Asante RC Mwambungu, Inspekta Anna

Septemba 28 ni siku ya pekee maishani mwangu. Ilikuwa ni siku mbili tu tangu niliposafiri na kufika Songea mkoani Ruvuma. Nilipanga katika hoteli iliyopo katikati ya mji iitwayo Safari Lodge.

Nilisafiri kwenda Songea kwa kazi maalum ya kufundisha waandishi wa habari wa mkoani humo, kuhusu Azimio la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji (DEFIR).


Mafunzo haya yamedhaminiwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Yanaendeshwa nchi nzima na wakufunzi mbalimbali, na yanasisitiza suala la maadili, uwajibikaji wa wahariri, waandishi wa habari, wajibu wa wamiliki, dola (Serikali), watangazaji, wafadhili na wadau mbalimbali wanaohusiana na vyombo vya habari kwa njia moja au nyingine.

 

Mafunzo haya yanalenga kusimika mizizi ya maadili miongoni mwa wanahabari, kwa kiwango cha kuwafanya wachukie vitendo vya rushwa, uonevu, masilahi binafsi na kuepuka upigaji chuku (sensationalism).

 

Yanalenga pia kuijenga tasnia ya habari iwe kimbilio na sauti ya wanyonge pasipo kuonea upande wowote. Mafunzo haya yanasisitiza suala la mizania (balancing) katika mchakato mzima wa kukusanya, kuchakata na kusambaza habari.

 

Nimeifanya kazi hii karibu mikoa minane sasa. Nawashukuru waandishi wa habari wa Songea kwa jinsi tulivyoshirikiana katika mafunzo haya, kwani kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni kubadilishana uzoefu na si kufundishana kama mwanafunzi na mwalimu. Hakika kundi la wajuzi likiongozwa na Profesa Issa Shivji lililoandaa DEFIR tangu mwaka 2008 hadi 2011, lilifanya kazi ya kupigiwa mfano.


Nikiwa Songea baada ya kuwa nimefundisha Alhamisi na Ijumaa, nilijikuta katika mtanziko wa mawazo ya aina yake usiku wa Septemba 28 kuamkia 29. Niliporejea hotelini nilikokuwa nimepanga, nilimsihi mhudumu anihifadhie vifaa vyangu muhimu ikiwamo kompyuta ya mkononi (laptop). Mhudumu alinihakikishia kuwa hakuna tatizo lolote la kiusalama hotelini hapo, hivyo akanisihi niache ndani vifaa vyangu vyote.


Nilikuwa nakatiza mitaa miwili kwenda kula chakula cha jioni katika Baa ya Serengeti, hivyo ikanibidi niache fedha Sh 170,000 kwenye mfuko wa laptop, na ndani ya mfuko huo kulikuwa na kila kitu ninachokitumia kama ofisi yangu. Nilimkabidhi mhudumu funguo nikaenda kula. Niliporejea nilikuta tayari wamefunga mlango wa mbele, mlinzi akazunguka dirishani na kumwita mhudumu aliyekuja kufungua mlango na kunikabidhi ufunguo wa chumba Na 2 nilichokuwa nimepanga.


Mara tu nilipofungua mlango wa chumba, nilikuta hakuna laptop yangu na mkoba wake umebebwa. Nilimwita harakaharaka huyo mhudumu, nikamuuliza iwapo amehamisha mfuko wangu, alichosema ni: “Ahaaaa, basi ni kweli itakuwa kuna mwizi ameingia humu ndani, maana kuna mteja pale Na 4, naye amelalamika kuibiwa Sh. 220,000.”


Baada ya maneno hayo tulikusanyika wateja kadhaa, nikampigia simu Mwenyekiti wa Ruvuma Press Club, Andrew Kuchonjoma, ambaye bila ajizi majira ya saa 7 hivi usiku, aliamka na kuja pale hotelini. Tuliambatana kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Songea, tukafungua jalada. Hadi tunakamilisha kufungua jalada, ilikuwa imefikia saa 11 alfajiri.


