Atatoka wapi Mzee Mayega mwingine?

DAR ES SALAAM

Na Abdul Saiwaad

Katikati ya miaka ya 1980, sikumbuki ilikuwa mwaka gani hasa, nilipofahamishwa kwa Paschally Boniface Mayega. Rafiki yangu aitwaye Kamugisha ndiye aliyenitambulisha. 

Tulikutana Posta Mpya ambapo Mayega alikuwa akifanya kazi Idara ya Mauzo ya Simu. Kamugisha alinieleza kuwa, Mayega alikuwa mpenzi wa vitabu na uandishi na alitaka kuanzisha kampuni yake binafsi ya uchapishaji wa vitabu. 

Akilini niliwaza na kuamua kuwa ama huyu mtu ni jasiri sana au hamnazo! Mawazo haya yalinipitia kwa kuwa katika kipindi hiki, hali ya uchapishaji vitabu ilikuwa mbaya kwa sekta binafsi na hata kwa mashirika ya umma. 

Sikudhani kuwa kulikuwa na maisha katika uchapishaji vitabu katika siku za usoni. Wakati huo mashirika ya umma yalikuwa taabani kwa kila hali. 

Vitabu vilikuwa havichapishwi, vitabu haviagizwi wala kununuliwa, mitaji ilikuwa imepelea kiasi kwamba muda mwingi wafanyakazi walikuwa wakipiga soga badala ya kufanya kazi! 

Wakati huo nilikuwa ninafanya kazi shirika la la umma, Eastern Africa Publications (EAPL), Arusha. Hata hivyo, MPB Enterprises, kampuni ya uchapishaji vitabu ilianzishwa, na Kamugisha akaajiriwa kama mhariri na meneja uchapishaji. 

Baada ya hapo tuliendelea kukutana na kuzungumza wakati wowote nilipokuwa Dar, kwani stesheni yangu ya kazi ilikuwa Arusha. Tulikuwa na maongezi mengi kila tulipokutana. 

Tulikutana na Mayega mara nyingi zaidi baada ya Septemba 1987 wakati Chama cha Wachapishaji Vitabu (Publishers Association of Tanzania – PATA) kilipoanzishwa. 

PATA ilipewa nafasi ya ofisi katika ofisi za Tawi la EAPL, Dar es Salaam, Jengo la Customs (wakati ule). Katibu Mtendaji wa kwanza wa asasi hiyo alikuwa Kamugisha; aliyekuwa bado mfanyakazi wa MPB. 

Ajira ya Kamugisha pale PATA ilikuwa kwa ahadi kuwa mambo yakiwa mazuri, atalipwa mshahara. Hivyo kimsingi alikuwa akiishi kutokana na kazi zake za MPB iliyokuwa ikifanya vizuri wakati ule kwani iliweza kutoa walau kitabu kimoja kila miezi sita. Tena kitabu kisichokuwa na oda maalumu, kama ilivyokuwa kwetu wachapishaji wa umma. 

Baada ya PATA kuanzishwa, moja ya madhumuni yake ilikuwa ni kuhamasisha na kuelimisha kuhusu umuhimu na uhitaji wa sekta ya uchapishaji ya uzawa iliyokuwa na nuru na kampeni iliyofanywa mapema kabisa ni kuandaa matamasha ya vitabu ili kusheherekea vitabu. 

Licha ya maonyesho ya vitabu vya wachapishaji mbalimbali yaliyofanyika Dar es Salaam, kulikuwapo sherehe za kila aina kama ngoma, tafrija, uzinduzi wa vitabu, semina, ukaribisho wa viongozi wa serikali na matoleo katika magazeti.  

Bwana Mayega alikuwa mjumbe Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Kwanza la Vitabu lililokuwa na dhima kuhusu usomaji wa vitabu. 

Walter Bgoya aliongoza kamati akiwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tamasha la Vitabu lililofanyika Septemba 1988, katika Ukumbi wa Arnautoglu, Dar es Salaam. 

PATA ilipotangaza nia ya kuandaa Tamasha la Wiki ya Vitabu, watu wengi walidhani pasipo shaka kuwa walikuwa na mamilioni ya shilingi kibindoni kufanikisha tamasha hilo. 

Ukweli ulikuwa tofauti kabisa. PATA haikuwa hata na senti moja, isipokuwa hamasa na matumaini ya akina Mayega na Kamugisha. 

