Atuzwa kwa kuisumbua Serikali (2)

Smaandaehemu iliyopita, viongozi wawili katika Tarafa ya Loliondo waliandika waraka kupinga hatua ya Maanda Ngoitiko ambaye ni kiongozi wa asasi ya Pastoral Women Council (PWC), kupewa tuzo ya Front Line Defenders Award for Human Rights inayotolewa na Shirika la The International Foundation For the Protection of Human Rights Defenders at Risk mjini Dublin, Ireland.

Wanapinga kwa maelezo kuwa Maanda amekuwa sehemu ya migogoro inayoendelea Loliondo kutokana na kupinga mambo mengi yanayofanywa na Serikali. Sehemu hii ya pili wanatoa mapendekezo wanayoamini yatasaidia kurejesha hali ya amani, utulivu na utangamano Loliondo.

 

Mapendekezo yetu

 Ili kukabiliana na tatizo la mifugo mingi kuzidi uwezo wa ardhi (carrying capacity), vijiji vya kata ya Oloipiri vinaiomba Serikali ichukue jukumu la kuhakiki mipaka ya vijii ili tuweze kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi na pia kupata vyeti vya vijiji na hatimaye kudhibiti uhamiaji haramu kutoka nchi jirani ya Kenya na vijiji vya kata zinazotuzunguka.

Ipo haja kwa Serikali kuangalia upya migongano ya sheria kuhusu ardhi na kurejea Sheria ya Wanyamapori, lakini vijiji vilazimishwe kufanya mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kulinda na kuendeleza uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vya leo na vijavyo.

Kwa muda mrefu sasa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikizuia wafugaji kupeleka mifugo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Ingawa tunakuabiliana na uzuizi huo kwa madhumuni ya kulinda mazingira na kuzuia ujangili, bado tunashauri wizara kujaribu kuruhusu wafugaji kuchunga katika eneo hilo katika kile kipindi cha kiangazi ambacho hakuna watalii wengi wanaotembelea hifadhi na wanyama wamehama katika mbuga hiyo, na wamehamia maeneo ya Hifadhi ya Maasai Mara na badala ya kutumia utaratibu wa kuchoma nyasi mbugani (controlled burning), wawaruhusu  kwa utaratibu maalumu wafugaji wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufanya malisho.

 Kwa kufanya hivi kutapunguza malalamiko kutoka kwa wafugaji na pia mifugo inaweza kabisa kuchangia pato la taifa kwa kiwango kikubwa kama mifugo itauzwa wakati muafaka, kama vile nchi za Botswana, Kenya na nchi nyingi za Afrika zinavyofaidika kutokana na mazao yatokanayo na mifugo kama nyama, ngozi na maziwa.

Serikali ichukue jukumu la kutoa onyo na hata adhabu kali pale inapostahili kwa viongozi wa mashirika haya yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna uhusiano chanya kati ya jamii na wawekezaji kwa manufaa yao binafsi.

Tunapendekeza kata na vijiji vyetu kufanya kazi na wawekezaji waliopo katika kata zetu na hata wale watakaojitokeza kutaka kuwekeza katika maeneo yetu yenye rasilimali zinazoweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wetu.

Tunaomba Serikali itusaidie kuwadhibiti wale wote watakao kuwa na madhumuni ya kuchafua kata zetu, kuwachafua wawekezaji wetu kupitia vyombo vya habari, mitandao na tovuti maana NGOs wamekuwa wakituharibia uhusiano wetu na wawekezaji.

Kwa ufupi, tunakubali na kutambua uwepo wa wawekezaji na tunaomba Serikali iwalinde wawekezaji wazuri waliopo katika kata na vijiji kwa ajili ya kuwaletea maendeleo jamii za kifugaji ndani ya maeneo ya uwekezaji.