Kwa muda wote hapo kituoni, nilipata msaada wa karibu wa Inspekta Anna Tembo, Inspekta Yesaya Edward Sudi na askari mmoja aitwaye Gabriel. Hakika mnyonge mnyongeni lakiniu haki yake mpeni. Inspekta Anna alifanya kazi ya kupigiwa mfano. Najua hakuna neno zuri zaidi ya asante, lakini afande huyu alinipa ushirikiano wa hali ya juu.


Bila kujali ni muda gani, alikuwa akinipigia simu hadi usiku wa manane kuuliza au kunijuza hatua ya uchunguzi iliyofikiwa. Hakulala tangu siku ya Ijumaa usiku wa kuamkia Jumamosi hadi Jumapili alipofanikiwa kukamata wahalifu wawili, waliokuwa wamepora laptop yangu na vitu kadhaa nilivyovitaja.


Kila nilipofika kituo cha polisi hakika niliburudika. Pamoja na uchungu wa kuibwa mali zangu, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nikipokewa bila kudaiwa rushwa au kuwekewa mazingira ya kuona kuwa pengine wakubwa hawa wanataka rushwa, hakika nilifarijika na natumia fursa hii kurejea tena kusema asanteni uongozi wa Kituo Kikuu cha Polisi Songea.


Inspekta Yesaya, kwa kushirikiana na Inspekta Anna, walihakikisha baada ya majambazi yale mawili kukamatwa kesi inapelekwa mahakamani Jumatatu. Nikatoa ushahidi na kwa ushirikiano ule ule, Hakimu Mkazi Mkuu akaamuru nirejeshewe vifaa vyangu vya kazi kama polisi walivyoomba nikabidhiwe, kwani ndiyo vitendea kazi vya msingi katika ofisi yangu.

 

Hakika utaratibu nilioushuhudia Songea katika utoaji haki, niliburudika. Nchi hii kama polisi wote wangefanya kazi kwa utaratibu huu kesi zisingerundikana, haki ingepatikana kwa wakati na waharifu wangepata hofu ya kutenda maovu kwani wangejua mkono wa dola hauko mbali na utawafikia wakati wowote.


Sitanii, mwingine katika orodha ya shukrani ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. Mkuu huyu wa Mkoa alipopata taarifa kuwa nimeibiwa aliniita nyumbani kwake akanifariji. Alishirikiana na uongozi wa Polisi Mkoa kuhakikisha unafanyika msako wa kila aina ili nipate vifaa vyangu vilivyoibwa.


Nikiwa nimeambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma, Kuchonjoma, Katibu wake, Andrew Chatwanga na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Joyce Joliga, Mkuu wa Mkoa Mwambungu alisema umefika wakati atahakikisha mkoani kwake usalama unaimarika. Alisema sasa ataitisha mkutano na wamiliki wote wa hoteli mkoani humo ili kuzungumza nao jinsi ya kuimarisha usalama katika nyumba za wageni.

 

Hakika nilifurahishwa si tu na uchangamfu wa Mkuu wa Mkoa Mwambungu, lakini pia moyo wa kuguswa aliouonesha na kunitia moyo kuwa mali zangu zingepatikana tu. Sehemu kubwa ya mali imepatikana, ukiacha fedha na vitu vichache vilivyokuwa kwenye mfuko uliobeba laptop yangu.


Sitanii, si nia yangu kujaza sifa tu, lakini ikilazimika nitafanya hivyo. Atanishangaa sana Nathan Mtega kama sitamtaja katika safu hii. Mwandishi huyu wa Radio One Stereo alifanya kazi kubwa ajabu. Aliweka mitego kila kona kuhakikisha kama kuna mtu anauza mali yoyote kati ya nilizoibwa ananaswa.

 

Ilifika mahala akaleta mtu laptop akitangaza anauza, kumbe ulikuwa mtego ulioandaliwa na Mtega. Ni bahati mbaya haikuwa ya kwangu, tukaiacha.


