1. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani na kuliboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya, je, idadi ya  abiria imeongezeka kiasi gani tofauti na ilivyokuwa awali?

JIBU: Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani Novemba 5, 2015. Kati ya ahadi zilizotolewa na Mhe. Rais wakati wa kampeni za uchaguzi ni pamoja na kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).  Mwaka 2016 tulikuwa tunabeba abiria 4,000 hadi 5,000 kwa mwezi, hiki ni kipindi ambacho ndiyo tulikuwa tuna ndege moja aina ya Bombardier Dash8-Q300 au kutumia ndege za kukodi, pia tulikuwa tunaruka viwanja vitatu ambavyo ni Mwanza, Kigoma na Comoro. Katika viwanja hivyo tulikuwa na safari chache sana kiasi cha kutotosheleza soko, mfano Kigoma tulikuwa tunaruka mara tatu kwa wiki, Mwanza mara nne kwa wiki, Comoro ilikuwa ni mara tatu kwa wiki.

Utekelezaji wa mpango wa kuifufua ATCL ulianza mwezi Oktoba 2016. Kipindi kilichomalizika cha Julai hadi Desemba 2018 tulibeba abiria 216,762, kwa mwaka, idadi hiyo ni sawa na wastani wa abiria 36,127 kwa mwezi.  Hivyo utaona kuwa tumekuwa tukiongeza idadi ya abiria mwaka hadi mwaka.

Kuongezeka kwa abiria kumechangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa ndege na kupanuka kwa mtandao wa safari zetu.

Sababu nyingine muhimu ni kuendelea kuboreka kwa huduma zetu, hivyo kuongeza imani kwa wateja wetu ambapo umiliki wa soko (market share) umepanda kutoka asilimia 2.5 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 41 mwaka 2018.

2. Je, ATCL ina mkakati gani wa kupanua soko kwa kuongeza safari zake nje na ndani ya nchi?

JIBU: Mkakati wa kupanua soko na kuongeza safari nje na ndani ya nchi unahusisha kupata ndege zenye uwezo unaotakiwa kukidhi ushindani na uchaguzi wa vituo vya safari unaotokana na upembuzi yakinifu. Hivyo utaona kuwa kufuatana na ndege zilizopo na upembuzi wa soko uliofanyika tunatarajia kupanua soko la ndani kwa kuongeza  safari mpya za Iringa, Mpanda (Katavi) na Pemba. Upande wa safari za nje tunategemea kuanzisha safari za Lusaka (Zambia), Harare (Zimbabwe) na Johannesburg (Afrika Kusini) hii ni kwa Afrika. Nje ya Afrika tunatarajia kuanza safari za India (Bombay), Bangkok (Thailand) na Guanzhou (China), safari hizo zitaanza wakati wowote kati ya Februari hadi Juni, mwaka huu. Kuna mikakati pia inayoangalia mbele zaidi kabla ya kukamilika kwa Mpango Mkakati wetu wa miaka mitano (Julai 2017 hadi Juni 2022), ambapo tunatazamia kuingia katika soko la Kenya, Nigeria, Ghana, DRC, Mashariki ya Kati, na Uingereza.

3.  Je, ATCL ina idadi ya watumishi wangapi kwa sasa ikilinganishwa na awali kabla ya kuongezewa ndege ambazo zinamilikiwa na serikali?

JIBU: ATCL ina jumla ya wafanyakazi 413 huku ikiwa na ndege sita zinazotoa huduma, hivyo kuwa na uwiano wa watumishi 69 kwa ndege moja. Awali kabla ya kuongezeka ndege, kampuni ilikuwa na wafanyakazi 171 huku ikiwa na ndege moja, yaani uwiano wa watumishi 171 kwa ndege moja. Tumejiwekea malengo katika Mpango Mkakati wetu wa miaka mitano kuwa na ukomo wa uwiano wa wafanyakazi 87 kwa ndege moja. Uwiano huu unashabihiana na idadi iliyopo kwa mashirika ya ndege yanayofanya vizuri.

4.  ATCL imeweka mikakati gani kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kwa kutumia usafiri wa ndege hizo?

JIBU: Pamoja na mikakati mingine, dhana ya serikali kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania ni kuiwezesha sekta ya utalii nchini. Kwa hiyo mkakati wetu wa kwanza ni kujiimarisha kwa safari za humu nchini ili kuwarahisishia watalii kufika katika vivutio vyetu. Hivyo pamoja na suala la kuangalia takwimu za wasafiri, mtandao wetu wa safari ndani ya nchi umetilia maanani urahisi wa kuvifikia vivutio vya utalii tulivyonavyo kwa kuwa na safari za Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro, Kilimanjaro kwenda Zanzibar, Dar es Salaam kwenda Kigoma, Mbeya, Mwanza na kuanzisha safari za Iringa na Mpanda na siku za mbeleni kuhakikisha tuna safari za Tanga, Pemba na Musoma.

