Arobaini ni mwarubaini (2)

Wiki iliyopita tuliishia mahali ambapo tulianza kuwaangalia wale tunaowaita mashujaa wa imani walijipaka majivu.

Majivu ni salio la moto, makazi yake ni jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya itakate! Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya sufuria. Majivu ya leo yakutakase kiroho!

Huu ni ujumbe ambao nilipokea kwenye simu siku ya Jumatano ya Majivu Februari 22, 2012. Ni siku ambayo Wakatoliki walipakwa majivu. Kupakwa majivu ni kuanza kipindi cha kufunga, kutoa sadaka, kusali kwa ajili ya kufanya toba. Ni kipindi ambacho kinaitwa Kwaresima.

Ujumbe mwingine ambao niliupokea katika simu unabainisha ya kufanya katika kipindi hiki. Ujumbe huo ni: Ukitaka kujua salio la mema yako – bonyeza kwaresima, kuongeza salio – toa sadaka, huduma ya kuongea na Mungu – piga sala, kwa maelezo zaidi, kwaresima njema.

Katika Biblia kuna mashujaa wengi wa imani waliojipaka majivu. Danieli alijipaka majivu. Katika sala yake Danieli alisali hivi: “Nikamwelekeza Bwana Mungu uso wangu katika sala na maombi, katika kufunga na kuvaa nguo za magunia na majivu.” (Danieli 9:3).

Mfalme Daudi ni shujaa mwingine ambaye hakujipaka tu majivu bali aliyachanganya na chakula. Katika Zaburi yake ya toba alisema hivi: “Nami, ninakula majivu kama mkate, ninachanganya kinywaji changu na machozi.” (Zaburi 102: 10).

Majivu haya yana rangi ya kijivu ambayo ni rangi ya toba. Toba ni mapinduzi ya kiroho. Toba ni kujirekebisha kiroho. Katika kufanya toba tunaungama dhambi zetu. Njia nyingine nzuri ya kufanya toba ni kuwaombea wengine. Majivu husaidia katika kusafisha vyombo kama sufuria. Kupakwa majivu ni ishara ya kuwa toba huondoa doa la dhambi. Majivu ni mbolea nzuri. Ishara hii ni kuwa toba inasaidia kurutubisha matendo mazuri kama mbolea ya majivu inavyosaidia kurutubisha mimea.

Majivu Wakristu wanayojipaka yanapatikana kutoka katika mti wa mtende ambao ni jamii ya mchikichi. Matawi haya ni yale ambayo huwa yamebebwa siku ya Jumapili ya Matawi ambapo tunakumbuka Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe. Matawi haya zamani yalibebwa baada ya ushindi vitani.

Nasi kwa kupakwa majivu ya matawi haya tunakiri kuwa pamoja na Yesu tutashinda. Majivu haya ni mabaki ya matawi yaliyochomwa kuonyesha utupu wa anasa za dunia. Majivu haya yanawekwa kwenye paji la uso ambalo ni kiti cha majivuno, kuonyesha sisi hatupaswi kujivuna. Padri anasema maneno haya: “Kumbuka wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi.” Waliokufa kama wangekuwa wanasema wangetwambia: “Jinsi mlivyo ndivyo tulivyokuwa. Jinsi tulivyo ndivyo mtakavyokuwa.” Majivu yanatukumbusha kifo chetu; maana yake kutumia muda wa maisha duniani ili tukaribishwe mbinguni.

Neno kufunga katika Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi linamaanisha kujizuia kula, kutosema, kunyamaza, kuzuia kisiingie au kutoka. Maana hii inaafikiana na kile ambacho kinafanyika katika kipindi hiki ambacho Wakatoliki hukiita kwaresima, kipindi cha siku arobaini cha kufunga, kuna kujizuia kula.  Kufunga huku kunaambatana na matendo ya kusaidia maskini, kutoa sadaka na kufanya toba.

Majivu hutumika kama mbolea. Kuna mbolea kama ya chumvi chumvi. Mbolea ni majani na kemikali zitiwazo mashambani kuimarisha ardhi iwe na rutuba ili kupatikane mazao mazuri kwa wingi. 

Katika jamii nyingi za Kiafrika, majivu yalitumiwa kama mbolea ya chumvi. Kipindi cha kufunga siku arobaini ni kipindi cha Wakatoliki kuweka ‘mbolea’ katika maisha yao ya matendo ya kujinyima na kuwasaidia wengine ili waweze kuzaa matunda mazuri ya matendo mema na maneno mema na kukua katika maisha ya kidini na kimaadili. Kwa kupakwa majivu usoni ni ishara ya kutaka kuboresha maisha yao kwa matendo mema, kusali na kuwasaidia maskini.

Wakatoliki siku ya Jumatano ya Majivu walipakwa majivu kwenye paji la uso kama ishara ya  kuwa kichwa ni kiti cha majivuno. Kuwakumbusha kuwa binadamu hana budi kunyenyekea badala ya kuwa na majivuno, kwa vile tutarudi kuwa mavumbi na majivu, hatuna haja ya kujivuna. Lakini kwenye majivu kuna cheche za moto wa matumaini ya ufufuko.