Siwezi kutaja majina ya wanahabari wote wa Ruvuma mmoja mmoja, ila itoshe tu kuwashukuruni kwa kuwaambia asanteni sana kwa ushirikiano wenu katika sakata hili. Sifa pia zimwendee rafiki yangu Abdallah Rutala kwa kuwa nami muda wote wa mahangaiko.


Hata hivyo, katika harakati hizi nilikumbana na kikwazo. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Kaizilege, pamoja na kuelekezwa na Mkuu wa Mkoa Mwambungu atupe ushirikiano, huyu alinikwaza. Safu hii si ndefu sana, ila naamini huyu kamanda anahitaji kufundwa kidogo. Anapaswa kufahamu kuwa yeye si wa kwanza kushika wadhifa huu hapa nchini na wala hatakuwa wa mwisho katika cheo hiki.

 

Sitanii, nikiwa nimeambatana na viongozi wa Ruvuma Press Club, alipoambiwa kuwa tupo mlangoni ofisini kwake akasema kwa sauti nasi tukamsikia: “Wakiwa na shida wanatujia, bila hivyo wanatususa.” Maneno haya yalinikumbusha msimamo wa waandishi wa habari kusitisha ushirikiano na polisi wa kihabari kwa siku 40, baada ya mauaji ya mwandishi wa habari Kituo cha TV cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyeuliwa kikatili huko Nyololo, Iringa.


Kaizilege hakuishia hapo. Alianza kunitolea maneno ya kejeli akisema ‘Unasemaje Nshomile’. Moyoni nilikereka. Nilipomdadisi, nikakuta yeye ndiye anayetokea Tarafa ya Kiziba, Bukoba Vijijini, sehemu ambayo watu wake walisababisha Wahaya wote wachukuliwe kuwa wana nyodo kila kona ya nchi hii, kwa kujidai wamekwenda shule sana kuliko yeyote awaye katika nchi hii.


Baadaye nilibaini kuwa ni kijana wa rika langu, maana aliniambia alihitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Nyakato jirani na kijijini kwetu Nyanga, mwaka 1982. Miaka hiyo nilikuwa nacheza mpira kwenye viwanja vyote viwili vya Shule ya Msingi na Sekondari Nyakato. Na pengine kama ana kumbukumbu, enzi hizo kidato cha kwanza walikuwa wakionewa kwa kutumia maneno matatu: “Lini, wapi na kwa nini”. Waliwaita Form One – Wagogo.


Mbwembwe za Kaizilege zilinikera zaidi wakati anapanda gari kuondoka ofisini kwake. Kamanda wa Polisi wa Mkoa tu, eti anapopanda gari msaidizi wake anamfunga mkanda kama Rais wa Jamhuri ya Muungano au Waziri Mkuu afungwavyo mkanda na walinzi wake. Nikasema huu ni usultani uliokithiri. Nyodo alizonazo Kaizilege amenikumbusha Waziba halisi na tabia zao. Ninachoweza kusema ajirekebishe vinginevyo kazi hii itamshinda.


Kamanda wa Polisi anapaswa kuwa rafiki wa jamii na askari anaofanya nao kazi, lakini kutembea amepandisha mabega utafikiri ana majipu kwenye kwapa, haitamsaidia kupata kwa urahisi taarifa za kiintelijensia. Watu watamkimbia na usalama utazidi kuwa hatarini katika mkoba wake.


Nimefanya kazi na makamanda wengi nchini ila Kaizilege anahitaji kubadilika. Sina cha kubembeleza kwake naye analijua hilo. Ni heri mjakazi amwambiaye mfalme yuko uchi, kuliko kumsifia huku wapita njia wakimcheka.


Ukiacha kero ya Kamanda Kaizilege, nasisitiza Mwambungu, Inspekta Anna, Inspekta Yesaya na Gabriel kuwa wamefanya kazi nzuri. Hawa wakiendelea na moyo huu, hakika usalama Ruvuma utaimarika kwa kiwango kikubwa. Mungu awabariki sana.