Miji tuliyoichagua kuanza nayo nje ya nchi nayo tumeichagua ikiwa na mkakati wa kuwabeba watalii kuja Tanzania. Tumeangalia masoko ya kawaida kwa watalii wanaokuja Tanzania kama Afrika Kusini kwa Afrika na Uingereza kwa watalii kutoka Bara la Ulaya na Marekani. Pia tumejielekeza katika masoko mapya lakini yenye kukua kwa kasi kubwa kwa kuleta watalii Tanzania kama China, India na nchi za Mashariki ya Mbali ambazo watalii wanaweza kuja Tanzania kwa urahisi kupitia China na Thailand. Kuna muongezeko pia wa watalii kutoka Afrika Magharibi hasa Nigeria, hivyo ni soko ambalo linatakiwa kuhamasishwa kwa kuwezeshwa usafiri wa moja kwa moja kuja Tanzania.

5.  Shirika la ATCL limejiimarisha kwa namna gani katika ushindani wa kibiashara dhidi ya mashirika mengine?

JIBU: Kwanza tunaanzia kwenye vitendea kazi vyenyewe, tunazo ndege za kisasa ambazo zitavutia wasafiri, zenye teknolojia ya kisasa kabisa huku gharama zake za uendeshaji zikiwa za chini. Kuhakikisha tunatoa huduma inayoendana na matarajio ya mteja wetu kuanzia anapokata tiketi yake hadi anapochukua mzigo wake mwisho wa safari yake. Tunamhakikishia msafiri, pamoja na huduma nzuri anayopata, usalama wake, uwezekano wa kufika anakokwenda kwa muda unaotakiwa na starehe katika safari yake (comfortability).

Hivyo mikakati yetu ya ushindani inatuhakikishia kuwa tunashughulikia matamanio ya mteja (customer expectations) kwani tuna ndege za kisasa, kuna viburudisho ndani ya ndege na tunajitahidi  kuondoka na kufika kwa muda  katika safari zetu. Sambamba na hilo, tumeendelea kuhakikisha nauli zetu zinakuwa za chini na zenye uhalisia. Tumeweka mtandao mzuri wa kuuza tiketi zetu hapa nchini na kimataifa kwa kuhakikisha upo uwezo wa kununua wewe mwenyewe kwa njia ya mtandao popote duniani, wakala zaidi ya 300 hapa nchini, pia kuwa katika mtandano wa uuzaji tiketi duniani (Global Distribution System – GDS) unaoratibiwa na Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA) ili kuhakikisha tiketi zetu zinapatikana kwa mawakala dunia kote.

6.  Je, ATCL imejipanga namna gani kuwapa mafunzo watumishi wake ili kuongeza ufanisi katika huduma ya usafiri wa anga ndani na nje ya nchi?

JIBU: Tuna mpango wa mafunzo unaoendana na Mpango Mkakati wetu wa miaka mitano ukihusisha mafunzo ambayo ni lazima kwa baadhi ya kada fulani za wafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za usafiri wa nga, mfano marubani, wahandisi, uendeshaji (operations) na mafunzo yanayohitajika katika kuongeza tija na weledi wa wafanyakazi wetu. Kutokana na gharama kubwa ya mafunzo ya wataalamu wa usafiri wa anga, tumeanzisha mashirikiano na baadhi ya mashirika ya ndege na makampuni mengine yanayotoa mafunzo haya ili kupeleka wafanyakazi wetu kujifunza katika vyuo vyao au kuleta wakufunzi hapa Tanzania.

7.  Je, ni lini ATCL itaanza kutumia ndege mbili zilizokuwa zinatumiwa na viongozi kama alivyoelekeza Rais Dk. John Magufuli?

JIBU: Maelekezo ya Mhe. Rais Dk. John Joseph Pombe Magufuli aliyoyatoa tarehe 11, Januari 2019 yalipokelewa na tayari tumekwisha kuanza mazungumzo na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), tayari tumezungumza namna ya kupaka rangi pamoja na namna ya kuzihamishia huku ATCL zitumike kama ilivyoelekezwa.

