Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kumpata kiongozi shupavu. Mungu ni mwema, akamuinua Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli awe Rais wa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015.
Kabla ya uchaguzi huo, Watanzania wengi walitarajia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kingeporomoka. Kusema kweli haikuwa kazi rahisi, bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kumpata rais shupavu na mchapakazi kama inavyofahamika sasa: “Hapa Kazi Tu.”
Siku moja kwenye basi la mwendokasi, Kimara kwenda Feri/Kivukoni baadhi ya watu walitathmini uchaguzi wa Oktoba 2015.
Mmoja alisema: “Kura za upinzani ziliibwa.” Hapo hapo mzee mmoja akajibu kwamba yeye wakati ule alipenda sana upinzani ushinde maana alikuwa amechoshwa na utendaji usioridhisha wa serikali. Baada ya kuona kuwa aliyeshinda kwa kipindi kifupi ameonyesha mwelekeo mzuri, akasema: “Kama kweli kura ziliibwa ni bora ilikuwa hivyo.”

Baadhi yetu tuliunga mkono kauli hiyo. Hakuna siri kwa kipindi kifupi cha miaka mitatu tangu awe madarakani tumeshuhudia masuala mazito ambayo ameyafanya kwa faida ya taifa letu na watu wake.
Rais anayo dhamira ya kweli kupigania rasilimali za nchi zisiendelee kuporwa na wachache (the elite); anapambana na rushwa na dawa za kulevya na ukiukwaji wa maadili. Ofisi za serikali kuna nidhamu na heshima ya kutosha. Huduma zinatolewa bila ubabaishaji tuliouzoea wa “njoo kesho; jalada husika halionekani/limepotea.” – Nia ya mtoa huduma ikiwa “apate kitu” kutoka kwa anayehitaji huduma.
Rais amenunua ndege ili kufufua Shirika la Air Tanzania (ATCL) ambalo ni chombo cha taifa (national carrier). Baadhi yetu tukadhani ni kisiasa, eeeh Mungu mwema, haukupita muda mrefu ndege zikaanza kuingia nchini na Desemba, 2018 tumepokea ndege kubwa zenye hadhi kimataifa.

Ujenzi wa ‘Terminal Three’ katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere umo katika hatua za mwisho. Hakuishia hapo, rais alitutangazia kujenga reli ya kisasa. Nilidhani ni masihara, lakini matokeo nimeanza kuyaona. Mwenyezi Mungu atupe nini kama si zawadi ya kumpata Rais Magufuli kimiujiza na wapinzani wakibaki kubadilisha ‘gear’ angani wakati wenzao (CCM) wakibadilishia ardhini na sasa wanakwenda mwendokasi kuiletea Tanzania maendeleo endelevu?
Rais amebobea sana kwenye miundombinu hasa ya barabara tangu akiwa mtumishi kwenye serikali za awamu zilizotangulia. Sasa ameshika ‘usukani’ na chombo kinakwenda kwa kasi sana hata kidhibiti mwendo hakifui dafu na ‘maofisa usalama barabarani wako pembeni wanashangilia.’

Mathalani, kazi inayoendelea eneo la Ubungo ujenzi wa barabara za juu inatia moyo. Vilevile, kuanzia Kimara kwenda Mlandizi ujenzi wa njia sita yakiwamo madaraja; ni ishara kuwa Tanzania yenye mabadiliko inakuja.
Wakati huo huo, barabara za kupunguza misongamano jijini Dar es Salaam zinajengwa. Mfano, kutoka Mbezi mwisho kwenda Gongo la Mboto hata Mbagala imejengwa. Ujenzi wa barabara: Kimara – Korogwe kuelekea Tabata, Segerea, Kinyerezi; kutoka Mbezi Mwisho kupita Goba hadi Mbezi (Barabara ya Bagamoyo) imekamilika. Barabara kutoka Kimara Baruti kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imekamilika. Miundombinu maeneo mbalimbali ya Kariakoo na manispaa zote jijini humo inaendelea kuboreshwa. Isitoshe, kazi za ujenzi wa barabara karibu zinaendelea nchi nzima na mikoa yote imeunganishwa kwa barabara za lami. Hili ni jambo kubwa sana maana taifa letu ni kubwa mno ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Kwa mfano, kutoka Songea au Mtwara hadi Bukoba, Kigoma au Musoma ni kilometa nyingi, lakini maeneo hayo yameunganishwa kwa barabara za lami.