Baada ya mafanikio ya tamasha la mwaka 1988, Mayega alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tamasha la Wiki ya Vitabu mwaka 1989; tamasha la pili. 

Kuchaguliwa kwa Mayega kulizua mshangao miongoni mwa wengi katika tasnia ya vitabu wakati huo. Mayega alikuwa mchapishaji mdogo, asiyejulikana kimataifa, na mchapishaji anayepambana kubaki katika biashara hiyo iweje awe mwenyekiti! 

Ilionekana ni maajabu na mchakato wa maafa na aibu. Hata mwaka 1989, PATA  haikuwa na fedha za kuandaa tamasha kwa ufanisi. Lakini Mwenyekiti Mayega alikuwa na imani  na alidhamiria kuwa tamasha hilo litakuwa kubwa na bora zaidi kuliko la mwaka uliotangulia. 

Na likawa hivyo! Waziri wa Habari wa wakati huo, Benjamin Mkapa, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi. Alipoona foleni inamkwamisha kufika eneo la tukio, Mkapa alishuka kwenye gari Starlight Hotel, na kuvuka barabara kwa miguu kuingia Arnautoglu, aweze kufika wakati uliopangwa. 

Mwaka 1989 kulikuwapo warsha ya uandishi wa vitabu vya watoto. Warsha hiyo iliteua miswada mitano bora kutoka kwa wachapishaji ambao baadaye ilichapishwa na kuwa vitabu vya watoto. 

Hivi vilikuwa vitabu vingi zaidi vya watoto vilivyowahi kuchapishwa kwa mpigo kwa miaka mingi. Uchapishaji wa vitabu hivyo ndiyo ilikuwa chanzo cha kufanya utafiti uliokuja kubuni kuanzishwa kwa Mradi wa Vitabu vya Watoto (Children’s Book Project in Tanzania). 

Mradi huo ukawa chachu ya kuchapishwa vitabu vingi bora vya watoto kwa miaka mingi baadaye.

Paschallly Mayega alizaliwa mwaka 1950 katika Kijiji cha Mkonko, Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. 

Alipata elimu Seminari ya Kaengesa, Sumbawanga, kisha Ntungamo Senior Seminary, Bukoba. Baada ya kumaliza elimu yake, alijiunga na East African Posts and Telecommunications Company (moja ya mashirika ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani) na akapata mafunzo Mbagathi Postal Training School nchini Kenya. 

Mayega ameacha mjane na watoto watano. Mkubwa ni msichana na mwanafunzi wa uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).  

‘Mkonko’ ni miongoni mwa vitabu vyake vya kwanza alivyoandika. Vilevile amechapisha vitabu vya waandishi wengi na maarufu kama Profesa Mugyabuso Mulokozi, Hammie Rajab na Thomas Kamugisha kwa kuwataja wachache. 

Ari yake kuhusu vitabu na uandishi ilimfanya aandike vitabu vingi vya watoto kama Sisimizi Amuua Tembo na vingine katika mfululizo wa Watoto wa Afrika wanatembelea Mbuga za Wanyama

Kitabu chake bora ambacho kimepata umaarufu mkubwa Tanzania na duniani ni Mwalimu Mkuu wa Watu ambacho kilichapishwa mwaka 2006. 

Kwa taarifa nilizopewa na Mayega, kitabu chake kinatumika kufundishia katika baadhi ya vyuo vikuu. Kitabu hiki pia kimetafsiriwa na kuchapishwa kama The Peoples Headmaster. 

Nakumbuka mwaka jana, baada ya mkutano wa Kamati ya Utendaji wa PATA uliofanyika Regent Estate, usafiri wangu haukuwasili. Nikamuomba Mayega anisogeze nikapande daladala niende Kariakoo, wakati yeye akiendelea na safari yake kwenda Mbagala. 

Akaniambia kwanza atanipeleka mimi Kariakoo, kisha atatumia njia ndefu kwenda kwake Mbagala. Katika nyakati hizi ngumu, ‘marafiki’ wengi wangeniacha kituoni. Lakini si rafiki Mayega. 

Katika miaka takriban 15 Mayega alikuwa na safu yake katika magazeti ya JAMHURI na Tanzania Daima. Safu hizi zilikuwa zikienda kama Fikra za Mwalimu Mkuu au Rais Wangu.  Katika safu hizi alikuwa akikosoa, akilaumu au kushauri sera au matendo ya serikali. 

