo kwanza yanatumbulia na kila lipasuliwapo jipu huwa pana jeraha nahata jeraha likipona basi panabaki kovu. Cha muhimu kwetu sisi sote ni uelewa kuwa matatizo yetu ni mengi, na wala hayatamalizika katika muda mfupi. Makovu ya majipu yaliyopasuliwa yataendelea kuonekana lakini hayatadhuru uchumi wa Taifa letu.

Basi kama alivyosema Rais Kennedy kule Marekani mwaka 1961 kuwa matatizo yote hayatamalizika katika muda wetu. Lakini tuanze ….. akimaanisha tuanze kuyashughulikia. Ndiyo maana Rais wetu Magufuli ameanza kuyashughulikia. Sasa Watanzania kwa nini tusimpe muda ayashughulikie? Aendelee kupasua majibu ili tupate unafuu kiuchumi na kimaendeleo.

Tusitegemee miujiza kutoka kwa Rais Magufuli, maana siku hizi hakuna miujiza kama ile aliyoifanya Bwana Yesu kwa Mayahudi kule Israeli. Pamoja na miujiza ile bado kuna watu hawakumwamini huyo Yesu. Tunasoma maneno namna hii, “…. naye alipofika nyumbani wale vipofu walimwendea Yesu akawaambia mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia “Naam Bwana”. Ndipo aliwagusa macho akasema, “kwa kadiri ya IMANI YENU mpate” macho yao yakafumbuka (MAT. 9:28 – 30). Rais Magufuli hana uwezo namna hiyo ila anatutaka tumsaidie kubadili hali ya wananchi iwe bora kuliko ilivyo leo hii.

 Siku hizi Dk. Magufuli anasema HAPA KAZI TU, sisi kwa yale mazoea yetu ya kamanyola, bila jasho lolote tuneemeke, hilo haliwezekani! Yatupasa tuisadie Serikali kuzalisha na kuwajibika ndipo nchi itasonga mbele. Kubweteka na starehe, kufanya dili au mishenitown ni kuitafuna nchi hii.

Watanzania hatuna budi kukumbuka na kujivunia historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa bara letu hili. Ukombozi na Uhuru wa nchi kadhaa umepitia Tanzania kuanzia mwaka 1963 pale OAU kule Adis Ababa walipoichagua nchi yetu kuwa kitovu cha mapambano ya ukombozi wa nchi za Afrika Kusini. Nchi hii imejijengea uhalali wa kuitwa kisiwa cha Amani.

 Wakuu wa nchi walichagua Tanzania kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya ukombozi (OAU Liberation Committee Secretariat HQs). Kuanzia hapo Makatibu Wakuu wa hiyo Sekretarieti wametoka Tanzania (Balozi Sebastian Chale, Balozi George Magombe na Brigadia Jenerali Hashim Mbita). Watanzania hawa wamefanya kazi sana kusaidia Uhuru wa Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Afrika ya Kusini na Namibia. Hilo pekee limetujengea jina zuri.

 Si hivyo tu bali nchi hii imepokea wakimbizi wengi kutoka Rwanda, Burundi, Congo DRC, Uganda na kadhalika. Basi hapo tujue nchi yetu ni mahali pa usalama. Sasa ikijatokea sisi tukavurugana, jamani tutakimbilia wapi? Nchi gani itatupokea kama wakimbizi? Tusidanganyanyike, tuisadie Serikali kutengemaa ili uchumi wa Taifa letu ukue, ufisadi usiwepo na kila mtu ale kwa jasho lake.

 Kama kuna mtanzania mwenye ndoto ya kukorofisha hapa nchini ili tuvurugane na waathirika wakimbilie nje ya nchi huyo ni mwehu na anajidanganya. Ndiyo sababu Rais Magufuli alipoongea na wazee wa Dar es Salaam pale Diamond Jubilee alisema yeye ni Amiri Jeshi Mkuu, atasimamia usalama wa nchi hii kwa hali yoyote ile na akatuhakikishia kuwa hali ya usalama ni shwari.  Tutajachekwa na wale tuliowasaidia kupata Uhuru katika nchi zao na tutakejeliwa na wakimbizi kutoka nchi jirani wanaotuzunguka. Tuachane na siasa uchwara eti nchi hii itaweza kuwa kama Hong Kong! Tuijenge nchi yetu kufikia uchumi wa hali ya kati tutakuwa tumepiga hatua ya kuridhisha.

 Mara tu baada ya kupata Uhuru wetu, Baba wa Taifa alikuja na kauli mbiu ya Uhuru na Kazi. Utawala wa Awamu ya Tano umekuja na kauli mbiu Hapa Kazi Tu. Hivyo watanzania tunapaswa kuzifuata kauli mbiu hizo. Nchi zote zilizoendelea zimefikia hali ile kutokana na Kazi. Kila mwenye kuwa na afya timamu anachapa kazi kupata riziki yake na wakati huo huo anasaidia uchumi wa taifa lake.

 Je, viongozi wetu wanalingana katika hili? Mmoja kasema Uhuru na Kazi na mwingine anasema Hapa Kazi Tu. Hapa pana kile mimi ninakiita “Comon Factor”. Hiyo mimi naona kifananisho cha pamoja ndio  neno lile  “KAZI”. Basi kumbe kimtazamo wanalingana.

2533 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!