Miundombinu ya bandari inaendelea kuboreshwa ili kuhudumia meli nyingi kwa wakati mmoja. Meli zinakarabatiwa, mpya zinaundwa kwenye maziwa na vivuko vinajengwa na kuboreshwa. Daraja la Mto Kilombero limekamilika – ni rahisi kwenda Mahenge na Malinyi. Elimu bure inatolewa ingawa kuna changamoto kadhaa kwenye sekta ya elimu, lakini mwelekeo unatia matumaini.
Sehemu nilizobahatika kutembelea mikoani nimeshuhudia majengo ya zamani ya shule kongwe yamekarabatiwa. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimepata mabweni.
Majengo ya kutolea huduma vituo vya afya na zahanati yanaboreshwa nchi nzima. Takriban miezi mitatu iliyopita nilitembelea Wilaya ya Kilwa, niliona Kituo cha Afya Kilwa Masoko kimeboreshwa sana. Desemba 26, 2018 nilitembelea zahanati eneo la Bukuna, Tarafa ya Maruku, mkoani Kagera; kazi nzuri imefanyika. Nilipouliza haya yote maana yake nini, wakazi wa pale wakaniambia bila Rais Magufuli kuwa madarakani ingebaki historia tu. Ukiacha uboreshaji wa majengo, pia upatikanaji wa dawa umeimarishwa kupitia MSD chini ya Wizara ya Afya.

Rais akaona bila ya kuwapo umeme wa uhakika itakuwa vigumu kufikia uchumi wa viwanda. Akaamua Tanzania izalishe umeme wa uhakika kutumia maji ya Mto Rufiji. Mpango ulikuwepo miaka ya 1970, lakini haukuendelezwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo Vita ya Kagera. Rais amethubutu, amedhamiria na sasa tunasonga mbele ingawa vipo vikwazo kibao ndani na nje ya nchi kuhusu azima hii. Kazi yake rais naifananisha na mtazamo wa “Yes I can, I must, I will”, maana penye nia pana njia.
Uongozi ulio shupavu kuinua maisha ya walio wengi ni mtaji mkubwa kwa maendeleo yetu. Tukisimamia vizuri bila kuwepo ubinafsi, ubadhirifu na roho za wizi na udanganyifu hakuna kitakachotuzuia kutimiza azima yetu ya kujiletea maendeleo. Rais anatutia moyo anaposema: “Tanzania ni tajiri, yenye rasilimali za kutosha, hakuna sababu ya kujiona maskini.” Anaongeza: “Fedha zipo, kinachotakiwa ni kuzisimamia vizuri zikatumika ipasavyo, kwa kipindi kifupi maendeleo tutayaona.”
Niwaombe Watanzania wenzangu tumuunge mkono rais wetu kwa kulipa kodi ili afanye kweli kwa ajili yetu na vizazi vijavyo. Hakuna taifa lililojipatia maendeleo bila kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Mataifa yaliyoendelea miaka takriban 200 iliyopita walikuwa kama sisi; lakini kwa kujituma na kusimamia mambo yao ipasavyo leo tunawasifu. Tutumie rasilimali tulizonazo kwa hekima tukimtanguliza Mwenyezi Mungu. Tumche yeye, maana kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa. Bila maarifa na ufahamu wa kweli tutaangamia.

Rais ameonyesha mfano mzuri katika kuiletea maendeleo Tanzania. Hata hivyo, kuna kupigwa ‘vijembe’ hapa na pale. Si wote wanayafurahia maendeleo yetu, lakini tusikate tamaa. Wapo wanaopenda tuishi maisha ya kuwategemea wakati uwezo wa kujitegemea upo. Hata hivyo, watakaotaka kutuunga mkono wanakaribishwa bila masharti yoyote.
Nimalize kwa kuupongeza upinzani kwa kazi waliyoifanya kabla ya uchaguzi mwaka 2015. Naamini yote haya tunayoyashuhudia leo ni kutokana na chachu hiyo. Sasa kwa pamoja tuijenge Tanzania kwa faida ya wote. MWENYEZI MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Please follow and like us:
Pin Share