Katika moja ya safu zake alizoandika mwishoni mwa mwaka jana au mapema mwaka huu ilikuwa na kichwa cha habari: Bado Kidogo Hamtaniona Tena; na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa marafiki na maadui kwa usawa huohuo. 

Watu wengi, mimi nikiwamo, tulipiga simu kuulizia kuhusu hali yake. Akatuarifu kuwa hajambo. Baada ya hapo tukarudi kusoma ile makala!

Katika ulimwengu wa vitabu, Mayega alikuwa maarufu. Alisafiri mara nyingi kwenda katika maonyesho ya vitabu ya Harare, yakiitwa ‘Zimbabwe International Book Fair’, pia ya Afrika Kusini; ‘Cape Town Book Fair’ na ya dunia; ‘Frankfurt Book Fair’. 

Licha ya kushiriki katika kuonyesha vitabu, pia alishiriki katika mahojiano kuhusu sababu na msukumo aliopata kuandika kitabu cha Mwalimu Mkuu. Alikuwa na urafiki na watu wa vitabu katika kanda ya Afrika Mashariki, Afrika na kimataifa. Baadhi ya vitabu vyake vinauzwa kwa leseni nchini Kenya na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa masharti maalumu. 

Safari ya mwisho tulipoonana ana kwa ana, ilikuwa mapema mwaka huu. Kabla ya hapo, mwaka 2019 katika makala yake alisanifu tatizo la usomaji wa vitabu vya burudani kwa watoto wa ‘shule za Kayumba’. 

Ikatokea kuna mtu serikalini aliguswa na makala yake na kwa hiyo kampuni yake pamoja na kampuni nyingine tisa zikaalikwa kuwasilisha vitabu vya watoto kwa ajili ya tathmini ili kutumika shuleni.  

Maelekezo ya mwanzo ilikuwa wanunue vitabu vyake tu. Alikataa upendeleo huo. Hakuna kitabu kilichowasilishwa kilichokuwa na kurasa zaidi ya 32 ya maandishi na michoro. 

Vitabu viliwasilishwa Desemba 2019. Vitabu vyake vilikuwa viwili vya wastani wa kurasa 20 na maneno 80 ya maandiko. Ilipofika Machi 2021, tulikuwa tukiliwazana na kulaumu kuhusu muda ambao taasisi inachukua katika kupata ithibati ya kitabu cha kurasa 20.  Hasa ukizingatia kuwa vitabu hivi vipo sokoni, si Tanzania tu bali hata katika nchi jirani na vinapendwa na watoto. 

Kisha tukazungumzia kuhusu hali mbaya ya tasnia ya vitabu na uchapishaji nchini, tunaweza kufanya nini? Kipi kifanyike? 

Saiwaad, we acha tu,” yalikuwa maneno yake ya mwisho wakati tulipokutana. Baadaye nikasikia anaumwa na aliwahi kulazwa Temeke Hospital. Nilipopata taarifa alikuwa tayari ameshatoka. Kwa hiyo tukaendelea kuwasiliana kwa simu. Siku zote alikuwa akimalizia maongezi yatu na: “Nashukuru kwa kunijulia hali kaka.”

Simu yangu moja haikuwa inafanya kazi Jumamosi ya Oktoba 30, mwaka huu, Margharita Mayega, mwanaye wa kwanza alijaribu kunipigia mara tatu kuniarifu kuhusu kufariki dunia kwa baba yake bila mafanikio. 

Nilipata taarifa ya kufariki dunia kwa rafiki yangu Paschally Mayega katika kundi sogozi la wachapishaji (WhatsApp).  Mayega amezikwa nyumbani kwake Novemba 1, 2021.

Hali ya sekta ya uchapishaji ya miaka ya 1980 inafanana sana na hali ambayo wanayo wachapishaji wa leo Tanzania. 

Atatokea wapi Mayega mwingine, jasiri kiasi cha kupambana na changamoto za tasnia zilizokuwapo?  Nani atawahamasisha wenzake umoja na umuhimu wake wa kupambana kubadili hali? Nani ataweza kuwahakikishia mapambano ili kupata paradiso wachapishaji wa vitabu hasa vitabu vya kiada?

Najua Mayega atakuwa anatabasamu katika kaburi lake na Mwenyezi Mungu atakuwa anatabasamu naye. Ametimiza wajibu wake kikamilifu. Pumzika kaka. Amina!

0683 286 406