Ninaomba kukunong’oneza jambo hili: Usithubutu kumuacha Mungu kwa ajili ya chochote, bali acha chochote kwa ajili ya Mungu, kwa sababu katika maisha chochote chaweza kukuacha wakati wowote. Lakini Mungu atakuwa nawe siku zote za maisha yako. 

Siri kubwa ambayo unatakiwa kuifahamu ni kwamba Mwenyezi Mungu ni rafiki yako mwema hata pale unapokabiliwa na nyakati ngumu katika maisha.

Kuna mtu ambaye aliota ndoto. Ndoto yake ilimuonyesha kwamba alikuwa anatembea kando ya bahari yenye mchanga. Alipokuwa na furaha alitazama nyuma na kuona nyayo za watu wawili. Alipokuwa na shida alitazama nyuma na kuona nyayo za mtu mmoja. Ndoto hii ilimtatiza sana. Akiwa bado kwenye ndoto yake alimuuliza Mungu maana ya ndoto yake. Mungu alimjibu kwa kumwambia: “Unapokuwa na furaha tunakuwa pamoja, ndiyo sababu unaona nyayo za watu wawili.” Mtu huyo alidadisi tena na kuuliza: “Mbona wakati  wa shida ninaona nyayo za mtu mmoja?” Mungu alimjibu kwa kumwambia: “Wakati wa shida ninakubeba mgongoni ndiyo sababu unaona nyayo za mtu mmoja.” Zile nyayo za mtu mmoja ni zangu mimi (Mungu). Yule mtu alishituka kutoka ndotoni na kupaza sauti akisema: “Mungu sitakuacha.” Tusimuache Mungu, tumuache shetani.

Nilipokuwa ninaandika makala hii nilitafakari kwa undani sana falsafa ya Mwanafalsafa wa kipagani, Bertrand Russel, inayosema: “Bila kukubali kuwa kuna Mungu, swali kuhusu kusudi la maisha halina maana.” Mchungaji Rick Warren aliandika hivi katika kitabu chake cha kumbukumbu: “Nilipompenda kwa mara ya kwanza mke wangu nilimwambia ninamwamini Mungu katika maisha yangu. Naye akanijibu kwa uso uliojaa tabasamu la upendo akisema kama ungekuwa humwamini Mungu nisingekubali kuolewa na wewe.”

Dunia inamkumbuka Adolf Hitler kama dikteta na katili, lakini pamoja na kwamba Hitler alikuwa katili aliamini uwepo wa Mungu. Kwenye sare za askari wake aliandika maneno haya: “Mungu yuko nasi.”

Mungu aliumba mtu ambaye anampenda. Mungu anakupenda sana. Naomba kukukumbusha jambo moja na la muhimu sana. Jambo hilo ni hili: “Siku zako za kuishi hapa dunia zinahesabika.” Mwisho wa maisha yako ya hapa duniani utasimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, na Mungu atakuonyesha namna ulivyoishi. Utaonyeshwa namna ulivyoutumia muda wako katika mambo ya msingi na yasiyo ya msingi. Utaonyeshwa namna ulivyokuwa na juhudi katika kusali na namna ulivyokuwa mvivu wa kusali. Utaonyeshwa namna ulivyotumia karama yako katika kujiendeleza na kuwaendeleza wengine.

Kama uliishi maisha ya sala utasikia sauti ikikuambia: “Hongera mwanangu, umepigana vita iliyo nzuri na mwendo umeumaliza.” Na kama haukuishi maisha ya sala, hautaisikia sauti ya heri. Utasikia sauti ikikuambia: “Pole kwa kuukosa utukufu wa wateule.”

Tujitahidi kusali ili mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani uwe wa baraka. Ukristu wetu usiwe wa kinafiki. Ninamaanisha hivi: Tusivae sura za Ukristu siku za Dominika tu. Matunda ya Ukristu wetu lazima yawe hai siku zote.

Wakati fulani Padri E. Stanley Jones alikwenda kumhubiria habari njema Baba wa Taifa la India, hayati Mahatma Gandhi. Mwisho wa mahubiri Mahtma Gandhi alimwambia Padri Jones: “Nampenda Yesu Kristo wenu lakini siwapendi Wakristo wenu. Hii ni kwa sababu Wakristo wenu hawafanani kabisa kimatendo na Yesu Kristo wenu.” Mahatma Gandhi alikuwa anafahamu maisha aliyoishi Yesu. Kristo hakuishi maisha ya kinafiki.  Kristo hakuwa ndumila-kuwili.

Swali la msingi ambalo unatakiwa kujiuliza katika makala hii ni hili: “Je, maisha yako yanafanana na maisha ya Yesu Kristo?” Jaribu kuyatazama upya mahusiano yako na Mungu wako kwa uzito unaotakiwa. Kuna wakati mwanadamu anaishi kama ‘Mungu’ na kuna wakati anaishi kama ‘shetani’.

Pale mwanadamu anapojisahau na kuishi maisha yake kwa mtindo wa ‘kishetani’, anapoteza hadhi yake ya ubinadamu na kupokea hadhi ya ‘ushetani’.

Tunapobatizwa tunakuwa tumempa shetani notisi ya kuhama kutoka kwetu, lakini maisha yako unayoyaishi yanaweza kumkaribisha tena shetani moyoni mwako au yanaweza kumfukuzia mbali.

Kumbuka Mtume Petro anavyotuonya: “Muwe na kiasi na kukesha kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba aungurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yaleyale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.” (1Pet 5:8,9).

Ukweli ni kwamba shetani hajalala wala hajaenda likizo. Yumo kazini. Shetani ana historia ya kupambana ila hana historia ya kushinda.  

Baba wa Kanisa Theophly alipata kuandika: “Yesu baada ya ubatizo alishawishiwa na shetani, kuonyesha kwamba hata sisi baada ya ubatizo hatuwezi kuvikwepa vishawishi vya shetani ila tunaweza kukabiliana navyo na kushinda.”

By Jamhuri