Wahenga walisema: “Tenda wema nenda zako.” Wahaya na Wanyambo wanasema: “Ekigambo kilungi kigambwa.” Nao Wahehe wanasema: “Uwema kigendelo” au “Utende wema ubitage”; na kadhalika. Sasa ni miezi minne tangu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani), alipofanya ziara ya kihistoria katika wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera. Lakini kazi na shughuli alizozifanya huko kwa siku mbili hazikumletea sifa nzuri yeye peke yake, bali zilimwongezea sifa na umaarufu Rais John Magufuli na serikali yake kwa ujasiri wa Chama Cha Mapinduzi kupigania haki na mali za watu wa hali ya chini. Kwa siku mbili alikutana na kusikiliza kero, migogoro na matatizo ya majanga yanayotokana na uonevu dhidi ya mama wajane na wazee kunyanyaswa na kudhulumiwa mali, mashamba na ardhi zao kwa mabavu. Waziri huyo amesifika sana kwa kufanya mikutano ya hadhara katika Kata ya
Kihanga, wilayani Karagwe na Kaisho wilayani Kyerwa, ambako alifanya mikutano ya hadhara na kuhudumia wananchi zaidi ya 300 kila siku tangu asubuhi hadi jioni bila kupumzika au kupata chakula cha mchana. Kutokana na wilaya za Karagwe na Kyerwa kuwa pembezoni mwa nchi na kuwa mbali na wanasheria wa utetezi wa vyombo vya kisheria, wananchi wanyonge hususan wajane na wazee walikuwa wanadhulumiwa haki na mali zao. Awali ilionekana kama milango ya kupata haki zao imefugwa au imepotea, hivyo kero hizo zilikuwa zinasababisha wananchi wengi hasa wale wa hali ya chini vijijini kuishi maisha ya unyonge na kukosa matumaini ya maisha bora. Lakini kutokana na ziara ya Lukuvi chini ya bango ‘Funguka na Waziri Lukuvi’ na msimamo wa Serikali ya Rais Magufuli, wananchi wengi hasa wale waliokuwa wanajihisi wanyonge sasa wameanza kuwa na imani ya matumaini ya kuishi vizuri katika mashamba na mali zao mahali popote walipo. Hivyo, kutokana na ziara ya Lukuvi na mambo ya kijasiri aliyoyafanya hadharani ya kuweka bayana hatua ya msimamo wa kulinda wananchi na mali zao, kukemea na
kuonya watendaji wakorofi, tayari mafanikio mema yameanza kuonekana hapa na pale. Baadhi ya vikundi vya wakulima na wasanii wamesikika wakijigamba na kuimba hadharani nyimbo za kumshukuru na kumsifu Waziri Lukuvi. Hata hivyo wananchi wa Karagwe na Kyerwa licha ya kuwa wakulima wazuri wa kahawa na mazao mengine ya biashara, tunaomba mawaziri wa Biashara na Viwanda; Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Madini kuiga au kufuata mfano mzuri wa Waziri Lukuvi kutembelea wilaya za Karagwe na Kyerwa zilizo na milima mirefu na mabonde yanayoashiria uwezekano wa uwepo wa madini mengi kama vile madini ya bati (tin) yanayochimbwa kiholela bila utaalamu na mitaji ya kutosha; cobalt, dhahabu, malighafi ya kutengeneza chokaaa na madini mengine yanayowezesha harakati za kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda na miundombinu kwa haraka katika Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa jumla.
Mwandishi, Mzee Clement Nsherenguzi, ni msomaji wa Gazeri la JAMHURI. Anaishi Kijiji cha Kishao. Anapatikana kupitia S.L.P 12, Karagwe, Kagera au barua pepe: lukizamakubo@yahoo.co.uk.

1519 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!