Tunaishauri Seriali kupitia vyombo vyake, kufanya uchunguzi wa kina kukagua (audit) haya mashirika (NGOs) kwa kufuatilia miradi waliyoombea pesa na kulinganisha kama miradi hiyo inaendana na pesa walizopata kutoka kwa wafadhili kama njia mojawapo ya kuwadhibiti na kuhakikisha fedha wazipatazo kutoka kwa wafadhili zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Faida kutoka kwa Wawekezaji

Ni dhahri kuwa picha ambayo dunia imekuwa nayo juu ya Loliondo ni ile ambayo imewekwa na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo kwa kweli huweka sura hasi juu ya Tarafa ya Loliondo, kata na vijiji vyetu, lakini pia nchi kwa jumla.

Pia huu upotoshaji huenda kinyume cha jitihada za serikali za kukaribisha wawekezaji wenye tija kwa jamii kutoka pande mbalimbali za dunia.

Pia inaonesha dunia kuwa Loliondo ni eneo la hatari kwa wawekezaji na kwa sababu hii wawekezaji wengi wameamua kutoka katika maeneo yetu, kwa mfano, Nomads, Hoopoe, Buffalo n.k.

Kwa kuwa mashirika haya yamekuwa na nguvu sana na kusababisha kutujengea jina baya kwa tarafa yetu ya Loliondo na miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikitoweka kwa ajili ya malumbano yanayosababishwa na Maanda Ngoitiko wa PWC na washirika wake, kwa mfano, mwaka 2010 Balozi wa Marekani alifanya ziara kwa mwekezaji wa Kimarekani kupitia TCL na alikuwa ametoa ahadi ya kuangalia ni jinsi gani kwa kushirikiana na wawekezaji wanaweza kusaidia kuwekeza kwenye ufugaji, lakini kwa kuwa shirika hili la PWC nia yake ni kuendeleza maslahi binafsi, walimwandika vibaya Balozi wa Marekani katika mitandao ya kijamii na kusababisha balozi huyo kujitoa katika mchakato huo.

 Tungependa kueleza baadhi ya miradi iliyotekelezwa na wawekezaji katika maeneo yetu. Kwa mfano, kampuni ya OBC: Wamejenga Shule ya Sekondari Loliondo, upanuzi wa Hospitali ya Wasso na  misaada ya vitanda, magodoro, blanketi, shuka, uchimbaji visima vya maji, ujenzi wa daraja la Mto Pololeti, ajira kwa vijana, ujenzi ofisi za vijiji vya Kirtallo, Soit-Sambu na uchangiaji wa madawati 200 katika shule za msingi wilayani Ngorongoro; na kadhalika.

Thomson Safaris: Wamejenga madarasa kwa shule za misingi, nyumba za walimu, mabweni kwa wavulana na wasichana katika Sekondari ya Soit-Sambu, ujenzi wa nyumba ya walimu wa Sekondari ya Soit-Sambu, ujenzi wa zahanati ya Sukenya, nyumba za watumishi wa zahanati, uchimbaji wa visima vya maji kwa ajili ya zahanati na miradi ya vikundi vya maendeleo ya akina mama (COCOBA) na kadhalika.

 KIDUPO NGO: Ufadhili wa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari; na wa vyuo na ujenzi wa shule za misingi ya Orkuyane na Mama Sara Lopolun.

Tunasisitiza kuwa matatizo yatakapojitokeza ni sharti yatatuliwe na wananchi kwenye vijiji na kata husika, na siyo Maanda Ngoitiko na shirika lake kuyasemea au kujaribu kuyatatua kwa maslahi yao binafsi.

Tunasisitiza kuwa hatupo tayari tena kutengenezewa migogoro na Maanda Ngoitiko na shirika lake la PWC dhidi ya Serikali na wananchi, dhidi ya wawekezaji na wananchi, dhidi ya koo na koo, dhidi ya kijiji na kijiji na pia dhidi ya NGO na NGO.

Hivyo, tunawaomba viongozi wetu wa Serikali kuhakikisha kwamba tunalindwa katika jitihada zetu za kupata amani na kutafuta maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wetu.

 

Imeandaliwa na:

Diwani wa Kata ya Oloipiri, Wilaya ya Ngorongoro – Mheshimiwa William M. Alais na

Mkurugenzi wa Shirika la KIDUPO (Integrated Development Peoples’ Organization) – Ndugu Gabriel K. Olle Killel.