Amani iliyopo Tanzania ni tunu ya taifa. Haikuibuka tu kama uyoga pori. Ni matokeo ya kazi kubwa na ya kutukuka iliyofanywa na waasisi wa taifa hili.

Wapo wanaodhani kuwa Watanzania ni tofauti na wanadamu wengi katika Afrika. Ni kweli tuko tofauti, lakini utofauti huu si wa kujitokeza wenyewe, au si wa kupendelewa na Mungu. Umoja na mshikamano wetu ni matokeo ya akili na utashi walioutumia wazee wetu na kuendelezwa na viongozi waliofuata – katika kujenga misingi imara ya utaifa.

Hii ina maana kwamba misingi hiyo ikiyumba – Mungu atusamehe tusifike huko – Tanzania itaingia kwenye klabu ya Burundi, Rwanda, Senegal, Afrika ya Kati na kadhalika.

Lugha ya Kiswahili, kuoleana, makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa, shule za kitaifa, uhuru wa kuishi popote nchini alimradi mtu havunji sheria, na kupinga aina zote za ubaguzi na ukandamizaji, ni baadhi ya mambo yaliyoiwezesha Tanzania kuwa kama ilivyo leo.

Ndiyo maana, kwa wanaoipenda hali hii iendelee, hawawezi kukaa kimya pindi wanapoona kuibuka kwa vimelea vya ubaguzi unaolenga kuleta mgawanyiko.

Hivi karibuni Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imempa onyo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, baada ya kujiridhisha na kosa la kusambaza kipeperushi na sauti kwa lugha ya Kisukuma akihamasisha kabila hilo kuunda kikundi.

Walichofanya polisi ni kumhoji Gwajima na baadaye kumuonya eti aache mara moja vitendo vya kuligawa taifa kwa kutumia vigezo vya ukabila.

 Pia anawataka Wasukuma kuunda vikundi kwenye mitandao ya kijamii vya watu 2,000 kwa lengo la kufuatilia watu wanaomtukana Mheshimiwa Rais na “kuwashughulikia”.

Huu ndiyo msimamo wa Gwajima, na hayo ndiyo majibu ya polisi katika kushughulikia jambo la hatari la kiwango hiki. Tangu lini polisi wakawa na uungwana wa kuwaonya watu waliokwishatenda makosa ya hatari kama haya ya kuligawa taifa?

Rais John Magufuli tunayemfahamu, hata kama lengo la Gwajima lilikuwa kumwonyesha kuwa anampenda sana, sidhani kama anaweza kufurahia kauli ya kuligawa taifa ya kiongozi huyo wa kiroho. Lakini pia sidhani tunaweza kuwa na polisi wanaodhani kuwa kwa kuwa aliyelengwa kutetewa ni rais, na kwamba rais ni wa hilo kabila lililosemwa, basi kumwachia Gwajima ilikuwa ni kumfurahisha Amiri Jeshi Mkuu! Siamini katika hayo yote mawili.

Ndugu zangu, Gwajima anao wafuasi wengi. Hata kama hatujui uwezo wa kutafakari wa waumini wake wote, bado tafakuri ya kawaida inatulazimu kuamini kuwa kauli yake ya “kuwashughulikia” wote wanaompinga rais inaweza kuamsha vita nchini.

Polisi wamemhoji Gwajima na kumwachia. Kama mtu anaweza kufanya jambo la hatari kama hili na akaishia kuhojiwa na kuonywa, vipi akijitokeza Mhaya, Mchaga, au Mtanzania mwingine anayetoka katika kabila kubwa – naye akatoa maneno ya kuhamasisha ukabila?

Itakuwaje akajitokeza muumini wa madhehebu fulani akasema mwaka huu wachaguliwe watu wa madhehebu fulani? Je, polisi wataishia kuwaita, kuwahoji na kuwaonya? Je, Gwajima anaachwa kwa sababu ni askofu au ni kwa sababu tunaogopa ‘vitisho’ anavyowarushia wanaomkosoa?

Ndugu zangu, kuna usemi wa kwamba ‘sumu haionjwi!’ Machafuko ni sumu. Tusilazimishe na wala tusithubutu kukaribisha machafuko.

Nchi nyingi zilizoyumba na kutoka kwenye mstari wa amani ni zile zilizoanza polepole kuwa na watu wanaotangaza ubaguzi kwa misingi ya ‘dini yetu’, ‘kabila letu’, ‘kanda yetu’, na kadhalika.

Gwajima alistahili kusimamishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Huyu hakuwa mtu wa kuhojiwa na kuachiwa. Ukabila katika Tanzania ni jambo linaloelekea kufa, kwa hiyo kulifufua ni kukaribisha balaa. Makabila yetu yameoleana kiasi kwamba Tanzania ni nchi yenye machotara wengi kweli kweli. Watoto wetu tunaopata leo si watoto wa makabila fulani kwa majina. Haya ndiyo mambo ambayo waasisi wetu walitamani kuyaona katika nchi hii – kwa maana kwamba tufike mahali mtu akiulizwa kabila lake ajibu bila wasiwasi kuwa yeye ni “Mtanzania”.

Mambo mazuri na yenye afya namna hiyo tunapoyavuruga kwa kuingiza mizizi ya kikabila, tunakosea. Wanaoitakia mema nchi yetu hawatakubali kuona Askofu Gwajima akimalizana na polisi kiulaini tu.

Na kama alifanya hivyo kwa kujipendekeza ili aonekane anampenda sana Rais Magufuli, basi atambue wapo wanaompenda na kumheshimu mno. Hao ndio wale waliohangaika juani kumpigia kampeni wakati yeye Gwajima akiwa upande mwingine akimvuta kanzu. 

Haya mahaba ya ghafla anayatoa wapi? Wanaompenda Rais Magufuli wanamuomba Mungu amjalie aendelee kuinyanyua Tanzania, na bila shaka yoyote aongezwe miaka mingine mitano na aimalize kwa mafanikio yaliyotukuka.

Wala sidhani kama Rais Magufuli anahitaji ulinzi wa kikabila kuliko ulinzi wa Mungu. Askofu Gwajima ni kiongozi mwenye heshima kubwa katika jamii. Basi, heshima hiyo imsaidie kulifanya taifa letu liendelee kuwa la watu wanaoishi kwa amani, upendo na mshikamano. 

Wote wanaoitakia mema nchi yetu waungane kuwakana watu wote wenye fikra kama za Gwajima. Makabila 126 kila moja likianza kuwaza kifedhuli, nchi hii itabaki magofu. Tuungane kuwapinga wote wenye kuhubiri na kuhamasisha aina zozote za ubaguzi.

650 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!