Kuongezeka kwa ndege hizo kutaongeza thamani kubwa kwetu, maana ndege hizo zitasaidia sana kwenda kwenye masoko ambayo yana idadi ya wasafiri wanaoendana na uwezo wa ndege husika.

8.  Ili kufanya biashara yoyote ni lazima kuwe na mwongozo (Business Plan), je, ATCL inayo business plan ambayo inatoa mwongozo wa biashara wa shirika?

JIBU: Mwaka 2014 ATCL ilitayarisha Mpango wa Biashara (Business Plan) wa miaka mitano (2015 – 2020) kupitia Kampuni binafsi ya Deloitte. Kampuni hii ilifanya utafiti juu ya soko la Tanzania na masoko ya nje ya Tanzania na kutayarisha mpango huo ukiwa na lengo la kufufua huduma za ATCL ambao hatimaye uliwasilishwa serikalini kwa hatua zaidi.

Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani iliteua timu ya wataalamu ambao walipitia mpango huo na kukubaliana na baadhi ya mapendekezo yakiwemo ununuzi wa ndege na aina inayotakiwa.

Katika mwendelezo wa kuifufua kampuni hii, serikali iliteua uongozi mpya wa ATCL, yaani bodi ya wakurugenzi na mkurugenzi mkuu. Uongozi mpya uliupitia mpango huo wa biashara  kwa upya na kuona kwamba una mambo ambayo yalikuwa yamepitwa na wakati, hivyo kuwa na haja ya kuunda mpango biashara mwingine wa mpito (Interim Business Plan) ukiwa kama mwongozo wa utekelezaji wa Mkakati wa Mageuzi wa ATCL (Turn Around Strategy) kuanzia Oktoba 2016 hadi Juni 2017 na kuhusisha pia mapitio ya Mpango wa Biashara wa Deloitte ili kutayarisha Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa mpango wa biashara wa mpito.

Mpango huo wa mpito ulilenga kuweka mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa biashara ya ATCL ili kuhakikisha kuna ufanisi na tija, kuweka miundombinu yenye tija inayotakiwa katika utoaji wa huduma, ikiwemo ya kuuza tiketi, kufufua tovuti ya kampuni, kufufua mifumo ya malipo kwa njia ya benki na mitandao ya simu na  kufungua ofisi kwenye vituo vipya. Mpango pia ulihusisha kupitia muundo wa ATCL (Organization structure) ili kupata muundo unaoendana na mikakati mipya, pia kutayarisha mpango mkakati mpya wa miaka mitano (Julai 2017 hadi Juni 2022).

Katika utekelezaji wa mpango huo wa biashara wa  mpito, uongozi huo uliamua kutengeneza mpango mkakati wa miaka miatano (Strategic Plan) kuanzia mwaka wa serikali 2017/18 mpaka 20121/22.

Mpango mkakati wa miaka mitano (Julai 2017 – Juni 2022), unatekelezwa kupitia mipango ya biashara (Business Plan)  ya kila mwaka kulingana na malengo na matarajio yaliyokusudiwa katika mpango mkakati kwa mwaka husika.

Hivyo mpango mkakati wa miaka mitano upo kama tulivyokuonyesha na hakuna kinachofanyika bila kuwa katika mpango mkakati huo  ukitekelezwa kupitia mpango wa biashara wa kila mwaka. Tumekuonyesha nakala ya Mpango wa Biashara (Business Plan) wa miaka mitano (2015 – 2020) uliotayarishwa na  Deloitte, uliokuwa msingi wa mpango wa ufufuaji wa ATCL,  pia umeona nakala ya Mpango Biashara wa Mpito (Interim Business Plan, Oktoba 2016 – Juni 2017) ulioongoza utekelezaji wa Mkakati wa Mageuzi wa ATCL (Turn Around Strategy).

9.  Shirika hili ni mali ya wananchi Watanzania. Je, Watanzania watarajie nini kwa shirika lao baada ya kupata ndege mpya na za kisasa?

JIBU: Watanzania watarajie shirika kuendeshwa kwa ufanisi na weledi, kupata huduma bora na za uhakika hapa nchini na nje ya nchi, nchi kutangazwa ndani na nje, watalii kuongezeka kwa wingi, mizigo kusafirishwa kwa wingi, ajira kupatikana kupitia ATCL na wataalamu wazawa katika sekta ya usafiri wa anga kuongezeka kutokana na kufundisha vijana wengi wa Kitanzania.

1420 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!